Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni ya kuhakikisha chanjo kwa watoto yalenga kuimarisha afya Kenya

Mama na mwana wapewa chanjo. Chanjo nyingi hutokea baada ya milipuko ya magonjwa  kama vile Polio, Kipindupindu na magonjwa mengine.
UNICEF/ Nangyo
Mama na mwana wapewa chanjo. Chanjo nyingi hutokea baada ya milipuko ya magonjwa kama vile Polio, Kipindupindu na magonjwa mengine.

Kampeni ya kuhakikisha chanjo kwa watoto yalenga kuimarisha afya Kenya

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF nchini Kenya kwa kushirikiana na serikali ya Kenya kupitia wizara ya afya na Muungano wa chanjo ulimwenguni,weendesha kampeni kwa ajili ya kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo muhimu kwa ajili ya kuzuia magonjwa.

Kampeni hiyo ikipewa jina, Linda kila mtoto. Hakikisha wamekamilisha chanjo zote! inachagiza wazazi kupeleka watoto kupata chanjo kwa ajili ya kuzuia magonjwa ikiwemo, polio, surua, kifua kikuu, homa ya ini, kichomi na magonjwa mengine. 

Jackline Juma ni mama mwenye mtoto mchanga,“Nafurahi sana wakati nikimleta mtoto wangu kupokea chanjo, kwa sababu nikimleta inapunguza idadi ya mara ambazo anaumwa, anakuwa na furaha na kwa kumuona mwanangu katika hali hii nami nakuwa na furaha.”

Kampeni inachagiza wazazi ikiwemo akina baba kufuatilia hali za watoto wao, James Otieno ni baba mzazi ambaye yeye na mkewe wamekuwa wakileta mwanao kupokea chanjo,“Ni vizuri kwa wazazi wao kudhamiria na kujihushisha kikamilifu licha ya mazingira magumu.”

Chanjo ambazo zinapatiwa kwa watoto ni za bila malipo kuanzia umri wa miaka sufuri hadi miaka mitano ambapo chanjo ya kwanza ni wakati ana umri wa kati ya siku moja hadi wiki mbili mpaka atakapotimia miaka mitano. Katika miaka miwili ya awali mtoto anahitaji kuhudhuria kliniki kila mwezi kwa ajili ya vipimo vya kutathmini ukuaji na kupokea dozi ya vitamini A kila miezi sita.

Katika vituo vya afya wazazi wanapokea mafunzo ya namna ya kumuangalia mtoto ikiwemo pia kuzingatia lishe bora.

Kampeni inachagiza watu mbali mbali kwenye jamii kuchukua wajibu wa kuhakikisha afya bora kwa watoto kwani, watoto wenye afya ni jamii yenye afya.