Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 297 wafanikiwa kuhamishwa kutoka eneo la vita mpaka eneo salama nchini Sudan

Watoto wakihamishwa kutoka kwa kituo cha watoto yatima cha Mygoma huko Khartoum, Sudan, hadi kituo cha muda katika eneo salama zaidi nchini humo.
© UNICEF
Watoto wakihamishwa kutoka kwa kituo cha watoto yatima cha Mygoma huko Khartoum, Sudan, hadi kituo cha muda katika eneo salama zaidi nchini humo.

Watoto 297 wafanikiwa kuhamishwa kutoka eneo la vita mpaka eneo salama nchini Sudan

Amani na Usalama

Kufuatia vita inayoendelea nchini Sudan, watoto 297 wamehamishwa kwa usalama kutoka kituo cha watoto yatima cha Mygoma huko Khartoum nchini Sudan hadi kituo cha muda katika eneo salama zaidi nchini humo.

Mafundi uashi wakichomelea vyuma na wengine wakiwa wanachomelea nguzo varandani…… Nje wahandisi wanaonekana wakijadili jambo eneo la genereta… haya yote yakiendelea ndani ya eneo ambalo linaonekana kama ukumbi mkubwa wenye viti vichache wakionekana wanawake wameketi wengine wamesimama na watoto wadogo wakicheza katika mikeka na zulia jekundu. 

Hapa ni Madani, mji mkuu wa jimbo la Al Jazirah lililoko mashariki ya kati mwa nchi ya Sudan. Eneo hili ndio makazi mapya salama ya watoto 297 waliotolewa katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Mygoma huko Khartoum ambapo sasa hali si shwari, vita vime taradadi. 

Kituo hichi ni cha mpito, watoto hapa wako chini ya uangalizi wa wizara za Ustawi wa Jamii na Afya ya Sudan wakishirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya watoto, UNICEF ambalo linasaidia kwenye matibabu ya watoto, lishe, msaada wa kisaikolojia, michezo na shughuli za elimu, na huku wakiwasaidia walezi wa watoto waliohamishwa.

Uhamisho wa watoto hawa umefanyika kwa kutumia magari ya kubebea wagonjwa ndani ya magari hayo watoto wamewekwa kwenye mabeseni ama hakika vita kitu kibaya sana. 

Na pia mabasi makubwa ya kubeba abiria yametumika, watoto wanaojiweza wakiwa wameshikiliwa na wazazi wao wanaonekana kupiga hatua ndogo ndogo kuingia kwenye kituo hicho ambacho bado kinatengenezwa, na wale wasiojiweza na watoto wachanga, wazazi na wahudumu wa UNICEF wanaonekana kuwabeba wakiwa katika mwendo wataratibu wakiingia nao ukumbini hapo. 

Mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan Mandeep O'Brien anasema kufanikiwa kwa uhamisho huu wa watoto kutoka eneo la vita kuja eneo salama kumeleta mwanga katikati ya vita vinavyoendelea nchini Sudan. 

Hata hivyo O’Brien anasema “Mamilioni mengi ya watoto, bado wako hatarini kote nchini Sudan, wanatishwa na mapigano, wanakimbia makazi yao na kuendelea kupata athari za vita kama vile kukosa huduma za kuokoa maisha yao. Mustakabali wa watoto unahatarishwa na vita hivi kila siku.”

Mbali na kutoa huduma za matibabu na lishe, UNICEF wanashirikiana na mamlaka husika katika kutambua watoto wasio na walezi.

Mpaka sasa takwimu za UNICEF zinaonesha kote nchini Sudan, zaidi ya watoto milioni 13.6 wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu wa kuokoa maisha, hii ni idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa nchini humo. 

Athari za vita zinaendelea kutishia maisha na mustakabali wa familia na watoto, na kuacha huduma za kimsingi zikiwa zimekatishwa na vituo vingi vya afya kufungwa au kuharibiwa.

UNICEF imetoa ombi la dola milioni 838 kushughulikia mzozo huo, fedha hii ikiwa ni ongezeko la dola milioni 253 tangu mzozo wa sasa uanze mwezi Aprili 2023.