Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya UN na wadau waendelea kusaidia watu wa Haiti licha ya changamoto

Kundi la watu waliohamishwa makazi katika shule moja katikati ya Port-au-Prince, Haiti.
© IOM/Antoine Lemonnier
Kundi la watu waliohamishwa makazi katika shule moja katikati ya Port-au-Prince, Haiti.

Mashirika ya UN na wadau waendelea kusaidia watu wa Haiti licha ya changamoto

Amani na Usalama

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu inaripoti kwamba licha ya ufikiaji mdogo na ukosefu wa usalama nchini Haiti, wadau wa kibinadamu wanaendelea kufanya kila liwezekanalo kuunga mkono juhudi za usaidizi.

“Hata hivyo, ufadhili wa ziada ili kuendeleza operesheni ya msaada unahitajika haraka.” Imeeleza taarifa ya OCHA iliyotolewa leo Machi 14.

Hapo jana, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) liliweza kutoa chakula cha moto kwa watu 13,000 waliokimbia makazi yao. Lakini WFP inasema huduma hii katika mji mkuu wa Port-au-Prince huenda ikafungwa wiki ijayo ikiwa ufadhili mpya hautapatikana. WFP inahitaji dola milioni 10 ili kuweza kuendeleza mpango huu wa kuokoa maisha.

Mapema wiki hii, Mkurugenzi wa WFP Jean-Martin Bauer ameonya kwamba Haiti iko kwenye ukingo wa janga la njaa, na zaidi ya Wahaiti milioni 1.4 wako hatua moja kuangukia kwenye njaa.

Wadau wa matibabu wanasalia na wasiwasi kuhusu hali ya afya kwa ujumla nchini Haiti, hasa uhaba mkubwa wa usambazaji wa damu.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO), la kuhudumia watoto UNICEF, la Uhamiaji (IOM) na mdao wao  Pan American Health Organization kupitia wadau wengine wa kimataifa wanatoa msaada wa matibabu kupitia kliniki zinazohamishika katika maeneo kadhaa ya watu waliofurushwa, pamoja na usaidizi mwingine muhimu, ikiwa ni pamoja na msaada wa maji na kisaikolojia.