Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

GAZA: Ripoti yasema baa la njaa ni dhahiri; Guterres asema tuepushe yasiyofikirika

Mama akiwaandalia watoto wake chakula nje ya nyumba yao ya mahema katika kambi ya wakimbizi huko Khan Younis, Gaza. (Maktaba)
© UNICEF/Abed Zagout
Mama akiwaandalia watoto wake chakula nje ya nyumba yao ya mahema katika kambi ya wakimbizi huko Khan Younis, Gaza. (Maktaba)

GAZA: Ripoti yasema baa la njaa ni dhahiri; Guterres asema tuepushe yasiyofikirika

Msaada wa Kibinadamu

Hali ya uhakika wa kupata chakula huko Gaza, ni tete na baa la njaa linanyemelea kwenye majimbo ya kaskazini mwa eneo hilo imesema ripoti mpya ya  hali ya chakula Gaza iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO, likisema jawabu la kuondokana na hali hiyo ni amani. 

Mkurugenzi wa Ofisi ya Masuala ya Dharura na Mnepo FAO, Rein Paulsen  akizungumza hii leo huko Roma, Italia wakati wa kutolewa kwa ripoti hiyo ya uchambuzi wa viwango vya uhakika wa kupata chakula au IPC kwa Ukanda wa Gaza, anasema takwimu zinajenga taswira ya hali ya kutia wasiwasi mkubwa. Na pindi tunapofikiria kuhusu Gaza Kaskazini, ambako hali ni mbaya zaidi, uchambuzi wa sasa  unatuonesha kuwa njaa ni dhahiri katika kipindi cha kuanzia sasa na Mei 2024.

Hii ina maana tunapotazama mwelekeo wa takwimu za hali ya upatikanaji chakula na lishe tunaona hali ya kutisha. Kusini, hali nayo imezidi kuwa mbaya na huko tunashikilia makadirio yetu ya uwezekano wa baa la njaa.”

Ripoti inaonesha kuwa mwendelezo wa uhasama umesambaratisha sekta ya kilimo, ambayo familia za Gaza inategemea kwa ajili ya kujipatia kipato.

Kuanzia kaskazini hadi kusini mwa Gaza watu hawana chakula

“Watu wote kwenye ukanda wa Gaza wanakabiliwa na viwango vya juu vya ukosefu mkubwa wa chakula ukiwekwa katika kiwango cha 3, na 4. Hii inaamanisha nusu ya idadi ya watu wote wa eneo hilo, takribani milioni 1.1 wanaweza kukabiliwa na janga kubwa la ukosefu wa uhakika wa chakula la kiwango cha 5.”

Tweet URL

Hivyo amesema usaidizi wa haraka unahitajika kurejesha uzalishaji wa chakula na kwa mujibu na ripoti “Inatueleza kuwa baadhi ya mifugo iko hai, na inaweza kusaidiwa na ndio maana FAO inajikita kusaidia mahitaji ya kujipatia kipato Ukanda wa Gaza. Kwa sasa tumepata kibali cha kupeleka tani 1500 za ujazo za chakula cha mifugo.”

Amesema uhai wa mifugo utakuwa hakikisho la upatikanaji wa maziwa kwa familia, maziwa ambayo yatakuwa ni lishe bora kwa watoto na hivyo kukabili utapimlo uliokithiri miongoni mwa watoto.

Akatamatisha akisema, “uhakika wa kupata chakula utawezekana kukiweko na amani. Na haki ya kupata chakula ni haki ya msingi. Hili linapaswa kuzingatiwa na wadau wote.”

Tuchukue hatua kuzuia yasiyofikirika - Guterres

Kufuatia kutolewa kwa ripoti hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amezungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani hii leo na kusema ripoti ni kithibitisho cha umuhimu wa sitisho la mapigano kwa misingi ya kibinadamu.

Ripoti mpya kuhusu ukosefu wa uhakika wa chakula Gaza ni shtaka la mazingira ya kusikitisha yanayokabili raia huko Gaza, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari hii leo jijini New York, Marekani punde tu baada ya ripoti hiyo kutolewa na FAO.

“Wataalamu wabobezi kuhusu ukosefu wa uhakika wa chakula wametoa chapisho hilo linalodhihirisha kuwa baa la njaa ni dhahiri Gaza,” amesema Katibu Mkuu.

Idadi ya wasio na uhakika wa kupata chakula Gaza haijawahi kutokea duniani

Wapalestina Gaza wanakabiliwa na viwango vya kutisha vya njaa na wanapitia machungu. Ripoti inasema watu milioni 1.1 wako taabani kutokana na ukosefu wa chakula, amesema Guterres akinukuu ripoti hiyo.

“Hii ni idadi kubwa ya watu kuwahi kuripotiwa kuwa wanakabiliwa na njaa kupitia mfumo wa IPC kokote kule duniani na katika wakati wowote ule,” amesema katibu Mkuu.

 Katibu Mkuu amesema hili ni janga lililotengenezwa na binadamu na ripoti inaweka bayana kuwa linaweza kukomeshwa.

Ametoa wito kwa Israel kuhakikisha misada ya kiutu inafikia walengwa Gaza yote bila vikwazo vyovyote na kwa jamii ya kimataifa isaidie juhudi za kiutu .

“Tuchukue hatua sasa kuzuia yasiyofikirika, yasiyokubalika na yasiyohalalishika,” ametamatisha Katibu Mkuu.