Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sitisho la mapigano ndio njia pekee ya kumaliza 'jinamizi' Gaza- Guterres

Katibu Mkuu wa UN António Guterres (kwenye mimbari) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Gaza. Kulia ni Msemaji wake Stéphane Dujarric.
UN /Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa UN António Guterres (kwenye mimbari) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Gaza. Kulia ni Msemaji wake Stéphane Dujarric.

Sitisho la mapigano ndio njia pekee ya kumaliza 'jinamizi' Gaza- Guterres

Msaada wa Kibinadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameelezea matumaini yake kuwa azimio la kufanikisha upelekaji misaada zaidi ukanda wa Gaza lililopitishwa leo Ijumaa na Baraza la Usalama linaweza kufanikisha makubaliano ya sitisho la mapigano kati ya Israel na wanamgambo wa kipalestina, Hamas.

Guterres alikuwa akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya UN punde tu baada ya azimio hilo kupitishwa.

Amesema hakujakuweko na mabadiliko dhahiri kwa jinsi vita inavyoendelea huko Gaza bila ulinzi wowote wa raia. Mashambulizi ya Israel yameendelea huku Hamas na vikundi vingine vilivyojihami wakiendelea kurusha maroketi na makombora nchini Israel.

Amesema mashambulizi hayo yamesababisha vifo wakiwemo zaidi ya wapalestina 20,000. Halikadhalika watu milioni 1.9, sawa na asilmia 85 ya wakazi wote wa Gaza wamekimbia makazi yao.

Mfumo wa afya umedhoofika, maji safi na salama ni haba, na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP, limeonya kuweko kwa tishio la baa la njaa.

"Sitisho la mapigano kwa minajili ya kiutu ndio njia pekee ya kuanza kukidhi mahitaji haya ya watu wanaohaha kila uchao Gaza na pia kumaliza jinamizi linalowakumba,” amesema Guterres akiongeza, “ni matumaini yangu kuwa azimio la leo la Baraza la Usalama litasaidia hatimaye hili kuwezekana lakini bado kuna mambo mengi yanahitajika haraka.”

Unapimaje ufanisi wa misaada na idadi ya malori?

Bwana Guterres amewaambia waandishi wa habari kuwa lilikuwa “ni kosa” kupima ufanisi wa operesheni za kiutu Gaza kwa misingi ya idadi ya malori yenye shehena za misaada ambayo yanaruhusiwa kuingia kwenye eneo hilo lililozingirwa.

“Tatizo halisi ni kwamba jinsi ambavyo Israel inaendesha operesheni zake inaweka vizingiti vya mgao wa misaada ya kibinadamu ndani ya Gaza,” amesema Katibu Mkuu.

Amesisitiza kuwa operesheni fanisi ya misaada ya kibinadamu inahitaji mambo makuu manne ambayo kwa sasa hayako Gaza, ambayo ni usalama, wafanyakazi watakaoendesha shughuli zao kwa usalama, uwezo wa vifaa na kurejea kwa shughuli za kibiashara.

Akimulika usalama, amesema mashambulizi ya makombora kutoka Israel na mapigano ya ndani Gaza kwenye maenoe ya watu yanatishia raia na wafanyakazi wanaogawa misaada.

Wakati watumishi wa misaada wanatakiwa wawe na uwezo wa kuishi na kufanya kazi zao kwa usalama, watumishi 136 wa shirika la Umoja wa Mataifa la kusaidia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA wameuawa tangu kuanza kwa mizozo, amesema, Katibu Mkuu, akiongeza kuwa “hakuna pahala popote salama Gaza.”

Miundombinu yakwamisha usambazaji wa misaada

Akigeukia vifaa, Katibu Mkuu ameripoti kuwa kila lori lenye shehena za misaada linapoingia Gaza kupitia moja ya vivuko viwili ambayo ni Kerem Shalom na Rafah – lazima lipakue na kisha lipakie tena  mizigo kwa ajili ya kugawa Gaza.

“Idadi kubwa ya magari yetu na malori yameharibiwa au kusalia nyuma kufuatia kushinikizwa au kuharakishwa kuondoka kutoka Kaskazini, lakini, mamlaka za Israel hazijaruhusu malori mengine ya ziada kufanya kazi Gaza. Hii inakwamisha sana operesheni za misaada,” amesema Katibu Mkuu.

Halikadhalika, usambazaji wa misaada eneo la Gaza Kaskazini ni hatari kupindukia kutokana na mapigano, vilipuzi, na barabara zilizoharibiwa kwa kiasi kikubwa, amesema Katibu Mkuu, akiongeza kuwa kukatika kwa mawasiliano mara kwa mara huko Gaza kunafanya vigumu mno kwa uratibu kupitia mtandao wa simu na watu wanaogawa misaada na wale wanaowasilisha misaada.