Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN: Idadi ya raia waliouawa Ukraine yavuka 10,000

Watu walitembelea eneo katika kijiji cha Hroza ambapo raia walipoteza maisha yao hivi karibuni katika shambulio la kombora.
© Yevhen Nosenko
Watu walitembelea eneo katika kijiji cha Hroza ambapo raia walipoteza maisha yao hivi karibuni katika shambulio la kombora.

UN: Idadi ya raia waliouawa Ukraine yavuka 10,000

Amani na Usalama

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kufuatilia Haki za Kibinadamu nchini Ukraine (HRMMU) umesema tangu kuanza kwa vita kati ya Urusi dhidi ya Ukraine tarehe 24 Februari 2022 zaidi ya raia 10,000 wamepoteza maisha nchini Ukraine kati yao watoto wakiwa ni 560 na zaidi ya 18,500 wamejeruhiwa. 

Katika taarifa iliyotolewa hii leo na ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR imemnukuu Mkuu wa tume hiyo Danielle Bell Mkuu akisema, “Vifo elfu kumi vya raia ni hatua mbaya kwa Ukraine. "Vita vya Urusi dhidi ya Ukraine, vina hatari ya kubadilika na kuwa mzozo wa muda mrefu, huku gharama kubwa ya binadamu ikiwa chungu kueleweka.”

Mkuu huyo wa HRMMU ameeleza kuwa tume yao kabla ya kutaja idadi hiyo wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali kuthibitisha na kwamba idadi halisi ya vifo vinawea kuwa kubwa zaidi ya 10,000 kutokana na changamoto na muda unaohitajika kwa ajili ya kufanya uhakiki.

Shambulio la hivi karibuni

Tarehe 15 Novemba, watu wanne waliuawa wakati kombora lilipopiga jengo la ghorofa nne katika kijiji cha Selydove huko Oblast Donetsk, katika eneo linalodhibitiwa na Ukraine, na kusukuma jumla ya waliouawa kuwa zaidi ya 10,000. Miongoni mwa waliopoteza maisha ni familia akiwemo bibi wa miaka 85. 

Familia hii hapo awali ilikimbia eneo walilokuwa wakiishi na Kwenda kupata hifadhi eneo hili jipya waliloshambuliwa.

HRMMU imesema tukio la wiki iliyopita huko Selydove ni mfano wa kawaida wa mashambulizi ambayo kwa sasa yanasababisha vifo vya raia.

Katika kipindi cha miezi mitatu ya hivi karibuni, (mwezi Agosti mpaka Oktoba), vifo vingi vya raia vilivyothibitishwa - asilimia 86 - vilitokea katika eneo linalodhibitiwa na serikali. 

Bell ameonya kuwa “Takriban nusu ya vifo vya raia katika miezi mitatu iliyopita vimetokea mbali na mstari wa mapigano. Matokeo yake, hakuna sehemu yoyote nchini Ukraine iliyo salama kabisa,”.

HRMMU wamesema katika ufuatiliaji wao wameona idadi kubwa ya vifo vya raia vinatokea mbali zaidi ya eneo la mapigano, hasa kutokana na vikosi vya Urusi kurusha makombora ya masafa marefu na mengine kurushwa kwenye maeneo yenye watu wengi sehemu mbalimbali nchini kote.