Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Polisi hawakuingilia kati mashambulio dhidi ya raia Haiti Novemba 2018- Ripoti

Kwenye mji mkuu wa Haiti, Port au Prince kamisheni ya kitaifa ya ushirikiano nchini haiti sambamba na UNESCO wakifundisha wanafunzi uandishi wa simulizi
Leonora Baumann / MINUJUSTH
Kwenye mji mkuu wa Haiti, Port au Prince kamisheni ya kitaifa ya ushirikiano nchini haiti sambamba na UNESCO wakifundisha wanafunzi uandishi wa simulizi

Polisi hawakuingilia kati mashambulio dhidi ya raia Haiti Novemba 2018- Ripoti

Amani na Usalama

Hatimaye Umoja wa Mataifa umetoa ripoti ya  uchunguzi wa kile kilichotokea huko eneo la Saline, kwenye mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince tarehe 13 na 14 mwezi Novemba mwaka jana wa 2018 ambako watu 26 waliuawa sambamba na matukio  ya ubakaji wa magenge.

Ripoti hiyo imeandaliwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya usaidizi wa kisheria, Haiti, MINUJUSTH, na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR ambao walichunguzi matukio hayo ya siku mbili ambapo magenge matano yenye silaha yalifanya shambulizi la kupangwa kwenye maeneo ya makazi ya watu wanaodaiwa kuwa na uhusiano na magenge ya upinzani.

Matukio ya uchunguzi huo yamebainisha pamoja na mambo mengine kuwa shambulio huko Saline lilidumu kwa takribani saa 14 bila ya polisi wa Haiti kuingilia kati.

“Saa 3 za mwanzo, mashambulizi yalikuwa mabaya sana, wafuasi wa genge husika waliweza kushambulia wakazi bila hofu yoyote ya polisi wa Haiti, PNH kuingilia kati licha ya vituo viwili vidogo vya polisi kuwepo takribani kilometa moja kutoka eneo hilo,” imesema ripoti hiyo.

Kwa mujibu wa shuhuda zilizotolewa, magari ya polisi wa Haiti yalikuwepo karibu na kitongoji cha Saline yakifanya doria kwa takribani saa 2 wakati wa shambulio.

Ripoti imesema kuwa saa 9 alasiri, mkuu wa kituo cha polisi Saline alijulisha idara ya juu kuhusu shambulio hilo “lakini mhusika alisema kuwa walitaka kuingilia kati ili kulinda raia lakini hawakuwa na rasilimali za kutosha na kwamba silaha walizokuwa nazo zilikuwa na uwezo wa kulinda kituo cha polisi peke ambako maafisa watatu walikuwa zamu.”

Kwa kuzingatia matokeo ya uchunguzi huo, “ripoti imeibuka hoja kadhaa kuhusu ukiukwaji wa  haki uliotekelezwa dhidi ya wakazi wa eneo la La Saline na madai ya kuhusika kwa baadhi ya mawakala wa serikali.”

Ripoti imerejelea wajibu wa serikali ya Haiti ya kuzingatia sheria za haki za biandamu za kimataifa na ikipendekeza mambo kadhaa ikiwemo kuhakkisha wahusika wa matukio hayo wanafikishwa mbele ya sheria wakiwemo watumishi wa umma.

Pendekezo lingine ni hatua sahihi zichukuliwe kuhakikisha usalaa, utu wa kimwili na kisaikolojia kwa manusura na mashuhuda ambao wamewasilisha malalamiko yao kuhusiana na matukio hayo, ikitaka pia uangalizi maalum kwa watoto na manusura wa ukatili wa kingono.

Hitimisho la ripoti hiyo linatoa angalizo kuhusu mazingira ya wakazi wa La Saline ambayo yamezidi kuzorota baada ya shambulio hilo, hususan hali ya huduma za msingi kama vile maji safi na salama ya kunywa, afya na elimu.

Wakati wa uchunguzi huo, maafisa walikutana na manusura pamoja na familia zao, mashuhuda, wawakilishi wa mashirika ya kiraia nchini Haiti pamoja na taasisi za umma kama vile mahakama.