Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ever Given yanasuliwa kutoka mfereji wa Suez, UNCTAD yazungumza 

Ilichukua siku kadhaa kwa meli hii Ever Given kuweza kunasuliwa kutoka kwenye mfereji wa Suez ambako ilinaswa kwa wiki nzima.
Suez Canal Authority
Ilichukua siku kadhaa kwa meli hii Ever Given kuweza kunasuliwa kutoka kwenye mfereji wa Suez ambako ilinaswa kwa wiki nzima.

Ever Given yanasuliwa kutoka mfereji wa Suez, UNCTAD yazungumza 

Ukuaji wa Kiuchumi

Hatimaye meli kubwa ya mizigo, Ever Given ambayo ilikuwa imekwama kwa wiki moja kwenye mfereji wa Suez huko kaskazini mwa Afrika imenasuliwa baada ya jitihada kubwa za kuinasua, huku ikielezwa kuwa itachukua miezi kadhaa kukabili hasara ya mkwamo wake katika biashara duniani.
 

Ever Given imenasuliwa baada ya kuchimbwa kwa mchanga na kunasua meli hiyo yenye kina cha futi 1,300 kutoka kwenye kuta za mfereji wa Suez ambao unaunganisha ukanda wa Ghuba na bara la Ulaya.
Jan Hoffman ambaye ni mtaalamu wa masuala ya usafiri majini kwenye kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa ,UNCTAD amesema hayo akihojiwa na Daniel Johnson wa Idhaa ya Kiingereza ya Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi.

Yaelezwa kuwa mkwamo wa meli hiyo ya mizigo unaweza kusababisha kuporomoka kwa asilimia 40 kwa usafirishaji wa shehena kutoka Asia kwenda Ulaya mwezi ujao wa Aprili.

Kufuatia kunasuliwa kwa meli hiyo, Bwana Hoffman amesema tayari meli ndogo zimeweza kupita, lakini meli kubwa tayari zilikuwa zimegeuka na kuelekea njia ya Cape of Good Hope nchini Afrika Kusini, safari ambayo ni ndefu ambayo italazimu meli kubwa kusafiri kwa kasi zaidi kumudu muda ambao zimepoteza na hivyo kuongeza uchafuzi zaidi wa hali ya hewa.

Meli ya Ever Given ilipokuwa imenasa kwenye mfereji wa Suez na kuzua sintofahmu kwenye mwelekeo wa biashara duniani.
Suez Canal Authority
Meli ya Ever Given ilipokuwa imenasa kwenye mfereji wa Suez na kuzua sintofahmu kwenye mwelekeo wa biashara duniani.

Alipoulizwa ni bidhaa gani zilizomo kwenye meli hiyo, Bwana Hoffman amesema, “kwa sisi wa hapa barani Ulaya, asilimia takribani 20 ya kile tunachokula na kunywa au kuva kinapitia mfereji wa Suez, na baadhi ya bidhaa kama vile vifaa vya kieletroniki, ofisini, vitambaa itabidi kama mtu ameagiza kupitia mtandaoni, itabidi ajiandae kusubiri kwa muda.” 

Kuhusu athari za kuchelewa kwa bidhaa hizo afisa huyo wa UNCTAD amesema bei zitaongezeka zaidi kwa kuzingatia kuwa, “gharama ya usafirishaji tayari ilishaongezeka kulinganishwa na miongo iliyopita kutokana na janga la COVID-19, na zilianza kupungua wiki chache, lakini sasa zitapanda tena.”

Ametaja sababu nyingine ya kuongezeka kwa bei ni upungufu wa kontena au makasha ya kusafirishia shehena akisema “hivi sasa hakuna kontena za kutosha duniani. Kama sasa hizo meli zilikuwa mfereji wa Suez, na pia huko California kuna meli zina shehena za kontena, kwa hiyo hali hiyo imesababisha gharama za kukodisha kontena kuongezeka. Eneo lingine ni njia ya China kwenda Amerika ya Kusini.”

COVID-19 imeleta ukosefu wa mizania kwenye biashara

Mtaalamu huyo wa UNCTAD ameenda mbali kuelezea kuwa janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 nalo limebadili mwenendo wa biashara duniani kwa kuwa hivi sasa mahitaji ya bidhaa yamebadilika, “idadi ya watu wanaokula mgahawani imepungua, watu siyo wengi wanaokwenda kwa vinyozi au saloni kwa ajili ya kutengenza nywele, na kwenye bandari nako kasi ya upakuaji wa shehena imepungua, makuli wanakuwa labda wamebainika kuwa na virusi vya Corona, kwa hiyo inachukua muda mrefu zaidi kupakua.”

Halikadhalika kuna nakisi ya biashara kati ya China ya Marekani, kontena nyingi zinaondoka tupu kutoka Marekani.

Nchi zinazoendelea na zile za visiwani zalipa gharama maradufu

Akifafanua zaidi kuhusu ni maeneo yapi yameathirika zaidi na mwenendo wa biashara duniani, Bwana Hoffman amesema nchi zinazoendelea na zile za visiwa vidogo hivi sasa zinalipa gharama maradufu za kusafirisha mizigo kuliko nchi tajiri sababu ikiwa ni pamoja na ukosefu wa uwekezaji wa kutosha katika miundombinu ya upakuaji wa shehena na ufuatiliaji, jambo ambalo amesema UNCTAD hivi sasa inaangalia jinsi ya kusaidia nchi hizo kuboresha bandari zao.