Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya pili ya sitisho la mpigano Gaza: UN yathibitisha kuwasili kwa misaada zaidi ya kiutu

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaaada ya dharura na ya kibinadamu, OCHA imethibitisha kuingia zaidi kwa malori yenye misaada ya kiutu ukanda wa Gaza.
© UNICEF/Eyad El Baba
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaaada ya dharura na ya kibinadamu, OCHA imethibitisha kuingia zaidi kwa malori yenye misaada ya kiutu ukanda wa Gaza.

Siku ya pili ya sitisho la mpigano Gaza: UN yathibitisha kuwasili kwa misaada zaidi ya kiutu

Msaada wa Kibinadamu

  • Ni chakula, magari ya kubeba wagonjwa na dawa
  • Lita 129,000 za nishati ya mafuta nazo zafikishwa eneo hilo
  • Mateka zaidi waachiliwa huru, OCHA yataka wote waachiliwe huru 

Malori 61 yakiwa na shehena za misaada ya kibinadamu yameingia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza leo Jumamosi, ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya malori tangu tarehe 7 Oktoba mwaka huu wanamgambo wa kipalestina wa Hamas walipoanza mashambulizi dhidi ya Israel na kusababisha makabiliano  yanayoendelea hadi sasa.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kiutu, OCHA imethibitisha kuingia kwa malori hayo ikisema shehena inajumuisha vyakula, maji na vifaa vya dharura vya matibabu. 

Magari 11 ya kubebea wagonjwa, mabasi matatu ya abiria na vitanda vya kubebea wagonjwa viliwasilishwa hospital ya Al Shifa kusaidia kuhamisha wagonjwa kwenda maeneo ya kusini mwa Gaza.

Halikadhalika siku ya leo Jumamosi, malori mengine 200 yaliondoka Nitzana, ambapo 187 kati yao yameingia Gaza saa moja usiku kwa saa za eneo hilo la Mashariki ya Kati. OCHA pia inasema lita 129,000 za nishati ya mafuta ziliingizwa Gaza.

Juhudi za pamoja

OCHA inasema hatua za leo zisingalifanikiwa bila ya juhudi za pamoja kati ya mashirika ya Hilal Nyekundu ya Palestina na Misri, hivyo ofisi hiyo inatoa shukrani kwa hatua za pamoja zinazofanywa na pande zote kufanikisha ufikishaji wa misaada.

Taarifa ya OCHA inasema kadri sitisho la mapigano litakavyozidi kuendelea, vivyo hivyo misaada zaidi ya kiutu itaingia Gaza.

Twakaribisha kuachiliwa zaidi mateka, lakini waachiliwe wote

Pamoja na kukaribisha kuachiliwa huru mateka zaidi siku ya Jumamosi, OCHA imerejelea wito wake wa kutaka kuachiliwa mateka wote haraka na bila masharti yoyote.

“Na tunatumaini kuachiliwa zaidi kwa wafungwa wa kipalestina ili kuleta nafuu kwa familia na wapendwa wao,” imesema taarifa hiyo.

Sitisho la mapigano kwa misingi ya kiutu limeanza kuzingatiwa Ijumaa asubuhi tarehe 24 Novemba 2023 ambapo mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wameweza kuimarisha kasi ya kuingiza misaada ya kibinadamu Gaza.