Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haiti: Guterres azungumzia makubaliano ya mipango ya utawala nchini humo

Kundi la watu waliohamishwa makazi katika shule moja katikati ya Port-au-Prince, Haiti.
© IOM/Antoine Lemonnier
Kundi la watu waliohamishwa makazi katika shule moja katikati ya Port-au-Prince, Haiti.

Haiti: Guterres azungumzia makubaliano ya mipango ya utawala nchini humo

Ukuaji wa Kiuchumi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ana taarifa kuhusu makubaliano yaliyofikiwa jana Jumatatu na wadau wa Haiti kuhusu mipango ya utawala wa mpito nchini humo, ikiwemo kuanzishwa kwa Baraza la Kirais na uteuzi wa Waziri Mkuu wa mpito.

Taarifa iliyolewa leo jijini New York, Marekani na msemaji wa Umoja wa Mataifa, imemnukuu Katibu Mkuu akielezea pia kufahamu kuhusu tangazo la Waziri Mkuu Ariel Henry ya kwamba atajiuzulu punde tu Baraza hilo la Mpito la Kirais litakapoanzishwa.

“Katibu Mkuu anatoa shukrani za dhati kwa CARICOM, na wadau wengine wa kimataifa kwa kufanikisha hatua hii ya kuelekea kutatua janga la kisiasa Haiti na anatoa wito kwa wadau wa taifa hilo kuchukua hatua za uwajibikaji na vile vile kuchukua hatua kuelekea kutekeleza makubaliano hayo,” amesema Guterres. 

CARICOM jumuiya ya nchi za ukanda wa Karibea. 

Ameongeza kuwa hatua hiyo itawezesha kurejesha taasisi za kidemokrasia kupitia chaguzi jumuishi, halai na shikiriki tena kwa njia ya amani. 

Amesema Umoja wa MAtaifa kwa upande wake kupitia ujumbe nchini Haiti, utaendelea kusaidia Haiti katika mwelekeo wa kufanya uchaguzi. 

“Katibu Mkuu amesisitiza mshikamano wake usiotetereka na wananchi wa Haiti ambao wanahitaji usalama, malazi, chakula na matibabu na vile vile wanahitaji kuishi maisha ya utu,” imetamatisha taarifa hiyo. 

Haiti iko katika janga la kiusalama ambako maeneo hususan kwenye mji mkuu Port-au-Prince na viunga vyake yanadhibitiwa na magenge ya uhalifu na hivyo kufanya vigumu kwa huduma za msingi kama afya, elimu na harakati za kiuchumi kuwafikia wananchi.