Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa ni rasmi, 2023 ulivunja rekodi zote za joto duniani-WMO

Majanga yatokanayo mafuriko yanababisha usumbufu, majeruhi wengi na hasara kubwa za kiuchumi katika sehemu mbalimbali za dunia.
Dinga Bienvenue/Congo National Hydrological Service
Majanga yatokanayo mafuriko yanababisha usumbufu, majeruhi wengi na hasara kubwa za kiuchumi katika sehemu mbalimbali za dunia.

Sasa ni rasmi, 2023 ulivunja rekodi zote za joto duniani-WMO

Tabianchi na mazingira

Mwaka 2023 ulikuwa mwaka wenye joto zaidi duniani katika rekodi zote zilizowahi kunukuliwa, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la hali ya hewa duniani, WMO katika ripoti yake iliyotolewa hii leo huko Geneva, Uswisi.

“Rekodi zimevunjwa, katika baadhi ya maeneo kwa kiwango kikubwa katika viwango vya hewa chafuzi, viwango vya joto ardhini, viwango vya juu vya tindikali na joto baharini, ongezeko la kiwango cha maji ya bahari na kupungua kwa barafu na theluji huko ncha ya  kusini mwa dunia au Antarctic,” imesema taarifa ya WMO kutoka Geneva.

Kama hiyo haitoshi mikondojoto baharini, mafuriko, ukame, mioto ya nyika na kasi kubwa ya vimbunga kwenye maeneo ya kitropiki vyote vimesababisha zahma na machungu na kuweka rehani maisha ya mamilioni ya watu, huku nazo nchi zikikumbwa na hasara za kiuchumi za mabilioni ya dola.

Kauli ya Katibu Mkuu UN

“Ving’ora vinalia katika kila viashiria… baadhi ya rekodi za awali si kwamba zinaongezeka bali zinavunja rekodi,” amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa MAtaifa António Guterres kupitia ujumbe wake wa video aliotoa wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo.

Kiwango cha joto mwaka 2023 kwa wastani kiliongezeka kwa wastani wa nyuzi joto 1.45 katika kipimo cha Selsiyasi ikilinganishwa na kabla ya mapinduzi ya viwanda. Ulikuwa ni mwaka wa kumi mfululizo kwa kiwango cha juu cha joto, imesema ripoti hiyo.

Kwa mwendo huu Mkataba wa Paris njiapanda- Saulo

“Kamwe hatujawahi kukaribia kabisa angalau kwa sasa kiwango cha nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi kwa ambacho hatupaswi kuvuka kwa mujibu wa mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi,” amesema Katibu Mkuu wa WMO, Celeste Saulo akiongeza kuwa WMO inatoa tahadhari kwa dunia.

“Mabadiliko ya tabianchi ni zaidi ya joto. Kile tulichoshuhudia mwaka 2023, hususan na viwango vya juu vya joto baharini, kupungua kwa barafu na theluji Antarctic ni jambo la kutia hofu kubwa,” amesema Bi. Saulo.

Joto la bahari liliharibu mifumo anuai na ile ya uzalishaji chakula. Mwishoni mwa mwaka 2023, asilimia 90 ya eneo la baharí katika kipindi fulani lilikumbwa na mazingira ya mikondo joto.

Katibu Mkuu huyo wa WMO anasema janga la tabianchi ndio changamoto inayokumba ubinadamu hivi sasa na inaenda sambamba na ukosefu wa usawa kutokana na ongezeko la ukosefu wa uhakika wa chakula, ukimbizi na upotevu wa bayonuai.

Idadi ya watu wasio na chakula imeongezeka maradufu kutoka milioni 149 kabla ya coronavirus">COVID-19 hadi milioni 333 mwaka 2023 kwenye nchi 78 ambazo zinafuatiliwa na shirika la Umoja wa MAtaifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP.

Hali ya hewa na tabianchi ni vichocheo na kuna nuru

Ripoti inatanabaisha kuwa hali ya hewa na tabianchi ya kupitiliza vinaweza kuwa sio sababu kuu ya changamoto za kiutu hivi sasa lakini ni vichochezi.

Hata hivyo ripoti inasema kuna matumaini hasa kupitia nishati jadidifu, ikiongozwa na nishati ya jua au sola, upepo na maji ambavyo vimeonekana kuwa muhimu katika kufikia malengo ya kuondokana na hewa ya ukaa.