Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Itachukua miaka kuondoa mamilioni ya kifusi Gaza: UNRWA

Watoto wakiwa wamesimama mbele ya nyumba iliyobomolewa na mlipuko wa bomu katika mji wa Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.
© UNICEF/Eyad El Baba
Watoto wakiwa wamesimama mbele ya nyumba iliyobomolewa na mlipuko wa bomu katika mji wa Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Itachukua miaka kuondoa mamilioni ya kifusi Gaza: UNRWA

Amani na Usalama

Vita huko Gaza imeacha takribani tani milioni 23 za vifusi na silaha ambazo hazikulipuka zimetawanyika katika eneo hilo, wahudumu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wamesema leo Ijumaa Machi 15.

Katika tahadhari mpya kuhusu hali mbaya ya dharura ya kibinadamu ambayo bado inatokea katika eneo hilo, shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, leo Ijumaa limesema kwamba "itachukua miaka" kabla ya Ukanda huo kuwekwa salama tena.

Maisha ya zaidi ya watu milioni mbili wa Gaza yameharibiwa na mashambulizi ya kila siku ya Israel, tangu mashambulizi ya kigaidi yaliyoongozwa na Hamas nchini Israel tarehe 7 Oktoba, UNRWA imeeleza katika chapisho kwenye mtandao wa X, zamani Twitter.

UNWRA ikiwa ndilo shirika kubwa zaidi la misaada huko Gaza linaendelea kutoa vifaa na huduma za kuokoa maisha kwa zaidi ya watu milioni 1.5 waliokimbia makazi yao kusini mwa eneo hilo. Shirika hilo linaendesha makazi kwa zaidi ya watu milioni moja, kuwapa misaada ya kibinadamu na huduma ya afya ya msingi.

Kazi ya kuokoa maisha ya kibinadamu imeendelea huku kukiwa na mashambulizi makali ya Israel ya mabomu na operesheni za ardhini pamoja na mapigano makali kati ya majeshi ya Israel na makundi yenye silaha ya Palestina.

Katika taarifa yake ya hivi punde kuhusu hali ya dharura, Ofisi ya uratibu wa misaada ya Umoja wa Mataifa, OCHA, inaripoti kwamba ghasia zinazoendelea "katika sehemu kubwa ya Ukanda wa Gaza, hasa katika eneo la Hamad la Khan Younis. Mapigano hayo yanasababisha vifo zaidi vya raia, kufurushwa na uharibifu wa nyumba na miundombinu mingine ya raia..”

Ufadhili

Habari hizo zimekuja wakati Australia imekuwa nchi ya hivi punde zaidi kutangaza kwamba inakusudia kurejesha ufadhili kwa UNRWA, ambayo ilishuhudia msaada wa wafadhili wa kimataifa ukipungua, huku kukiwa na madai ya Israeli kwamba baadhi ya wafanyakazi wa shirika hilo walishiriki katika shambulio la kigaidi la Oktoba 7 lililoongozwa na Hamas huko Israeli.

Uchunguzi wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa unaendelea kuhusu madai hayo, ambayo UNRWA pia inakamilisha uchunguzi wake yenyewe. Muda mfupi baada ya madai hayo kuwekwa hadharani, wafanyakazi tisa wa UNRWA walifutwa kazi.

Mchango wa misaada ya baharini

Meli ya shirika la Open Arms ikiwa imesheheni chakula na maji na wafanyakazi waliojitolea tayari kusaidia walio hatarini zaidi huko Gaza.
© Open Arms

Wakati huo huo, juhudi za kupata njia mpya ya usaidizi wa baharini kutoka Cyprus hadi Gaza zimeendelea leo Ijumaa ya Machi 15 huku meli ya Open Arms ikisogea karibu na ufuo wa Gaza.

Kulingana na ripoti, meli hiyo, ambayo imeonekana ikiwa imefika kwenye ufuo wa Mji wa Gaza kaskazini mwa eneo hilo leo asubuhi, iliondoka Larnaca kusini mwa Cyprus Jumanne ikiwa na tani 200 za msaada. Hizi zitawasilishwa ufukweni mara jeneo maalumu litakapojengwa kusini mwa Gaza City, kulingana na ripoti.