Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakiwa Somalia, viongozi wa OCHA na FAO waona ujasiri na mnepo wa wanawake

Beth Bechdol ambaye ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO (kulia) na Joyce Msuya, Naibu Mkuu wa OCHA, (kati) wakiwa kwenye picha ya pamoja na wanawake na wanaume, wakati wa ziara yao  ya pamoja nchini Somalia.
FAO
Beth Bechdol ambaye ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO (kulia) na Joyce Msuya, Naibu Mkuu wa OCHA, (kati) wakiwa kwenye picha ya pamoja na wanawake na wanaume, wakati wa ziara yao ya pamoja nchini Somalia.

Wakiwa Somalia, viongozi wa OCHA na FAO waona ujasiri na mnepo wa wanawake

Msaada wa Kibinadamu

Tunaondoka Somalia tukiwa na simulizi za wengi akiwemo mwanamke mmoja mkimbizi wa ndani kwa zaidi ya miaka 10 lakini sasa ni mfugaji anayeweza kutunza familia yake, amesema Joyce Msuya, Naibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya dharura na kiutu, OCHA.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Mogadishu, Somalia leo baada ya ziara ya siku mbili na nusu akiambatana na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo, FAO, Beth Bechdol, Bi. Msuya amesema mwanamke huyo licha ya kuwa mkimbizi wa ndani anajihusisha na kilimo ambacho kimemwezesha kununua mbuzi anayempatia maziwa bora kwa ajili ya familia yake.

Kilimo na ufugaji vyamkomboa mkimbizi wa ndani

“Ameweza pia kupata fedha ya kupeleka watoto wake shuleni,” amesema Bi. Msuya ambaye yeye pia na Bi. Bechdol waliweza kushiriki maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kwenye kambi za wakimbizi wa ndani za Kaharey na Qansahley huko Doolow.

Msingi wa uimara wa wanawake wa Somalia, wajasiriamali, wakulima ambao wamepitia magumu lakini bado wana ujasiri wa kusonga mbele, vimenitia moyo sana,” ameongeza Bi. Msuya.

Ameshukuru serikali ya Somalia na wananchi wake kwa ukarimu wao wakati wa ziara hiyo ya pamoja ya viongozi hao wa FAO na OCHA akisema ushirikiano baina ya mashirika ya Umoja wa Mataifa ndio jawabu la kufanikisha utatuzi endelevu wa kile kinachowakumba wananchi wa Somalia.

Beth Bechdol ambaye ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO (kulia) na Joyce Msuya, Naibu Mkuu wa OCHA, (kati) wakiwa kwenye picha ya pamoja na wanawake wakulima, wakati wa ziara yao  ya pamoja nchini SomaliA.
FAO
Beth Bechdol ambaye ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO (kulia) na Joyce Msuya, Naibu Mkuu wa OCHA, (kati) wakiwa kwenye picha ya pamoja na wanawake wakulima, wakati wa ziara yao ya pamoja nchini SomaliA.

Changamoto hazijatowesha uimara na mnepo wa wasomali

“Kila mahali nilipokwenda niliguswa mno na uimara, mnepo, ujasiri na azma kwa maslahi ya wannchi wote wa Somalia, kuanzia kwenye jamii hadi serikali kuu. Katika kambi ya wakimbizi wa ndani nilivutiwa na jinsi wenyeji na wakimbizi wa ndani wanavyoishi kwa utangamano na kwa amani,” amesema Bi. Msuya.

Amegusia pia madhara ya mabadiliko ya tabianchi kuanzia ukame, mafuriko na kusema inatia moyo sana kuona jinsi gani baa la njaa liliweza kuepukwa kutokana na juhudi za kila pande. Lakini pia ni vema kutambua kuwa Somalia inakabiliwa na janga la madhara ya tabianchi ambalo haikusababisha.

 “Madhara makubwa zaidi ya tabianchi bado hayajaisha. Ziara yetu hapa ililenga kuchechemua usaidizi zaidi wa kimataifa kwa Somalia, kiutu, tabianchi na mendeleo,” amesema Bi. Msuya.

Tumeona mabadiliko chanya Somalia- Bechdol 

Kwa upande wake, Bi. Bechdol pamoja na kushukuru wote waliofanikisha ziara yao na alichondoka nacho ni mabadiliko makubwa chanya yaliyopatikana nchini humo.

“Hii ni Somalia ambayo haikuwa hivi miaka 10 au 20 iliyopita, na juhudi ambazo Serikali Kuu, wananchi wa Somalia, wadau, wahisani na jamii wameunganisha ili kurekebisha na kuleta amani, utulivu na ahadi za maendeleo licha ya vikwazo vikubwa, vikwazo ambavyo baadhi vipo. Haya ni mambo ambayo ninaondoka nayo,” amesema Naibu Mkurugenzi Mkuu huyo wa FAO.

Amegusia kwa kina suala la kilimo akisema ni wakati wa mabadiliko ili kiweze kuwa na tija zaidi.

“Kile nilichoshuhudia hapa, ni mwanzo wa kile ninachofikiria kuwa ni mabadiliko makubwa ya jinsi chakula na kilimo hapa Somalia kinashughulikiwa. Hii inatokana na serikali yenyewe kwa ahadi yake ya dhati ya kuleta mabadiliko, kuwekeza, kujenga mfumo unaotakiwa kwenye chakula na kilimo chenye tija kiuchumi,” amesema Bi. Bechdol.

Mambo hayo ni mbegu bora, ufugaji wenye tija, mafunzo, utafiti kwa wakulima wadogo, nchini kote na utatuzi wa tatizo la muda mrefu la maji kwa ajili ya umwagiliaji.