Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtoto au kijana mmoja anakufa kila baada ya sekunde 4.4 - UN

Mtoto wa miaka miwili akiwa na mamake baada ya kupewa dawa ya kutibu malaria katika zahanati ya kijiji katika wilaya ya Kasungu Malawi.
© UNICEF/UN066838/Hubbard
Mtoto wa miaka miwili akiwa na mamake baada ya kupewa dawa ya kutibu malaria katika zahanati ya kijiji katika wilaya ya Kasungu Malawi.

Mtoto au kijana mmoja anakufa kila baada ya sekunde 4.4 - UN

Afya

Takribani watoto milioni 5 walikufa kabla ya kusherehekea mwaka wao wa tano wa kuzaliwa, ilihali watoto wengine milioni 2.1 pamoja na vijana wenye umri wa kati ya miaka 5 hadi 24 walikufa mwaka 2021. 

Hii ni kwa mujibu wa makadirio ya hivi karibuni zaidi yaliyotolewa na kundi la mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayofuatilia vifo vya watoto, UN IGME kupitia taarifa yao iliyotolewa leo katika miji ya New York na Washington DC Marekani pamoja na Geneva, Uswisi. 

Utashi wa kisiasa ungaliweza kuzuia vifo hivyo 

Sambamba na makadirio hayo mapya, ripoti nyingine ya kando ya kundi hilo imebaini kuwa katika kipindi hicho hicho, watoto milioni 1.9 walizaliwa wafu. “Idadi kubwa ya vifo hivi vingaliweza kuzuiwa kwa kuhakikisha kuna upatikanaji sawa wa huduma bora za afya na zenye ubora wa juu kwa wajawazito, watoto wachanga na vijana  barubaru,”  amesema Vidhya Ganesh, Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF Idara  ya uchambuzi wa data, mipango na ufuatiliji. 

Amesema kila siku, wazazi wengi zaidi wanakumbwa na kiwewe na msongo wa kupoteza watoto wao, na wakati mwingine hata kabla ya pumzi yao ya kwanza. 

“Kusambaa kwa janga hilo linaloweza kuzuilika hakupaswi kukubalika. Maendeleo yanawezekana ikiwa kuna utashi wa kisiasa na uwekezaji unaolenga sekta hiyo kuhakikisha huduma ya afya ya msingi inapatikana kwa kila mama na kila mtoto,” amesema Afisa huyo wa UNICEF. 

Mama akimleta mtoto wake wa miezi sita kufanyiwa uchunguzi wa afya katika kliniki moja huko Chipata, Zambia.
© UNICEF/Karin Schermbrucker
Mama akimleta mtoto wake wa miezi sita kufanyiwa uchunguzi wa afya katika kliniki moja huko Chipata, Zambia.

Karne ya 21 ilipoanza mambo yalikuwa shwari 

Ripoti inaonesha matokeo chanya na hatari ndogo ya vifo miongoni mwa watu wa umri wote tangu mwaka 2000. Ikionesha kuwa vifo vya watoto wachanga vilipungua kwa 50% tangu kuanza kwa karne hii ya 21, huku vifo vya watoto wakubwa na vijana vilipungua kwa asilimia 36 na vifo vya watoto wachanga tumboni vilipungua kwa asilimia 35. 

Hii ilifanikishwa na uwekezaji zaidi uliokuweko katika kuimarisha mifumo ya afya ya msingi ikilenga wanawake, watoto na vijana. 

Hali ilianza kuporomoka mwaka 2010 

Hata hivyo mafanikio yote hayo yaliporomoka tangu mwaka 2010 na nchi 54 zitashindwa kufikia malengo ya maendeleo endelevu kuhusu watoto wenye umri wa chini ya miaka 5. 

“Iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa kuimarisha huduma za afya, takribani watoto milioni 59 na vijana watakufa kabla ya kufikia mwaka 2030 na takribani watoto milioni 16 watazaliwa wakiwa tayari wameshakufa,” yameonya mashirika hayo. 

“Inasikitisha sana kuwa fursa ya mtoto kuishi inatokana na pahali alipozaliwa, na kwamba kuna ukosefu mkubwa wa uwiano kwenye fursa yao ya kupata huduma za afya,” amesema Dkt. Anshu Banerjee Mkurugenzi wa huduma za wajawazito, watoto wachanga, watoto na vijana barubaru katika shirika la Umoj awa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO

Amesema watoto kokote waliko wanahitaji mifumo thabiti ya afya ya msingi, ikikidhi mahitaji yao na ya familia zao ili kokote pale walikozaliwa wana fursa nzuri ya kuanza maisha na wana matumaini ya siku zao usoni. 

Tofauti ya fursa ya kuishi – Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara hali ni tete 

Kauli ya unakozaliwa ndio kunakoonesha utaishi muda gani inadhihirishwa na ripoti hiyo ikisema nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara pamoja na zile za kusini mwa Asia, ndio zina mzigo mkubwa wa vifo vya watoto wachanga, watoto na vijana. 

“Ingawa nchi hizo za Afrika zina 29% ya vifo vyote hai duniani kote, ukanda huo wa Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara linabeba asilimia 56 ya vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka 5 kwa mwaka 2021,” imesema ripoti hiyo huku zile za kusini mwa Asia zikiwa na 26%. 

Await Said anamwangalia mjukuu wake mchanga Ayah, ambaye anasumbuliwa na ugonjwa wa kichocho na uzito wa kilo 1.3 tu, kwani yuko kwenye incubator katika Hospitali ya Ualimu Juba, Juba, Sudan Kusini
© UNICEF/UN0159228/Naftalin
Await Said anamwangalia mjukuu wake mchanga Ayah, ambaye anasumbuliwa na ugonjwa wa kichocho na uzito wa kilo 1.3 tu, kwani yuko kwenye incubator katika Hospitali ya Ualimu Juba, Juba, Sudan Kusini

Kuzaliwa kusini mwa janga la Sahara na kusini mwa Asia ni janga? 

Watoto waliozaliwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi ya vifo utotoni ikilinganishwa na duniani kote ambapo hatari yao ya kufa ni mara 15 zaidi kuliko watoto wanaozaliwa Ulaya na Amerika ya kaskazini. 

Akina mama katika maeneo hayo mawili pia wanakabiliwa na machungu ya kupoteza watoto kwa kuwazaa wafu katika kiwango kisichokubalika ambapo 77% ya vifo mfu vilitokea Afrika na kusini mwa Asia. 

Hatari ya mjamzito kujifungua mtoto mfu kwenye maeneo hayo mawili in mara 7 zaidi uliko Ulaya na Amerika ya kaskazini. 

Juan Pablo Uribe, Mkurugenzi wa afya, lishe na idadi ya watu katika Benki ya Dunia anasema ni vema kutambua kuwa “nyumba ya takwimu au namba hizo ni mamilioni ya watoto na familia ambazo zimenyimwa haki yao ya msingi ya afya.” 

Amesema kinachohitajika ni utashi wa kisiasa na uongozi wa kuendeleza ufadhili kwa huduma ya afya ya msingi ambayo ni moja ya vitegauchumi bora zaidi ambavyo nchi na wadau wa maendeleo wanaweza kufanya. 

COVID-19 kwa kiasi fulani imechangia kurudisha nyuma maendeleo 

Ingawa COVID-19 haijachangia moja kwa moja kwenye vifo vya watoto, kwa kuwa watoto wana uwezo mdogo zaidi wa kufa kwa COVID-19 kuliko watu wazima, janga hilo linaweza kuwa limeongeza hatari yao ya kuishi siku za usoni. 

Ripoti inataja kuvurugwa kwa ratiba za kampeni za chanjo, huduma za lishe na kupata huduma za msingi za afya, vitu ambavyo vitahatarisha afya na ustawi wao kwa miaka ijayo.