Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan: Watu 300 wakatwa miguu mwezi mmoja uliopita pekee

Jill Lawler, Mkuu wa Operesheni za Mashinani na Dharura wa shirika la Umoja wa MAtaifa la kuhudumia watoto UNICEF, nchini Sudan akiwa ziarani Khartoum.
© UNICEF
Jill Lawler, Mkuu wa Operesheni za Mashinani na Dharura wa shirika la Umoja wa MAtaifa la kuhudumia watoto UNICEF, nchini Sudan akiwa ziarani Khartoum.

Sudan: Watu 300 wakatwa miguu mwezi mmoja uliopita pekee

Amani na Usalama

Miezi 11 ya vita nchini Sudan imesababisha machungu kwa watoto na vijana ambako ujumbe wa hivi karibuni wa shirika moja la Umoja wa Mataifa uliozuru hospitali kwenye mji mkuu Khartoum umeshuhudiwa vijana waliokatwa miguu, huku Mkurugenzi wa hospitali hiyo akisema mwezi mmoja uliopita pekee watu wapatao 300 walikatwa miguu yao kutokana na madhara ya vita.

Jill Lawler, Mkuu wa Operesheni za Mashinani na Dharura wa shirika la Umoja wa MAtaifa la kuhudumia watoto UNICEF, nchini Sudan ndiye aliongoza timu ya watu 12 wa shirika hilo wiki iliyopita kujionea hali halisi Omdurman na Khatoum, ikiwa ni ziara ya kwanza kabisa ya UNICEF mjini Khartoum tangu vita ianze mwezi Aprili mwaka jana.

Jill Lawler, Mkuu wa Operesheni za Mashinani na Dharura wa shirika la Umoja wa MAtaifa la kuhudumia watoto UNICEF, nchini Sudan akizuru Khartoum.
© UNICEF
Jill Lawler, Mkuu wa Operesheni za Mashinani na Dharura wa shirika la Umoja wa MAtaifa la kuhudumia watoto UNICEF, nchini Sudan akizuru Khartoum.

Wodi ya majeraha imefurika, wagonjwa watatu kitanda kimoja

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo, Bi. Lawler amesema katika hospitali ya Al-Nau moja ya hospitali pekee zinazofanya kazi Khartoum ambako wodi ya majeruhi imefurika, tulikutana na vijana wawili ambao wamekatwa miguu hivi karibu.. maisha ya vijana hawa yamebadilika kabisa. Na tulielezwa na Mkurugenzi wa hospitali kuwa watu wapatao 300 walikatwa miguu yao hospitalini hapo mwezi mmoja uliopita.

Amesema mahitaij yanaongezeka kila uchao kwani walishuhudia wagonjwa watatu wakiwa kwenye kitanda kimoja, wafanyakazi wamechoka na wengi wao wakigeuza hospitali kuwa ni makazi na mishahara hawajalipwa.

Watoto wenye utapiamlo na walezi wao wako gizani

Bi. Lawler anasema “katika hospitali nyingine tulikuta watoto wenye utapiamlo na walezi wao wakiwa kwenye giza totoro kutokana na kukatika kwa umeme. Jenereta iliharibika wiki moja iliyopita hivyo wanafanyia kazi gizani. Chanjo ziko kwenye majokofu yaliyowekewa vifurushi vya barafu. Tunavyokaribia msimu wa joto kali hizi barafu hazitadumu.”

Wanawake na wasichana waliobakwa wamejifungua

Wakati wa ziara yetu tulibaini kuwa wanawake na wasichana waliobakwa miezi ya mwanzo ya vita sasa wanajifungua watoto baadhi  yao wametelekezwa watunzwe na wafanyakazi wa hospitali ambao wamejenga eneo la kutunza watoto karibu na wadi ya kujifungua.

Afisa huyo amesema waliona pia mtambo wa kusafisha maji wa Al Manara unaofadhiliwa na UNICEF ambao ndio pekee unaofanya kazi kati ya mitambo 13 kwenye eneo la Khartoum ukisambaza maji kwa watu 300,000 eneo la Omdurman ukiwa umeharibiwa kutokana na mapigano na sasa unafanya kazi kwa asilimia 75 pekee. “Mtambo huo utaacha kufanya kazi katika wiki mbili zijazo iwapo klorini inayotumika kusafisha maji haitapelekwa.”

Mtoto akikimbia kutoka Wad Madani, jimbo la Al Jazirah mashariki-kati mwa Sudan kufuatia vita ya kutumia silahaya hivi majuzi.
© UNICEF/Ahmed Elfatih Mohamdee
Mtoto akikimbia kutoka Wad Madani, jimbo la Al Jazirah mashariki-kati mwa Sudan kufuatia vita ya kutumia silahaya hivi majuzi.

Tulisikia milio ya makombora na tuliona vijana wengi wamebeba silaha

Amesema ingawa waliweza kusikia milio ya risasi na makombora kwa mbali, angalau kulikuwa na utulivu eneo walilokuwako, lakini eneo la masoko, mitaani na hata hospitali kulikuweko na idadi kubwa ya wanajeshi.

“Tuliona vijana wengi wamebeba silaha, hatukuweza kufahamu umri wao lakini ni wadogo na bila shaka hawako shuleni kwani shule zimefungwa tangu kuanza kwa vita,” amesema Bi. Lawler.

Njaa nayo imeshamiri, hakuna vyakula sokoni, na hata kilichoko, familia haziwezi kumudu kwani kukatwa kwa mawasiliano kunafanya familia zishindwe kupokea mgao wa fedha taslimu.

UNICEF inataka nini kifanyike?

Akasema kile ambacho UNICEF inataka hivi sasa ni pande kwenye mzozo ziwezeshe ufikishaji wa misaada ya kiutu bila vikwazo vyovyote, na vile vile zilinde watoto kwani ni wajibu wao kisheria na kimaadili. Halikadhalika jamii ya kimataifa ichangishe rasilimali zinazotakiwa kufikishia mahitaji wananchi wa Sudan na pia ifanikishe sitisho la mapigano.