Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zambia chukua hatua kuepusha ukatili na mauaji ya watu wenye ualbino

Watu wenye ualbino mara nyingi wanakuwa na uoni hafifu na wanahitaji matunzo maalum ili waweze kujikinga na jua. (Maktaba)
Corbis Images/Patricia Willocq
Watu wenye ualbino mara nyingi wanakuwa na uoni hafifu na wanahitaji matunzo maalum ili waweze kujikinga na jua. (Maktaba)

Zambia chukua hatua kuepusha ukatili na mauaji ya watu wenye ualbino

Haki za binadamu

Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu wenye Ulemavu (CRPD)  imeeleza wasiwasi wake kuhusu mashambulizi, kukatwa viungo, kutekwa nyara na mauaji ya watu wenye ualbino nchini Zambia, na hivyo imesihi serikali ichukue hatua za haraka za kisera na kisheria kulinda kundi hilo.

Kamati hiyo imesema hayo katika ripoti yake iliyochapishwa leo huko Geneva, Uswisi, kuhusu haki za watu wenye ulemavu katika nchi 7 ikiwemo Zambia. Nchi zingine ni Azerbaijan, Bahrain, Costa Rica, Kazakhstan, Nicaragua na Sweden baada ya mapitio ya ziara za wataalamu wake kwenye nchi hizo.

Ripoti hiyo inajumuisha hofu, wasiwasi na mapendekezo ya jinsi ya kutekeleza Mkataba wa kimataifa wa Haki za watu wenye  ulemavu, CRPD, sambamba na mambo chanya ambayo yalipatikana kwenye ziara hizo.

Elimu, afya mashakani kwa watu wenye ualbino

“Kumekuweko na ripoti za ukatili dhidi ya watu wenye ualbino,” imesema ripoti hiyo na hivyo ripoti inataka “kuchukuliwa kwa hatua mahsusi za kisheria, kisiasa na kiutawala zenye lengo la kuwalinda watu wenye  ualbino na kuadhibu wale wote wanaosaka kuwanyanyasa na kuwafanyia ukatili.”

Kwa  upande wa elimu kwa watu wenye ualbino, ripoti imeelezea wasiwasi wake kuwa watoto wenye ualbino mara nyingi wanaenguliwa kwenye mfumo wa kawaida wa elimu na hivyo “watoto wenye ualbino wanawekwa kwenye shule maalum za watu wenye ulemavu wa kutoona na kufundishwa kwa kutumia maandishi ya nukta nundu.”

Hivyo basi ripoti hiyo inataka watoto hao wasiwekwe kwenye shule hizo na kulazimishwa kufundishwa maandishi ya nukta nundu, na badala yake wapatiwe msaada unaohitajika na malazi ndani ya mfumo wa kawaida wa elimu.

Ripoti pia imemulika afya ya watu wenye ualbino ikiwemo changamoto ya jua Kali kwenye ngozi na miwani hivyo inataka huduma ya afya imulike mahitaji yao muhimu.