Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchini Yemen UNICEF yatumia watoto kuhamasisha jamii kupata chanjo

Mtoto Leen mwenye umri wa miaka 10 kutoka nchini Yemen ambaye anahamasisha jamii kuhakikisha watoto wenzake wamepatiwa chanjo.
UNICEF Yemen
Mtoto Leen mwenye umri wa miaka 10 kutoka nchini Yemen ambaye anahamasisha jamii kuhakikisha watoto wenzake wamepatiwa chanjo.

Nchini Yemen UNICEF yatumia watoto kuhamasisha jamii kupata chanjo

Afya

Katika kuhakikisha watoto wanapata chanjo zote zinazohitajika, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF nchini Yemen limekuja na mbinu ya kutumia watoto kuhamasisha jamii kupeleka watoto kupata chanjo.

Mtoto Leen mwenye umri wa miaka 10 kutoka nchini Yemen, anasema kupitia mpango wa ufadhili wa mtoto, programu inayotumia watoto kwenda kuhamasisha jamii kupata chanjo ili wawe na afya bora amefanikisha watoto 150 kupata chanjo katika jamii yake.  

Akieleza hasa jumuku lake Leen anasema ‘Nawasisitiza walezi, umuhimu wa kupata chanjo na pia nacheza na watoto pale wanapokuwa wanachomwa sindano za chanjo ili kuwafanya wajisikie vizuri”

Katika kipindi cha miaka mwili UNICEF imefanikiwa kuwapatia mafunzo watoto 1000 ambao kwa pamoja wamefanikiwa kushawishi watoto 33,000 kupatiwa chanjo. 

Mtoto akipatiwa chanjo nchini Yemen katika kliniki ambayo inashirikisha watoto kama Leen (kulia akiketi) kuhamasisha jamii kuhusu chanjo kwa watoto.
UNICEF Yemen
Mtoto akipatiwa chanjo nchini Yemen katika kliniki ambayo inashirikisha watoto kama Leen (kulia akiketi) kuhamasisha jamii kuhusu chanjo kwa watoto.

Watoto hao kama Leen huambatana na mtu mzima ambaye ni muhamasishaji wa jamii kwenda kuhamasisha familia kuhusu chanjo za kawaida ambazo watoto wanapaswa kupata. 

Mmoja wa waliohamasishwa na mtoto Leen ni Somaia Mohammed, mama wa watoto watatu.

“Nilikuwa najizuia kwenda kuwapatia chanjo watoto wangu, hata hivyo baada ya Leen kunitembelea nyumbani kwangu baada ya mtoto wangu kuugua surau na kunielezea kama ningekuwa nimewapatia chanjo watoto wangu wasingeugua kiasi hicho nilihamasika na ushauri wao na kutembelea kituo cha afya kuwapatia chanjo watoto wangu.” 

Na mtoto Leen anafurahi kuona jirani yake Somaia na watoto wake watatu wamepata chanjo baada ya kumtembelea mara kadhaa.

Anasema kati ya mambo aliyokuwa akimwambie wakati akienda kumhamasisha alikuwa akisema “Angalia nilivyo na afya bora na nilivyo na nguvu naweza kwenda shuleni sababu nimepata chanjo zote zinazohitajika”