Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kimbunga Gombe, Msumbiji, UNHCR na wadau wanaharakisha msaada kwa maelfu

Familia ya raia wa Burundi mbele ya nyumba yao iliyoharibiwa na kimbunga Gombe, katika makazi ya wakimbizi ya Maratane, Msumbiji.
© UNHCR/Juliana Ghazi
Familia ya raia wa Burundi mbele ya nyumba yao iliyoharibiwa na kimbunga Gombe, katika makazi ya wakimbizi ya Maratane, Msumbiji.

Kimbunga Gombe, Msumbiji, UNHCR na wadau wanaharakisha msaada kwa maelfu

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR pamoja na serikali ya Msumbiji na washirika wa kibinadamu, wanaharakisha kusaidia maelfu ya familia zilizoathiriwa na kimbunga cha Tropiki cha Gombe, ambacho kilipiga katika jimbo la Nampula mnamo tarehe 11 ya mwezi huu wa Machi na kuharibu nyumba, maji kufunika mashamba, na kuwalazimisha watu kuyakimbia makazi yao ili kutafuta usalama.   

Msemaji wa shirika hilo Boris Cheshirkov hii leo akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Usiswi ameeleza kuwa kimbunga ndio kimbunga Gombe ni kikali zaidi kuwahi kutokea nchini Msumbiji tangu kimbunga Idai na Kenneth viliposababisha maafa katika majira ya kuchipua mwaka wa 2019, na kuua mamia ya watu na wengine milioni 2.2 kuyahama makazi yao.  

Kimbunga Gombe kimeikumba Msumbiji chini ya miezi miwili baada ya Kimbunga cha Tropiki kwa jina Ana, ambacho kilitua kaskazini na katikati mwa Msumbiji tarehe 24 Januari, na kuathiri watu 180,869, kujeruhi watu 207 na kuua takribani watu 38, wengi wao wakiwa katika majimbo ya Zambezia, Nampula na Tete. 

Wakati nguvu na athari za Kimbunga Gombe zikionekana kuwa kali zaidi kuliko Idai na Kenneth, dhoruba hii ya aina ya 4 ilileta upepo mkali wa hadi kilomita 190 kwa saa na mvua za mara kwa mara na radi, kuharibu miundombinu muhimu na kukata umeme na mawasiliano katika Jiji la Nampula, pia katika  makazi ya wakimbizi ya Maratane yaliyo karibu na maeneo yanayohifadhi wakimbizi wa ndani (IDPs) kutoka jimbo la Cabo Delgado. 

Bwana Cheshirkov ameeleza kuwa zaidi ya watu 380,000 wameathirika katika jimbo la Nampula pekee, kwa mujibu wa taarifa za mamlaka za mitaa, ikiwa ni pamoja na maelfu ya watu waliokimbia makazi yao. “Wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu, ikiwa ni pamoja na vifaa vya makazi ili kujenga upya nyumba zilizoanguka wakati wa kimbunga.” 

Miongoni mwa walioathiriwa ni mkimbizi wa Burundi na mama wa watoto watatu asiye na mume ambaye aliiambia UNHCR kwamba familia yake ilikimbilia kwenye nyumba ya jirani katika kazi ya Maratane baada ya nyumba yao kuharibiwa. Kijana mmoja alisema mazao yake yameharibiwa na dhoruba hiyo na hivyo kumuacha na hofu kwamba hataweza kujikimu yeye na familia yake ya watu wanne. 

UNHCR inaratibu makazi yanayohitajika haraka na vitu vingine muhimu kutoka kwenye hifadhi zake ili kusaidia wakimbizi 62,000, wakimbizi wa ndani na wanajamii wenyeji. 

Miundombinu kadhaa ya kimsingi pia iliharibiwa katika makazi ya Maratane ambayo huhifadhi wakimbizi 9,300 kama vile shule ya msingi, kituo cha afya, maghala ya UNHCR, kituo cha mpito na mfumo wa umwagiliaji. Ufadhili zaidi unahitajika ili kuhakikisha ukarabati huo unaweza kufanywa ili huduma za kimsingi kwa wakimbizi zisikatishwe. 

Kama kiongozi wa Ulinzi wa watu, UNHCR na washirika wanatembelea vituo vya malazi ambavyo hukaribisha familia mpya zilizofurushwa ili kutathmini mahitaji yao kuanzia malazi, chakula na huduma ya afya hadi ulinzi dhidi ya unyonyaji na unyanyasaji wa kijinsia (PSEA), pamoja na huduma za afya ya akili na kisaikolojia. “Zaidi ya hayo, tunajitahidi kuwapa wakimbizi wa ndani upataji wa hati za kiraia, ambazo wengi walipoteza walipokuwa wakikimbia nyumbani.” Ameeleza Bwana Cheshirkov. 

UNHCR inasema kila eneo la dunia linakabiliwa na hatari za tabianchi. Vimbunga na dhoruba nyingine zinaongezeka mara kwa mara na kali, mafuriko yana nguvu zaidi, ukame unaongezeka, na moto wa nyika unazidi kuharibu. 

Mabadiliko ya tabinchi yanayotokana na binadamu yanaongezeka kwa kasi, na tayari yanasababisha usumbufu hatari na ulioenea kwa asili na watu. Wale walio na uwezo mdogo wa kukabiliana na hali hiyo ndio walioathirika zaidi, wakiwemo wakimbizi, wakimbizi wa ndani na wasio na utaifa. Wanawake, watoto, wazee, watu wenye ulemavu, na watu wa kiasili wameathirika kwa kiasi kikubwa. Zaidi ya asilimia 80 ya wakimbizi na wakimbizi wa ndani wanatoka katika nchi zenye mazingira magumu zaidi ya tabianchi duniani kote.