Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakulima Kaskazini mwa Haiti na kilimo cha kujijengea mnepo

Mtaalam kutoka WFP Rose Senoviala Desir akiwa na wakulima kaskazini mwa Haiti.
© WFP Haiti/Theresa Piorr
Mtaalam kutoka WFP Rose Senoviala Desir akiwa na wakulima kaskazini mwa Haiti.

Wakulima Kaskazini mwa Haiti na kilimo cha kujijengea mnepo

Ukuaji wa Kiuchumi

Wakulima wa kaskazini mwa Haiti wanajitahidi kujijengea mnepo wa kustahimili hali mbaya ya hewa ili kujaribu kujilinda vyema kutokana na upotevu wa mali na mazao ambao mara nyingi hutokana na majanga ya asili.

Idadi kubwa ya wakazi wa vijijini hasa kaskazini mwa taifa hilo wanakabiliwa na janga la njaa na taarifa hizo in kutokana na ripoti ya hivi karibuni ya pamoja ya uhakika wa chakula au IPC ambayo inatoa muhtasari wa undani na ukubwa wa ukosefu wa uhakika wa chakula na utapiamlo.

Serikali ya Haiti, shiŕika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani (WFP) na wadau wengine, wamekuwa wakiwasaidia wakulima katika kanda hiyo wakati huu wanapoibuka kutoka katika mzunguko wa madhara ya ukame na mafuriko. Wengi wamelipwa ujira kwa kufanya kazi kwenye miradi ambayo imewajengea mnepo katika jamii zao. Kama ilivyo kwa wakulima kote ulimwenguni, nao pia wanajivunia mwenendo wao wa maisha na mimea wanayopanda na wana nia ya kuandaa maisha ya baadaye kwa familia zao. Hizi ni simulizi zao tatu.

Mariette Samson: “Nilipoteza maharagwe yote”

Mariette Samson alipoteza mazao yake kufuatia mafuriko kijijini kaskazini mwa Haiti.
© WFP Haiti/Theresa Piorr
Mariette Samson alipoteza mazao yake kufuatia mafuriko kijijini kaskazini mwa Haiti.

“Mashamba yetu yanapofurika, tunapoteza mazao yetu yote. Mnamo Januari, nilipoteza maharagwe na mahindi, ndizi, viazi, viazi vikuu na malenge au maboga. Shamba hili linalisha familia ya watu 10, lakini tulikuwa hatuna chakula. Nimekuwa nikifanya kazi katika shamba la jirani yangu ili nami niweze kupata kiasi cha mavuno kutoka kwake. Leo hii ni wajukuu wangu watatu tu ndio wamekula; walinipatia kahawa na mkate na sasa ninatayarisha maharagwe kwa ajili ya familia yote ambao utakuwa mlo wetu kwa siku ya leo.

Nimepanda mazao kwa ajili ya msimu ujao na kwa hiyo tutakuwa na chakula tena mwaka huu, lakin hadi wakati huo tutakaa na njaa.

Nimechangia pia katika kazi kwa ajili ya jamii hapa Dubuisson kati ya Julai na Septemba mwaka jana kwa ajili ya kujenga miundombinu ambayo itadhibiti athari za mafuriko na ujira niliolipwa umenisaidia sana.

Marc Magloire: “Nakula viazi sukari kila Jumapili”

Marc Magloire akiwa amebeba mazao yake.
© WFP Haiti/Theresa Piorr
Marc Magloire akiwa amebeba mazao yake.

"Ardhi iliyoko Limonade ina rutuba na tunapata mvua nyingi, lakini mara kwa mara tumekuwa tukipata ugumu wa kumwagilia maji mimea. Tulishirikiana na WFP kuchimba mifereji ya umwagiliaji katika mashamba yote ya wanachama wa chama chetu cha wakulima 200 na sasa tunaweza kusukuma maji ili kukuza aina mbalimbali za mazao mapya, ikiwa ni pamoja na biringanya, kabichi, mchicha, vitunguu na viazi sukari au beetroot kwa lugha ya kiingereza. Sasa ninaweza kula saladi ya kiasi sukari tena kila Jumapili, desturi ya nyumbani ambayo ninafurahia.

Kabla ya umwagiliaji, wakati wa ukame tulikuwa tunakula mlo mmoja tu kwa siku, lakini sasa tunaweza kula mara tatu kwa siku na pia kuuza chakula ili kulipia mahitaji ya familia zetu.

Najivunia kuwa mkulima, haya ndio maisha yangu; ni maisha mazuri. Watoto wangu wataendeleza utamaduni wa kilimo ambao ni thabiti katika mkoa huu.

Elie Devil: “Niliepusha mwembe usikatwe"

Elie Devil akiwa amesimama mbele ya mwembe alioepusha usikatwe.
© WFP Haiti/Theresa Piorr
Elie Devil akiwa amesimama mbele ya mwembe alioepusha usikatwe.

“Jirani yangu alitaka kuukata mwembe wa zamani ili achome mkaa, lakini nilimzuia kufanya hivyo kwani najua ukataji miti unasababisha mmomonyoko wa udongo ambao unawadhuru watu wote na hususan wakulima wa Pilette ninakoishi.

Nilifahamu kuhusu umuhimu wa upandaji miti ili kulinda udongo na kuzuia mafuriko kama sehemu ya mradi wa shirika la chakula duniani, WFP na nina nia ya kuhakikisha upanzi wa miti mingi ya miembe, parachichi, kakao na kahawa. Hivi vitalinda mazingira yetu na kutupatia chakula chenye lishe. Kama jamii, tulifanya kazi pamoja ili kuhakikisha tunajikinga dhidi ya mafuriko katika mitaro ya maji ambayo hutiririka mtoni. Hii ilizuia udongo kutoka kwenye milima, lakini tunahitaji kufanya mengi zaidi kwani mvua kubwa za hivi majuzi bado zilisababisha uharibifu kwenye bonde.

Hali ya hewa inabadilika katika eneo hili; mvua inapungua na sio ya kutegemewa, watu wengi kama jirani yangu wanataka kukata miti wachome mkaa na hatimaye waweze kupata kipato na kuishi. Hapo awali, mvua zilikuwa zinanyesha mara kwa mara na kwa hivyo kulikuwa na chakula zaidi na ni mara chache mafuriko yalisomba mazao yetu ya chakula, kwa hivyo watu hawakuhitaji kukata miti kuchoma mkaa. Jirani yangu hazungumzi nami tena, lakini sijali kwa sababu niliokoa mwembe huo.”

Rose Senoviala Desir, mtaalam wa kilimo na uchumi WFP: “Wakulima wanafahamu kinachohitajika kufanywa”

Rose Senoviala Desir kutoka WFP
UN Haiti/Daniel Dickinson
Rose Senoviala Desir kutoka WFP

 

Kuna utamaduni thabiti wa kilimo kaskazini mwa Haiti na wakulima wanataka kuhifadhi mienendo yao ya maisha na kuhakikisha mustakabali salama kwa familia zao. Mabadiliko ya tabianchi ambayo yamesababisha hali ya hewa kutotabirika ikiwemo ukame na mvua kubwa inayosababisha mafuriko

yameathiri vibaya jamii hizo. Ukataji miti kote kaskazini umechangia ongezeko la athari hizi zinazohusiana na hali ya hewa na kwa hivyo WFP imechukua hatua mbali mbali kukabiliana na hilo ili kupunguza athari mbaya na kuwajengea mnepo wakulima.

Hizi ni pamoja na hatua za kuzuia ambazo husaidia kudhibiti mtiririko wa maji kutoka kwenye milima, kwa mfano ukarabati wa njia za umwagiliaji na mabonde madogo ya maji na upandaji wa miche ya miti ili kuzuia mmomonyoko. Pia husaidia kuzuia mafuriko na kuhakikisha kuwa maji yanayopatikana yanatumika vizuri. Takriban watu 17,750 wamelipwa ujira kushiriki katika miradi hii.

Jamii hizi za wakulima zinafahamu nini kifanyike; hii ni ardhi yao na urithi wao. Hawana rasilimali zilizopo, ndiyo maana msaada wa WFP, wadau wake na wafadhili ni muhimu sana.