Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asante UNFPA kwa kuniaminisha kuwahudumia wajawazito Kenya- Goretti

Mkunga nchini Kenya akitumia kifaa  cha kuchunguza hali ya ujauzito tumboni mwa mama. Kifaa hiki anaweza kwenda nacho kokote kutoa huduma hiyo hata majumbani.
© UNFPA Kenya
Mkunga nchini Kenya akitumia kifaa cha kuchunguza hali ya ujauzito tumboni mwa mama. Kifaa hiki anaweza kwenda nacho kokote kutoa huduma hiyo hata majumbani.

Asante UNFPA kwa kuniaminisha kuwahudumia wajawazito Kenya- Goretti

Afya

Katika miaka yake 4 kwenye kituo cha afya cha Sena, kilichoko kisiwani Mfangano kwenye kaunti ya Homa Bay nchini Kenya, mkunga Goretti Adhiambo ameshuhudia wanawake wengi wakipoteza maisha kutokana na matatizo ya kiafya wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua. 

 “Huwa tunatoa huduma zote za msingi za afya kwenye kituo hiki cha afya ikiwemo huduma za afya ya uzazi, lakini wajawazito ambao hali zao ni tete zaidi na wanahitaji huduma zaidi tunawapa rufaa ya hospitali zilizoko bara,” anasema Bi. Adhiambo.

Kwa mujibu wa makala iliyochapishwa kwenye wavuti wa UNFPA, kituo hiki cha afya cha Sena hadi mjini Mbita  ni mwendo wa angalau saa moja kwa boti na kama hali ya hewa si nzuri basi safari ni saa mbili. Kukitokea dharura yoyote, kuchelewa safarini kunaweza kusababisha madhara makubwa na kumtia hatarini mjamzito.

Katika mwaka 2018, Bi. Adhiambo alishughulikia  mtoto mjamzito aliyekuwa na matatizo wakati wa kijifungua. Mwanamke huyu alipatiwa rufaa ya kwenda mjini Mbita ambako ni bara ili kupata usimamizi maaluk wakati akijifungua.

 “Alikuwa na umri wa miaka 18 pekee, na kupoteza mtoto huyu lilikuwa ni jambo la kuumiza kwangu na kwa wakunga wenzangu,” Anakumbuka Bi. Adhiambo.

Hii leo, Bi. Adhiambo ni mkunga anayehusika na matunzo ya wazawazito na watoto wachanga  pindi wanapozaliwa. Sasa ana kifaa kipya kinachoweza kutambua matatizo ya mjamzito mapema sana kabla ya kuanza kutishia maisha: kifaa hicho husaidia kuona hali ya mtoto akiwa bado tumboni mwa mama yake na kinaitwa kwa kiingereza ‘ultrasound’.

Kuweka vifaa mikononi mwa wakunga

Kwa miaka mingi wanawake wajawazito kwenye Kisiwa cha Mfangano walikuwa wakilazimika kwenda mjini Mbita sio tu kwa huduma za dharura, bali pia kwa ajili ya huduma za kupimwa kwa kutumia kifaa hicho ha Ultrasound ili kufahamu hali ya mtoto tumboni.

Vifaa kama hivi kawaida mara nyingi huwa kwenye vituo maalumu vya afya vipatikanavyo katika miji na majiji. Kutokana na hilo matatizo yatokanayo na ujauzito hubainika kwa kutumia vifaa maalum na pia kwa gharama kubwa, huchelewa kupata tiba au kutoshughulikiwa kabisa. 

Tweet URL

Lakini hali hii imeanza kubadilika.

Katika ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani, UNFPA, Chuo Kikuu cha kimataifa cha AMREF  na Phillips Foundation, wakunga kwenye vituo mbalimbali vya afya mashinani nchini Kenya, wanapatiwa teknolojia ya Ultrasound Mkononi na mafunzo ya jinsi ya kutumia kifaa hicho.

Miongoni mwao ni Bi. Adhiambo ambapo yeye na wenzake walifundishwa jinsi ya kutumia kifaa hicho kijulikanacho kama Lumify Probe. Walifundishwa na wataalamu jinsi ya kutumia kifaa hicho ili kuthibitisha iwpao ujauzito unafaa kuendelea, kubaini hali ya mfuko wa uzazi na pia usalama wa viungo vyote tumboni.

Kutokana na kupata ujuzi wa kutambua matatizo haya, kama hali ya mfuko wa uzazi, wakunga wanaweza kutoa huduma bora, ufuatiliaji na utoaji wa rufaa.
 
“Wakati wakunga wanapopata uwezo wa kutoa huduma za msingi za kutambua hali ya ujauzito tumboni,  uamuzi sahihi kuhusu matatizo yatokanayo na ujauzito hufanyika na kuruhusu rufaa kwa kwa wakati mwafaka kwa ajili ya usimamizi bora,” anasema Priscilla Ngunju, Mratibu wa mradi wa Chuo Kikuu cha AMREF.

Matumaini yetu ni kwamba mwanamke anaweza kupata huduma ya kuchunguzwa ujauzito wake angalau mara moja kabla ya wiki ya 24 ya ujauzito kwa kuzingatia maelekezo ya shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO.

Wawezeshwa kuokoa maisha

Baada ya mafunzo, wakunga walipatiwa kifaa husika Lumify Probe ili wavitumie vituoni. Kwa kuzingatia kwamba kifaa hicho ni chepesi na rahisi kubebwa, wakunga wanaweza kuwa nacho wakati wote wanapotembelea wajawazito majumbani huku wakiongeza wigo wa huduma zao.

Kando na kuondoa gharama za usafiri nje ya kisiwa hadi bara, programu hii imepunguza kabisa gharama za upimaji kwa kuwa katika zahanati nchini Kenya, huduma ya kuchunguzwa hali ya ujauzito tumboni ni saw ana dola 5, huku ikiwa inanweza kuwa maradufu au mara tatu juu zaidi ya huduma maalumu kwenye vituo vya afya. 

Bi. Adhiambo anasema,  anafurahi kuona  kwamba wajawazito ambao hutembelea kituo cha afya cha Sena wataweza kuepuka gharama hizo.

“Nimefahamu mengi kutokana na mafunzo haya ikiwemo kuelewa kutafsiri picha za Ultrasound, kubaini pahala pa kondo la nyuma na kufanya uamui kuhusu matatizo makubwa” aliiambia UNFPA na kwamba “kwa sasa ninaweza kutumia ujuzi wangu kuokoa uhai wa mjamzito.”