Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yalaani vikali mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine 

Miji kote Ukrainia, ikiwa ni pamoja na Dnipro (pichani), ilishambuliwa kwa mabomu sana katika kipindi cha sikukuu. ( Maktaba)
© UNOCHA/Oleksii Holenkov
Miji kote Ukrainia, ikiwa ni pamoja na Dnipro (pichani), ilishambuliwa kwa mabomu sana katika kipindi cha sikukuu. ( Maktaba)

UN yalaani vikali mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali mashambulizi makubwa ya leo ya makombora na ndege zisizo na rubani yaliyotekelezwa na Urusi kwenye miji na maeneo mbalimbali ya nchi ya Ukraine 

Taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari na Naibu Msemaji wake Farhan Haq, kutoka jijini New York Marekani imeeleza kuwa mashambulio hayo dhidi ya raia, nishati na miundombinu mingine muhimu yanaripotiwa kuua na kujeruhi raia wengi na kusababisha uharibifu mkubwa, ikiwa ni pamoja na Kiwanda cha Umeme wa Maji cha Dnipro katika mkoa wa Zaporizhzhia, na kuwaacha zaidi ya Waukraine milioni moja bila huduma ya umeme na maji huko Kharkiv, Kryvyi Rih na Zaporizhzhia. 

 Katibu Mkuu amesikitishwa na kuendelea kwa mauaji na uharibifu, na kwa mara nyingine tena amesisitiza kwamba mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia yanakiuka sheria za kimataifa za kibinadamu. 

Taarifa hiyo imehitimisha kwa kukemea vitendo hivyo kuwa havikubaliki na lazima viishe mara moja.