Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Faida isiyo halali ya dola bilioni 236 yapatikana kutokana na utumikishaji binadamu, waajiriwa wakisalia hohehahe - ILO

ILO inasema faida isiyo halali ya dola bilioni 236 yapatikana kutokana na utumikishaji binadamu, waajiriwa wakisalia hohehahe
© UNICEF
ILO inasema faida isiyo halali ya dola bilioni 236 yapatikana kutokana na utumikishaji binadamu, waajiriwa wakisalia hohehahe

Faida isiyo halali ya dola bilioni 236 yapatikana kutokana na utumikishaji binadamu, waajiriwa wakisalia hohehahe - ILO

Ukuaji wa Kiuchumi

Utumikishaji binadamu kwenye sekta ya uchumi binafsi ikiwemo biashara ya ngono, viwandani na kwenye mashamba huingiza dola bilioni 236 za faida isiyo halali kila mwaka, imesema ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO.

Ikipatiwa jina Faida na Umaskini: Uchumi wa utumikishajiripoti inakadiria kuwa faida hiyo imeongezeka kwa dola bilioni 64 sawa na asilimia 37 tangu mwaka 2014, ongezeko likichochewa na ongezeko la idadi ya watu wanaotumikishwa, na faida kubwa itokanayo na utumikishaji binadamu kwenye sekta mbali mbali. 

Ukokotozi wa faida isiyo halali

Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Tathmini ILO Michaelle De Cock amesema utumikishaji uko kwenye sekta ya umma na ile ya binafsi lakini ile ya umma ni asilimia 27 ilhali sekta binafsi ni asilimia 73.

Amefafanua maana ya faida isiyo halali kuwa ni kiwango cha fedha kinachosalia baada ya kuondoa ujira wa mtumikishwaji kwenye thamani halisi ya kazi aliyoifanya.

Ulaya na Asia zaongoza kwa faida zisizo halali, biashara ya ngono yaongoza

Mapato ya mwaka yasiyo halali kutokana na utumikishaji yalikuwa ya juu zaidi Ulaya na Asia ya Kati kwa dola bilioni 84, Asia na Pasifiki zikishika nafasi ya pili kwa dola bilioni 62, Amerika ya tatu dola bilioni 52 huku Afrika ikichukua nafasi ya nne kwa dola bilioni 20 na nchi za kiarabu dola bilioni 18. 

Watumikishaji hujipatia dola 10,000 kwa kila muathiriwa, ikiwa ni ongezeko kutoka dola 8,269 muongo mmoja uliopita.

Utumikishaji kwenye biashara ya ngono ndio unabeba asilimia 73 ya faida yote isiyo halali licha ya waathiriwa kwenye sekta hiyo wakiwa ni asilimia 27 tu ya watumikishwaji wote. 

Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Tathmini ILO Michaelle De Cock.
UN Video
Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Tathmini ILO Michaelle De Cock.

Utumikishaji wazidi kutwamisha wengi kwenye lindi la  umaskini- Houngbo

Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa ILO Gilbert F. Houngbo amesema “utumikishwaji kwenye ajira unaendelea mzunguko wa umaskini na unyonyaji na unatokomeza na kurarua utu wa kibinadamu. Tunafahamu imezidi kuwa mbaya. Jamii ya kimataifa lazima iungane ichukue hatua kumaliza ukosefu huu wa haki.” 

Ripoti inasema duniani kote kwa siku moja mwaka 2021 kulikuweko na watu milioni 27.6 waliokuwa wanatumikishwa. Hii ina maana katika kila watu 1000 duniani, watu 3.5 wanatumikishwa kila siku.

“Watu wanaotumikishwa hukabiliwa na aina mbali mbali ya machungu, na changamoto ikiwemo ujira wao kushikiliwa na mwajiri.

Nini kifanyike sasa? Sheria pekee hazitoshelezi

Ripoti inataka uwekezaji wa haraka kwenye usimamizi wa mikakati ya kuzuia usafirishaji wa fedha haramu zitokanazo na faida zitokanazo na utumikishaji haramu wa binadamu na wahusika wawajibishwe.

Imependekeza pia kuimarisha mifumo ya sheria kwa kupatia mafunzo maafisa wa ukaguzi kwenye maeneo ya kazi, halikadhalika uratibu mzuri kati ya taasisi za usimamizi wa shreia za ajira na uhalifu.

Ingawa hivyo, ILO inasema utumikishaji kwenye ajira hauwezi kutokomezwa kupitia usimamizi wa sheria pekee, bali pia kupatia kipaumbele hatua za kushughulikia mizizi au visababishi na kulinda manusura na waathiriwa.