Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wenye ualbino wapata madhara kutokana na mabadiliko ya tabianchi- Mtaalamu

Watu wenye ualbino mara nyingi wanakuwa na uoni hafifu na wanahitaji matunzo maalum ili waweze kujikinga na jua.
Corbis Images/Patricia Willocq
Watu wenye ualbino mara nyingi wanakuwa na uoni hafifu na wanahitaji matunzo maalum ili waweze kujikinga na jua.

Wenye ualbino wapata madhara kutokana na mabadiliko ya tabianchi- Mtaalamu

Haki za binadamu

Mabadiliko ya tabia nchi yanatajwa kuwa na madhara kwa watu wenye ualbino duniani kote, na kusababisha viwango vya juu vya vifo vitokanavyo na saratani ya ngozi katika baadhi ya kanda. 

Amesema hayo Mtaalamu Huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu watu wenye Ualbino Muluka-Anne Miti-Drummond wakati akiwasilisha ripoti yake ya mwaka mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo jijini New York, Marekani, akisema hali ni mbaya kiasi kwamba amekuwa akifanya kampeni bila kuchoka ili watu wenye ualbino wapewe mafuta ya kujikinga na jua ambalo sasa ni Kali kupita kiasi.  

Mafuta ya kuzuia jua si kipodozi bali ni dawa  

"Mafuta ya kuzuia madhara ya jua kwa watu wenye ualbino si bidhaa ya anasa bali ni bidhaa ya matibabu ya kuokoa maisha ambayo inaweza kurefusha na kuboresha ubora wa maisha kwa wengi ambao hawana uwezo wa kumudu," alisema mtaalamu huyo.  

Madhara makubwa ya mabadiliko ya tabianchi kwa watu wenye ualbino ni mojawapo ya mambo ambayo hayazingatiwi sana katika suala hili.  

Barani Afrika, inakadiriwa kuwa watu wenye ualbino wana uwezekano wa hadi mara 1000 zaidi wa kupata saratani ya ngozi kuliko wale ambao hawana, huku wengi wakifa wakiwa na umri wa miaka 40,” alisema Muluka-Anne Miti-Drummond.  

"Vifo vinaweza kuzuilika kwa kutumia mafuta bora ya jua na vifaa vya kujikinga ambavyo vinapatikana kwa urahisi kwa watu wenye ualbino, cha kusikitisha ni kwamba wengi wanaishi katika umaskini na hawawezi kumudu gharama ya bidhaa hizi,” Miti-Drummond alisema.  

Mafuta yajumuishwe kwenye orodha ya dawa muhimu  

Mtaalamu huyo na washirika wengine wamekuwa wakishawishi Shirika la Umoja wa Mataifa la afya (WHO) kuongeza tena mafuta ya jua kwenye orodha yake ya dawa muhimu, huku akitoa wito kwa Mataifa kufanya vivyo hivyo katika ngazi ya kitaifa.  

"Hili sasa ni la dharura zaidi kuliko wakati mwingine wowote wakati hali ya hewa ya joto inapoongezeka na mionzi ya UV inaongezeka, na kufanya jua kuwa hatari sana kwa watu wenye ualbino, hasa katika hali ya hewa ya joto," alisema.  

Watu wenye ualbino sio tu wanashambuliwa na saratani ya ngozi, lakini pia wana ulemavu wa kuona na kwa hivyo wanachukuliwa kuwa watu wenye ulemavu.   

"Inajulikana kuwa watu wenye ulemavu wanaathiriwa kwa kiasi kikubwa na majanga yanayohusiana na mabadiliko ya tabia nchi, wana uwezekano wa kufa mara nne katika majanga yanayohusiana na mabadiliko ya tabia nchi kuliko watu wasio na ulemavu,” mtaalamu huyo alisema.  

 Alibainisha kuwa majanga ya mabadiliko ya tabia nchi, yamesababisha watu wenye Ualbino kupoteza maisha yao, kufanya kazi kwa muda mrefu juani ili kukabiliana na uhaba wa chakula, na kuhama kutafuta hali ya hewa inayofaa zaidi kwa hali yao.  

Iman za kishirikina  

Miti-Drummond alionya juu ya jambo la kuhuzunisha linalohusisha mashambulizi ya kutisha na mauaji ya watu wenye ualbino, kutokana na imani potofu za kishirikina za wahusika kwamba ualbino ndio chanzo cha majanga ya mabadiliko ya tabianchi.   

"Baadhi ya mashambulizi na mauaji yanalenga kutumia viungo vya watu wenye ualbino katika matambiko kwa imani potofu kwamba hii italeta hali nzuri ya hewa au mavuno mazuri," alisema.  

Mtaalamu huyo alisisitiza wito wake wa kujumuishwa kwa watu wenye ualbino katika mikutano yote inayohusiana na mabadiliko ya tabianchi katika jamii zao mbalimbali na kuhakikisha wanashiriki katika kupanga, kudhibiti na kukabiliana na maafa.  

"Kutengwa sio chaguo. Mabadiliko ya hali ya hewa ni suala la maisha na kifo kwa watu wengi wenye ualbino,” Ametamatatisha Miti-Drummond.