Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haiti: Misaada inaendelea licha ya hatari dhidi ya wafanyakazi - OCHA

Zaidi ya watu 160,000 kwa sasa wamekimbia makazi yao katika eneo la mji mkuu wa Port-au-Prince nchini Haiti.
© IOM
Zaidi ya watu 160,000 kwa sasa wamekimbia makazi yao katika eneo la mji mkuu wa Port-au-Prince nchini Haiti.

Haiti: Misaada inaendelea licha ya hatari dhidi ya wafanyakazi - OCHA

Amani na Usalama

Jumuiya ya kibinadamu nchini Haiti inaendelea kufanya kila iwezalo kutoa msaada kwa watu wenye uhitaji, licha ya hatari kwa usalama wa wafanyakazi wanaosambaza misaada hiyo, imeeleza taarifa iliyotolewa leo Machi 11 na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya dharura na kiutu.

Tangu mwishoni mwa Februari, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na washirika wake wamewasilisha zaidi ya milo 50,000 kwa watu ambao wamekimbia makazi yao. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) wametoa karibu galoni 70,000 za maji na vifaa vingine vya makazi ya dharura.

Umoja wa Mataifa na wadau wake pia walisambaza vifaa 1,500 vya usafi kwenye maeneo ambayo watu waliofurushwa na ghasia wanaishi.

“Hata hivyo, msaada huu wa kibinadamu hautoshi. Pande zinazousika na mzozo huu lazima zitoe nafasi ya ufikiaji usiozuiliwa, salama wa kibinadamu bila masharti.” Inasema Ocha.

Familia zilizohamishwa zinafadhiliwa katika shule iliyo katikati mwa Port-au-Prince, Haiti.
© IOM/Antoine Lemonnier
Familia zilizohamishwa zinafadhiliwa katika shule iliyo katikati mwa Port-au-Prince, Haiti.

Ukosefu wa usalama umeilazimu WFP kusitisha huduma yake ya usafiri wa baharini. Huku barabara zikiwa zimefungwa, hiyo ndio ilikuwa njia pekee ya kusafirisha chakula na dawa kwa mashirika ya misaada na maendeleo kutoka mji mkuu Port-au-Prince hadi maeneo mengine ya Haiti

Washirika wa kibinadamu wanaripoti uhaba wa dawa na vifaa vya matibabu, pamoja na damu, vitanda na wafanyakazi wa kutibu wagonjwa wenye majeraha ya risasi kutoka maeneo karibu na Port-au-Prince.

Wanawake wameathiriwa kwa kiasi kikubwa na ghasia na wanachangia zaidi ya nusu ya wale waliokimbia makazi yao. Ikiwa vurugu zitaendelea, wanawake wajawazito 3,000 hivi huko Port-au-Prince huenda wasipate huduma ya matibabu wanayohitaji.

Mpango wa Mahitaji na Hatua za Kibinadamu wa mwaka huu kwa Haiti, ambao unahitaji dola milioni 674, unafadhiliwa kwa asilimia 2.6 tu, na ni dola milioni 17.7 zimepokelewa. Ufadhili wa ziada unahitajika haraka kusaidia watu wa Haiti.