Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN na wadau watoa wito wa mshikamano Haiti, wakati kipindupindu kikiibuka tena

Kunawa mikono kunasaidia kuzia maambukizi ya kipindupindu
UN News/Daniel Dickinson
Kunawa mikono kunasaidia kuzia maambukizi ya kipindupindu

UN na wadau watoa wito wa mshikamano Haiti, wakati kipindupindu kikiibuka tena

Msaada wa Kibinadamu

Umoja wa Mataifa na jumuiya ya misaada ya kibinadamu nchini Haiti leo wametoa wito wa kufunguliwa mara moja kwa upenyo wa kibinadamu ili kuruhusu kuondoka kwa mafuta kutoka kwenye kituo cha Varreux huko Port-au-Prince, kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya haraka ya wakazi wakati huu kukiwa kumezuka tena ugonjwa wa kipindupindu.

Kuzuiwa kwa kituo kikuu cha Varreux, ambacho ni kituo kikuu cha kuingilia mafuta nchini Haiti, kwa wiki kadhaa sasa kumesababisha kufungwa kwa vituo vya afya, na kupelekdea kusitishwa kwa huduma za kusafisha maji zinazofanywa na kurugenzi ya kitaifa ya maji ya kunywa na usafi wa mazingira ya Haiti (DINEPA) na makampuni binafsi yanayozalisha na kusambaza maji yaliyosafishwa.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya video kutoka Haiti naibu mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa na mratibu wa masuala ya kibinadamu nchini humo  Ulrika Richardson amesema "Upatikanaji wa maji ya kunywa, usafi wa mazingira na huduma za afya umetatizwa sana, wakati ni huduma muhimu sana katika kuzuia na kukabiliana haraka na kipindupindu,”

Ameongeza kuwa hadi sasa visa 11 vya kipindupindu vimethibitishwa, ikiwa ni pamoja na vifo saba vilivyothibitishwa na kwa sasa kuna kesi 111 zinazoshukiwa.

Bi. Richardson amesema, milipuko ya kipindupindu "inaweza kuibuka haraka sana na idadi halisi tunayofikiria inaweza kuwa kubwa zaidi."

Mratibu huyo wa misaada ya kibinadamu ameelezea wasiwasi wake juu ya kukatizwa kwa usambazaji wa maji na kubainisha kuwa "maji safi ni mojawapo ya chahu za mlipuko wa kipindupindu na kuokoa maisha wakati wa mlipuko wa kipindupindu. Hivi sasa maji ya kunywa ni vigumu sana kupata, na usafi wa mazingira na huduma za afya zimeathiriwa sana. .”

Amesisitiza kuwa “bila mafuta hakuna maji safi, bila maji safi kutakuwa na ongezeko la wagonjwa wa kipindupindu na itakuwa vigumu sana kudhibiti mlipuko huo.”

Walio hatarini zaidi ndio wa kwanza kuteseka

Mgogoro ambao Haiti unapitia unaathiri idadi ya watu katika eneo lote na watu walio hatarini zaidi ndio wa kwanza kuteseka kutokana na vizuizi, kutokana na kudorora kwa hali ya uendeshaji wa vituo na hospitali nyingi za afya, wagonjwa wanaougua magonjwa ya muda mrefu, wajawazito, watoto na watoto wachanga ndio wa kwanza kuathirika na ugumu wa kupata huduma za afya msingi. Ameeleza mratibu huyo.

Katika kipindi cha miezi mitatu ijayo, amesema Urlka “Baadhi ya wanawake wajawazito 28,900 na zaidi ya watoto wachanga 28,000 wako katika hatari ya kutopata huduma za afya, wakati matatizo 9,965 ya uzazi yatakosa kutibiwa. Kwa kuongezea, mzozo wa mafuta unaweza kuzidisha zaidi uhaba wa chakula nchini, ambao tayari ungefikia asilimia 45% ya watu kulingana na makadirio yaliyofanywa mnamo Machi 2022.”

Haha hivyo amesema "Tunafanya kazi kwa karibu sana na serikali na tunaipongeza kwa uongozi wa kitaifa katika kukabiliana na hali hii, lakini tunatambua kwamba kwa hali ya sasa ya Haiti tunaweza kukabiliwa na ongezeko kubwa lavisa vya kipindupindu. Na kwa bahati mbaya mtu anaweza hata kusema kwamba pengine hali zipo kwa ajili ya kuleta zahma kubwa.”

Hali ni mbaya zaidi maeneo 36

Umoja wa Mataifa na washirika wa misaada ya kibinadamu wana wasiwasi hasa kuhusu hali ya hatari katika maeneo 36 ya papo hapo katika eneo la mji mkuu wa Port-au-Prince, ambayo yana takriban watu 21,600 waliokimbia makazi yao kutokana na ghasia za hivi karibuni za magenge ya wahalifu. 

Katika baadhi ya maeneo, upatikanaji wa huduma za kimsingi kama vile maji, usafi wa mazingira na huduma zingine za kujisafi vimekatizwa, na hivyo kuimarisha mazingira yanayowezesha kuenea kwa kipindupindu.

Ingawa kinaweza kusababisha vifo bila uangalizi wa haraka wa matibabu, kipindupindu kinaweza kuzuilika na kutibika. 

Mratibu huyo amesema ingawa kuna visa vilivyothibitishwa, vinavyoshukiwa na vifo vilivyotokea bado kuna wakati wa kukomesha kuenea kwa ugonjwa huo.

Umoja wa Mataifa na washirika wake wamekumbusha "Umuhimu wa kuheshimu kanuni za kibinadamu za ubinadamu, kutoegemea upande wowote, kutopendelea na kujitegemea katika kuanzisha na kudumisha ufikiaji wa watu walioathiriwa na hali ya hatari".