Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Muhula wa shule za UNRWA mwaka huu uko shwari licha ya ukata :UN

Wanafunzi katika shule zinazofadhiliwa na UNRWA wakiwa kwenye mahojiano na UN News kwenye shule ya maandalizi ya wasichana ya Ar Rimal huko Ukanda wa Gaza
UNRWA/Khalil Adwan
Wanafunzi katika shule zinazofadhiliwa na UNRWA wakiwa kwenye mahojiano na UN News kwenye shule ya maandalizi ya wasichana ya Ar Rimal huko Ukanda wa Gaza

Muhula wa shule za UNRWA mwaka huu uko shwari licha ya ukata :UN

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA limesema mwaka huu huenda likaweza kuendelea kuendesha shule zake kwa wakimbizi hadi mwisho wa muhula wa shule 2019.

Kwa mujibu wa Matthias Schmale mkuu wa operesheni za UNRWA mjini Gaza, bado shirika hilo  lina pengo kubwa katika bajeti yake lakini hawakati tamaa na wana matumaini ya mwakani.

Bwana Mathias Schmale amesema, “bado tuna upungufu katika bajeti yetu kuu lakini tumebakiwa na mwezi mmoja na nusu tu kufika mwisho wa mwaka 2018. Endapo tutafika mwisho wa Desemba tunajua kwamba kuna nchi wanachama ambao waliahidi fedha kwa mwaka ujao. Hivyo naweza kusema kwamba muhula wa mwaka huu wa shule kimsingi umesalimika. Tuna changamoto za kupata fedha , lakini naweza kuweka bayana hadharani kwamba tunaweza tukakamilisha muhula wa shule mwaka huu.”

Ameongeza kuwa  na hii ni katika maeneo yote matano wanamoendesha operesheni zao ambayo ni Jordan, Syria, Lebanon, Ukingo wa Magharibi ukijumuisha Jerusalem Mashariki na Gaza.

UNRWA inakabiliwa na ukata wa fedha baada ya uamuzi wa serikali ya Marekani wa kupunguza kwa kiasi kikubwa mchango wake kwa shirika hilo.

Shirika hilo limekuwa likitoa ulinzi na msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina milioni 5 na ufadhili wake unatokana na michango ya hiyari kutoka kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.