Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN: Jumuiya ya kimataifa saidieni kuunda misheni ya usaidizi nchini Haiti

Kundi la watu waliopoteza makazi katika shule katikati ya Port-au-Prince, katika tovuti ya Jean-Marie Vincent.
© IOM/Antoine Lemonnier
Kundi la watu waliopoteza makazi katika shule katikati ya Port-au-Prince, katika tovuti ya Jean-Marie Vincent.

UN: Jumuiya ya kimataifa saidieni kuunda misheni ya usaidizi nchini Haiti

Amani na Usalama

Baada ya Kenya kutangaza kusitisha mpango wake wa kupeleka askari nchini Haiti mpaka pale hali ya kisiasa itakapo tengamaa, Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kusaidiana katika kuunda misheni ya usaidizi kwa watu wa Haiti haraka iwezekanavyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York Marekani msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema hali ya kisiasa nchini Haiti “imebaki kidogo nje ya mwelekeo” na kueleza kuwa ni muhimu kwa viongozi wa kisiasa nchini humo na mashirika ya kiraia kukubaliana njia bora ya kusonga mbele ambayo ni kuunda Baraza la Rais haraka iwezekanavyo ili kurejesha mambo ya kisiasa kurejea kawaida nchini humo. 

Alipoulizwa na waaandishi wa habari iwapo Umoja wa Mataifa itazungumza na serikali ya Kenya kuwashawishi kubadilisha msimamo wao Bw. Dujarric alisema kuwa “Tunachoomba ni jumuiya ya kimataifa kuunga mkono uundaji wa misheni hii ya usaidizi haraka iwezekanavyo. Nchi nyingine pia zimeonesha nia ya kuchangia. …Sidhani kama ni sawa kuweka mustakabali wa Haiti na usalama wa Haiti kwenye mabega ya Kenya pekee.”

Msemaji huyo akaenda mbali zaidi na kukumbusha jumuiya ya kimataifa kusaidia kwa kutoa fedha za kuwezesha kufanikisha misheni hiyo. 

Kuhusu wananchi wa Haiti wanaokimbilia mataifa jirani kusaka hifadhi kutokana na ukosefu wa usalama nchini mwao, msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa amekumbusha kuwa “Ni muhimu kwamba utu na haki za binadamu za Wahaiti ambao wametafuta maisha bora katika maeneo mengine, iwe ni Jamhuri ya Dominika au nchi nyinginezo, ziheshimiwe. Hatutaki kuona watu wanaoyakimbia makazi yao kulazimishwa kurudi katika nchi ambayo ni wazi si salama.”

Umoja wa Mataifa umesisitiza tena kuwa pamoja na kuendelea kuwepo na kutoa usaidizi nchini Haiti umeweka wazi kuwa suluhu kwa watu wa Haiti zinatokana na makubaliano yao wenyewe na hivyo ni vyema kwa wanasiasa na asasi za kiraia kukubaliana kufikia makubaliano ya kuunda Baraza la Rais haraka iwezekanavyo. 

Ikumbukwe kuwa siku ya jumatatu wiki hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa taarifa kuhusu makubaliano yaliyofikiwa na wadau wa Haiti kuhusu mipango ya utawala wa mpito nchini humo, ikiwemo kuanzishwa kwa Baraza la Kirais na uteuzi wa Waziri Mkuu wa mpito. Soma taarifa hiyo hapa.