Dola Milioni 105 kunufaisha Mama na Mtoto Msumbiji

Constangelina Basílio mwenye umri wa miaka 23 alinususrika kifo akijifungua mtoto wake wa kiume Magalhães, na hapa anaeleza jinsi huduma za afya vijijini Musimbiji zilivyomsadia. Picha: UNFPA

Dola Milioni 105 kunufaisha Mama na Mtoto Msumbiji

Huduma ya msingi ya afya kwa mama na mtoto sasa itaimarika nchini Msumbiji baada ya Benki ya dunia kuidhinisha dola Milioni 105 kwa ajili ya kuipa serikali ya nchi hiyo.

Msaada huo wa kifedha unafuatia programu maalum ya miaka mitano iliyoanzishwa na Msumbiji kwa ajili ya kuwezesha kuboresha huduma za afya ambazo kwa sasa viko chini sana kwa mujibu wa viwango vya maendeleo ya binadamu vikishika nafasi ya 181 kati ya 188

Mwakilishi wa Banki ya Dunia nchini Msumbiji Mark Lundell,amesema wanataka kuona wananchi waliopembezoni wananufaika na mradi huo ambao fedha zake zitakuwa zinatolewa kidogo kidogo kulingana na maendeleo ya mradi

Kati ya dola hizo Milioni 105 dola milioni 80 zimetolewa na Muungano wa maendeleo – IDA na nyingine Milioni 20 zimetoka mfuko wa kimataifa wa uwezeshaji( GFF)

Utafiti wa hivi karibuni wa huduma za msingi za Afya umeonyesha Msumbiji bado haijafikia maendeleo endelevu kwenye sekta ya Afya huku upungufu mkubwa ukionekana kwenye utoaji huduma ya mama na mtoto, na kuna idadi kubwa ya wajawazito wanaoacha kwenda hospitali kupata huduma baada ya kujifungua.