Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi za kila mmoja zapunguza vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka 5

Mtoto akipokea chanjo za BCG na polio katika kitengo cha chanjo karibu na Maduka ya Matibabu ya Kati huko Freetown, Sierra Leone.
UNICEF Sierra Leone/2014/James
Mtoto akipokea chanjo za BCG na polio katika kitengo cha chanjo karibu na Maduka ya Matibabu ya Kati huko Freetown, Sierra Leone.

Juhudi za kila mmoja zapunguza vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka 5

Afya

Idadi ya vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka 5 duniani kote imepungua na kufikia kiwango cha chini zaidi kuwahi kufikiwa katika historia, ambapo takwimu mpya zilizotolewa na Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa mwaka 2022 idadi ya vifo ilikuwa chini ya milioni 4.9, sawa na pungufu kwa asilimia 51 tangu mwaka 2000. 

Takwimu hizo zimetolewa na kundi la pamoja la mashirika ya Umoja wa Mataifa linalotoa makadirio ya vifo vya watoto wachanga, UN IGME ambalo linajumuisha mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo la kuhudumia watoto, UNICEF, la afya, WHO, Benki ya Dunia na kitengo cha Idadi ya Watu cha Idara ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Kiuchumi na Kijamii, DESA.

Rwanda na Malawi ni miongoni mwa nchi zilizofanya vizuri

Taarifa ya pamoja iliyotolewa Jumatano na kundi hilo katika majiji ya New York na Washington DC nchini Marekani na Geneva, Uswisi imetaja Cambodia, Malawi, Mongolia na Rwanda kuwa ni nchi ambamo idadi ya vifo vya watoto hao imepungua kwa zaidi ya asilimia 75 kati ya 2000 na 2022.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF Catherine Russel akinukuliwa kwenye taarifa hiyo amepongeza juhudi za wakunga, wahudumu wa afya wakiwemo wale wa kijamii, ambao amesema kujituma kwao ndio kumefanikisha kupungua kwa kiasi kikubwa kwa idadi ya vifo hivyo.

“Miongo kadhaa ya mtu mmoja mmoja, jamii na mataifa kujituma kuhakikisha watoto wanafikishiwa huduma bora na fanisi za afya kwa gharama nafuu, imethibitisha kuwa tuna ufahamu na mbinu za kuokoa maisha,” amesema Bi. Russell.

UN IGME inayoongozwa na UNICEF, iliundwa mwaka 2004 kubadilishana takwimu na kuboresha mbinu kwa ajili ya takwimu za vifo vya watoto na kufuatilia maendeleo kuelekea kufikia malengo kuhusu uhai wa mtoto. 

Safari bado ni ndefu

Licha ya mafanikio hayo, ripoti inaonya kuwa bado safari ni ndefu kufikia lengo la kutokomeza vifo vya watoto vinavyoweza kuzuilika, kwa kuwa mamilioni wanaendelea kufariki dunia kutokana na magonjwa yanayotibika, ikiwemo changamoto za ujauziot, vichomi au numonia,  kuhara na malaria.

Idadi kubwa ya vifo hivyo ni katika nchi za Afrika zilizo Kusini mwa jangwa la Sahara na kusini mwa Asia, hali inayodhihirisha tofauti za kikanda katika upatikanaji wa huduma bora za afya.

Ripoti imetambua pia ukosefu wa utulivu kiuchumi, mizozo, mabadiliko ya tabianchi na changamoto zilizoachwa kutokana na janga la COVID-19, ikisema mambo hayo yanazidi kuchochea tofauti za usawa kwenye utoaji wa huduma za afya.

“Ingawa kumekuweko na maendeleo makubwa, kila mwaka mamilioni ya familia bado zinakabiliwa na machungu ya kupoteza mtoto, mara nyingi siku za mwanzo za uhai wa mtoto huyo,” amesema Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO.

Eneo ambalo mtoto anazaliwa, halipaswi kuamua iwapo ataishi au la. Ni muhimu kuimarisha huduma za afya kwa kila mwanamke na kila mtoto, ikiwemo wakati wa dharura na kwenye maeneo yaliyoko mbali.”

Wahudumu walio mstari wa mbele kwenye majanga

Kuimarisha huduma bora za afya na kuokoa maisha ya watoto dhidi ya vifo vinavyoweza kuzuilika kunahitaji uwekezaji kwenye elimu, ajira, na mazingira bora ya kazi kwa wahudumu wa afya ili waweze kutoa huduma za afya ya msingi, na hii ijumuishe pia wahudumu wa afya wa kijamii.

Juan Pablo Uribe, Mkurugenzi wa Afya, Lishe na Idadi ya Watu katika Benki ya Dunia amesisitiza umuhimu wa kusongesha maendeleo yaliyopatikana.

“Tuna deni kubwa kwa watoto wetu wote kuhakikisha wote wana fursa sawa na huduma sawa za afya bila kujali eneo wanakozaliwa,” amesema Uribe