Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Simulizi za raia wa Msumbiji wanaokimbia mashambulizi kaskazini mwa nchi

Familia zilizopoteza makazi yao katika majimbo ya kaskazini mwa Msumbiji yenye mgogoro wanaishi katika makazi ya muda. (Maktaba)
© UNHCR/Martim Gray Pereira
Familia zilizopoteza makazi yao katika majimbo ya kaskazini mwa Msumbiji yenye mgogoro wanaishi katika makazi ya muda. (Maktaba)

Simulizi za raia wa Msumbiji wanaokimbia mashambulizi kaskazini mwa nchi

Amani na Usalama

Hizi ni sauti za baadhi ya waliofurushwa katika makazi yao katika jimbo lenye utajiri mkubwa wa mafuta, Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji. Watu hawa kwa takribani miaka saba wamevumilia unyanyasaji unaotekelezwa na makundi yenye silaha.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi (UNHCR) linasema zaidi ya watu milioni moja walifurushwa na takribani 670,000 wamesalia bila makazi tangu mizozo ilipoanza katika jimbo hilo mwaka wa 2017. Wengi wamelazimika kuhama mara kadhaa kutafuta usalama.

Ines Ambrosio, mama anayelea watoto wake watatu bila mume alifurushwa kutoka katika Kijiji chake.

“Baada ya kuingia vita, vita imeingia usiku saa tano. Tumesikia bunduki zinalia. Hatukujua risasi zilikokuwa zinatokea. Tulikuwa tunasikia tu bunduki zinalia. Kila mtu akaanza kutoka anakimbia (akipiga kelele), vita jamani, vita jamani.”

Wakazi wengi wametafuta makazi katika vituo vya wakimbizi wa ndani katika ukanda huo ambako huduma za maisha zimelemewa. Ingawa UNHCR inajitahidi kusaidia, vituo mara nyingi vimefurika watu huku kukiwa na uhaba wa maji safi na salama na pia ukosefu wa mahali pa kujisafi.

Mwingine ni Eduarte Tumbati. Yeye kwa haraka alikikimbia kijiji chake akiwa na mkewe na watoto wao watatu baada ya kaka yake kuuawa kikatili na watu wenye kujihami kwa silaha,

“Washambuliaji walipofika, yule mke wakamkamata, mwanaume wakamfunga kamba. Wakapika chakula wakala. Sasa wakamwambia mke wa kaka yangu, mwangalie mumeo tunachotaka kumfanya. Wakamchinja. Mke wakamwambia kimbia. Mke akakimbia akaja nyumbani kutuambia.”

Watoto hapa wameshuhudia mambo ambayo hakuna mtoto angepaswa kuona. Usiku mara nyingi wanakuwa na majinamizi na wanaishi katika hofu ya kushambuliwa tena.

Wasia Suale anasema, “Watoto wangu wameniuliza na pia walikuwa wanasikia kuwa hapa nyumbani hapa amani. Na mpaka sasa wanajua kuwa sisi tulikuwa tumekimbia Al shabaab. Hata yule mdogo mpaka sasa anakumbuka kuwa baba alikuwa amenibeba tukikimbilia makokoni.”

Zaidi ya watu 600,000 wameamua kurejea nyumbani lakini ukosefu wa usalama katika baadhi ya jimbo la Cabo Delgado inaamaanisha bado wengi wanahitaji kulindwa na pia usaidizi wa kibinadamu lakini muhimu, mwishowe amani.