Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasichana ni majaji watarajiwa, wafuate ndoto zao jamii ziendelee kunufaika - Hakimu Pamela Achieng

Pamela Achieng, Hakimu katika mahakama ya Ngong iliyo katika Kaunti ya Kajiado nchini Kenya.
UN News
Pamela Achieng, Hakimu katika mahakama ya Ngong iliyo katika Kaunti ya Kajiado nchini Kenya.

Wasichana ni majaji watarajiwa, wafuate ndoto zao jamii ziendelee kunufaika - Hakimu Pamela Achieng

Wanawake

Mkutano wa 68 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW68 ukiendelea hapa jijini New York Marekani tunavinjari hadi nchini Kenya kumsikia Hakimu Pamela Achieng ambaye azma yake ya kujikita kwenye masula ya kusimamia haki ilichochewa na swali alilojiuliza yeye mwenye ya kwamba  “kama mwanaume anaweza kufanya kazi zinazotambulika hasa za kutetea haki za raia katika mahakama kwanini mwanamke asiweze?”

 

 

Katika kufahamu sasa amefikia wapi, Redio washirika wetu Redio Domus ya nchini Kenya ilifanya mahojiano Bi. Achieng, ambaye sasa ni hakimu katika mahakama ya Ngong iliyoko katika Kaunti ya Kajiado.

Katika mahojiano haya yaliyofanyika pia kuadhimisha siku ya majaji wanawake duniani tarehe 10 mwezi Machi mwaka huu  inayolenga kusongesha  juhudi za kimataifa za kuhakikisha usawa wa kijinsia na kushughulikia masuala ya uadilifu wa mahakama yanayohusiana na jinsia, , Hakimu Achieng anaanza kwa kuelezea ni kwa nini kama mwanamke aliamua kuingia katika tasnia hii.

“Nilivutiwa sana kuingia katika masomo ya sheria kwa sababu babangu mzazi ni Mwanasheria. Pia niligundua kwamba wanasheria wengi ni wanaume na wanawake ni wachache sana, na kwa kufikiria tu hilo likanipatia changamoto chaya kwa sababu niliona kwamba kama mwanaume anaweza kufanya kazi zinazotambulika hasa za kutetea haki za raia katika mahakama kwanini mwanamke asiweze? Na sasa nimejikuta kwamba mimi ni mmoja wa wanawake ambao wamefaulu kuingia katika tasnia ambayo imesalia kuwa na wanaume wengi kwa muda mrefu”  

Kama Hakimu mwanamke, mnafanya nini kuhakikisha wanawake wote wanapata kujua haki zao na kesi zao kuwasilishwa na kusikilizwa kwa usawa katika mahakama?

“Mosi, mimi ni mwanachama wa chama cha kimataifa cha majaji wanawake inayoungwa mkono na Shirika la Umoja wa Mataifa la wanawake UN Women, na ninajivunia kwamba tulipatiwa siku hii ya Majaji wanawake. Cha pili ni kwamba kesi nyingi za dhuluma kwa wanawake na unyanyasaji kwa upande wa umiliki wa shamba wakati wanafiwa na waume wao, na mara kwa mara tunatilia mkazo mambo hayo na kuenda vijijini kufundisha wanawake na jiamii kuhusu haki zao na kuhamasisha jamii ili ziweze kukomesha ukatili huo au unyanyasaji wa kijinsia. Kama Hakimu kesi zikiletwa mbele ya mahakama kazi zetu ni kuhakikisha kila mtu anapata kusikilizwa kwa haki na kuzingatia usawa wa kijinsia.”

Kwa kuzingatia kwamba tasnia hii imegubikwa na mfumo dume, Pamela anatoa ujumbe wa kutia moyo wasichana shuleni ili waweze kujiamini na kuingia katika masomo ya uanasheria na hatimaye kuchangia kuongezeka kwa mahakimu au majaji wanawake.

“Kwanza kabisa Jaji Mkuu wakati huu nchini Kenya ni mwanamke.  Huu ni mfano kubwa ambao umeanza kuchochea wasichana shuleni kuona kwamba pia wao wanaweza kama Jaji Mkuu ameweza. Pia kwa sasa Kenya tunao majaji au mahakimu wanawake wengi, kwa hivyo ni mfano Chanya, wasichana wanaweza.”