Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP: kuna uhaba wa chakula mashariki mwa DRC

Ugawaji wa dharura wa chakula unaendelea Mashariki mwa DRC. (Maktaba)
© WFP/Michael Castofas
Ugawaji wa dharura wa chakula unaendelea Mashariki mwa DRC. (Maktaba)

WFP: kuna uhaba wa chakula mashariki mwa DRC

Msaada wa Kibinadamu

Umoja wa Mataifa unasema wananchi milioni 23.4 sawa na robo ya wananchi wote takriban milioni 96 wa Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC, wanakabiliwa na njaa. Wengi wa wananchi hao wanaishi katika hali duni na yenye msongamano wa watu wasio na uwezo wa kupata chakula, huduma za afya na elimu.

Miaka nenda, miaka rudi katika eneo la mashariki mwa DRC, suala la ulinzi na usalama limekuwa vinywani mwa wengi ulimwenguni kwani usalama ndio bidhaa adimu zaidi. Hali imekuwa tete zaidi kuanzia miaka mitatu iliyopita. Maisha ya kila siku yanahusisha kuona wanajeshi wakipita wakifanya doria au wakiwa mitaani ili kulinda raia na mali zao. 

Wananchi nao ambao wamekuwa wakifanya shughuli mbalimbali kama vile kilimo ili wajipatie mazao ambayo mengine wangeweza kula na mengine kupeleka sokoni kwa ajili ya kuuza na kujipatia kipato, mara nyingi wamejikuta wakishindwa kabisa kufanya hivyo kwani makundi ya waasi wenye silaha wanapoibuka tu na kuanza kushambulia vijiji, raia hunyanyua vile wanavyoweza kubeba na kuanza safari ya kusaka usalama. Haya ndio maisha ya wengi. 

Taswira kutoka angani inapeleka katika kambi ya wakimbizi ya Bulengo iliyoko Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini. Mji huu unapakana na mji wa Rwanda wa Gisenyi. 

Video ya shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa Chakula duniani WFP inaonesha kambi ya wakimbizi ya Bulengo. Hapa idadi ya watoto inaonekana kuwa kubwa, watoto wakileana wenyewe. 

Vibanda vilivyofunikwa na maturubai meupe na vichache ndio vimejengwa na mabati juu mpaka chini. Kwingine mkimbizi mmoja anajenga kibanda chake kwa kutumia vijiti na makaratasi  ya nailoni. 

WFP inasema ndani ya kipindi cha miezi miwili pekee idadi ya wakimbizi katika eneo la Goma imeongezeka kwa takriban watu milioni moja. Wakimbizi wapya waliofika hapa wanaonekana wakijenga malazi kwa kutumia vipande vya plastiki na vijiti vya mbao. Mmoja wa wakimbizi wapya ni Lumoo Msabia Furaha. 

“Tumekimbia vita, tumetoka Sake ambako kulikuwa kunarindima risasi na mabomu, nilikimbia na watoto sita, nimefika hapa kwa sasa tunanjaa bado hatujapata msaada na tunakosa jinsi ya kufanya.” Amesema Lumoo. 

Hali kama ya Lumoo inawasibu wengi wanaofika hapa, mmoja wapo ni msichana Asifiwe Vumilia Shukuru ambaye anaonekana kukata tamaa kabisa, akiwa amemshikilia mtoto wake anayepimwa utapiamlo na kipimo kikionesha mtoto yupo kwenye alama nyekundi ikimaanisha kuwa anahitaji msaad wa haraka sana ili kuokoa maisha yake na mama yake huyo huku machozi yakimlenga anasema, 

“Hali ya mtoto wangu inaniogopesha sana, nina wasiwasi sana kumuona mtoto akiwa hivi, mtoto kuwa hivi inamaanisha malisho ni madogo. Jana waliniambia nimpeleke Kichero kisha nikatetemeka, sina nguvu. Maisha yakibadilika hata mwezi mmoja yakawa bora nitashukuru Mungu kwasababu hapa hata nikienda kukata kuni ili niuze ninamuachia mtoto wangu mtoto mwingine na nikirudi nakuta vile walivyolala nyumbani ndio hivyo hivyo hawajala.” 

Ama hakika baada ya kupumua kutoka kilio cha kuokoa maisha kutokana na vita sasa ni kilio cha kusaka chakula. 

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaendelea na utoaji wa misaada ya kibinadamu katika eneo hili hata hivyo ufinyu wa fedha inamaanisha Shirika la UN la mpango wa chakula wanalazimika kuchagua nani apate chakula na nani akose hususan katika eneo hili la mashariki ambako mahitaji ya kibinadamu yanazidi kuongezeka

Msemaji wa WFP Shelley Thakral anasema wanahitaji dola milioni 548.5 ili kuweza kushughulikia mahitaji ya DRC.

“Mzozo bado haujaisha kwa miaka tatu.  Watu wamelazimika kuzikimbia nyumba zao, ardhi zao, sio mara moja, sio mara mbili, lakini mara nyingi. Sisi, kama Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, inabidi tuwepo ili kutoa msaada wa chakula, kutoa fedha, ili kuhakikisha kwamba familia hizi hazikabiliwi na njaa… akina mama hawa, hawageuki nyuma na kuwaeleza watoto wao sina chakula cha kulisha familia. Na pia, tunapaswa kuendelea kuiambia jumuiya ya kimataifa, wasikate tamaa na watu hawa, msiwapuuze watu hawa, msiruhusu hali hii kuvumiliwa.”