Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nilipoteza matumaini ya kuishi gerezani Urusi- Mfungwa wa vita wa Ukraine

Vita vya Ukraine vimeshamiri uvamizi wa makombora wa Urusi katika maeneo yaliyojengwa sana, kulingana na wachunguzi huru wa haki.
© UNICEF/Oleksii Filippov
Vita vya Ukraine vimeshamiri uvamizi wa makombora wa Urusi katika maeneo yaliyojengwa sana, kulingana na wachunguzi huru wa haki.

Nilipoteza matumaini ya kuishi gerezani Urusi- Mfungwa wa vita wa Ukraine

Haki za binadamu

Ushahidi mpya kabisa wa ukatili wa kimfumo na uliosambaa na uwezekano wa kuweko kwa uhalifu wa kivita uliotekelezwa na majeshi ya Urusi dhidi ya raia na mateka wa kijeshi nchini Ukraine umewekwa bayana hii leo kupitia ripoti mpya ya wachunguzi huru waliochaguliwa na Umoja wa Mataifa.

Tume Huru ya Kimataifa ya Uchunguzi wa kinachoendelea Ukraine tangu Urusi ianze mashambulizi tarehe 24 mwezi Februari mwaka 2022 iliunda na Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu na ripoti yake inaonesha madhara makubwa ya uvamizi huo.

“Nilipoteza matumaini na nia ya kusihi,” anasema mmoja wa maaskari wa Ukraine na mfungwa wa zamani wa vita wakati akizungumza na wajumbe wa Tume hiyo, akielezea “jinsi amekuwa akikabiliwa na mateso ya mara kwa mara huku akiwa amesalia na mifupa yake iliyovunjwa, meno na  maambukizi” kwenye moja mguu wake aliojeruhiwa.

Baada ya kujaribu kujiua kwenye gereza moja lililoko mji wa Donskoy mkoa wa Tula kusini mwa Moscow, mji mkuu wa Urusi, askari huyo alielezea jinsi watekaji wake “walivyompatia kipigo,” amesema Erik Møse, Mwenyekiti wa Tume hiyo.

“Maelezo ya manusura yanadhihirisha vipigo na utesaji mkubwa na maumivu  na machungu wakati waliposhikiliwa kwa muda mrefu huku utu wao ukipuuzwa. Hilo lilisababisha majeraha ya kimwili na kiakili,” amesema Mwenyekiti huyo akizungumza na waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi.

“Waliwapiga kwenye makalio yake akiwa kwenye eneo lililotengwa, na kumsababishia uvujaji damu kwenye njia yake ya haja kubwa,” wameeleza wachunguzi hao.

Akiwa kwenye eneo la uwazi, walimpiga usoni na kujeruhi mguu wake, na hivyo kumsababishia uvujani mkubwa wa damu. Waligonga meno yake. Aliwasihi wasimuue.”

Erik Møse, MWenyekiti wa Tume Huruya Uchunguzi Ukraine (kati) Kamishna Vrinda Grover (kushoto) na mwendeshaji wa kikao Todd Pitman, kutoka OHCHR, wakati wa mkutano na waandishi wa habari Geneva, Uswisi.
UN News/ Anton Uspensky
Erik Møse, MWenyekiti wa Tume Huruya Uchunguzi Ukraine (kati) Kamishna Vrinda Grover (kushoto) na mwendeshaji wa kikao Todd Pitman, kutoka OHCHR, wakati wa mkutano na waandishi wa habari Geneva, Uswisi.

Ubakaij na vipigo

Shuhuda za ubakaji na mashambulizi mengine ya kingono dhidi ya wanawake “pia yalikuwa ni mateso,” wamesema makamishna hao, wakitaja vitisho vya ubakaji dhidi ya wafungwa wa kivita wanaume, matumizi ya nyaya zenye umeme vikilenga kuwaumiza au kuwajengea hofu wafungwa.

“Kulikuwa na vipigo, manyanyaso kwa njia ya kauli, matumizi ya vifaa vya umeme kwenye miili yao, ilikuwa shida kupata chakula, maji,” amesema Bwana Møse. “Matendo yote dhidi ya askari wa vita, taswira tuliyopata na jinsi ambavyo walikabiliana na hali husika inafanya tutumie neno ‘kusababisha kitisho’”.

Shuhuda zinazokupatia taswira

Ripoti hiyo ya kurasa 20 inatokana na shuhuda kutoka kwa mamia ya watu ili kuwezesha kuchunguza madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu na manyanyaso  dhidi ya sheria za kimataifa za kibinadamu, vitendo vinavyodaiwa kufanywa na jeshi la Urusi na mamlaka.

Chapisho linajikita kwenye kuzingirwa na mashambulizi yasiyokoma dhidi ya mji wa Mariupol mara tu baada ya kuanza kwa uvamizi, na matumizi ya mateso na ubakaji dhidi ya raia, wafungwa wa vita na washirika washukiwa, uhamishaji wa watoto 46 kinyume cha sheria mwezi Oktoba 2022 kutoka kituo cha Kherson kwenda eneo la Crimea linalokaliwa na Urusi, halikadhalika uharibifu wa maeneo yanayolindwa ya hazina za kitamaduni.

“Ushahidi unaonesha kuwa mamlaka za Urusi zimetekeleza ukiukwaji wa sheria za kimataifa za haki za binadamu na kibinadamu na uhalifu mwingine unaombatana nao,” amesisitiza Kamishna Vrinda Grover.

“Uchunguzi wa ziada unahitajika kubaini iwapo baadhi ya mazingira ya vitendo vilivyofanyika yanaweza kubainika kuwa uhalifu dhidi ya binadamu.”

Soma ripoti nzima hapa.

Ripoti itawasilishwa mbele ya Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu Jumanne Machi 19, 2024. Unaweza kutazama hapa siku hiyo ikiwasilishwa Geneva, Uswisi https://webtv.un.org/en/schedule/2024-03-19 .