Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola bilioni 3.6 zahitajika kukwamua watoto mwaka 2018- Unicef

Maji ni moja ya mahitaji ya msingi ya kuendeleza maisha, lakini kwa wastani watu milioni 117 hawana maji safi na salama katika nchi zinazokumbwa na mgogoro. Picha: UNICEF

Dola bilioni 3.6 zahitajika kukwamua watoto mwaka 2018- Unicef

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limetangaza ombi la dola bilioni 3.6 kwa ajili ya kufikisha misaada ya kibinadamu kwa watu milioni 82 wakiwemo watoto. Taarifa zaidi na Selina Jerobon.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limetangaza ombi la dola bilioni 3.6 kwa ajili ya kufikisha misaada ya kibinadamu kwa watu milioni 82 wakiwemo watoto. Taarifa zaidi na Selina Jerobon.

 (Taarifa ya Selina Jerobon.)

Vita, majanga ya asili na yale yasababishwayo na binadamu pamoja na vitendo vya ukatili, vimekuwa chanzo cha watoto kulazimika kukimbia makwao.

Kuanzia Bangladesh, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Sudan Kusini, watoto hawapati tena fursa ya kuwa watoto.

Maradhi, ujinga wa kutokujua kusoma na kuandika pamoja na umaskini vikiwa ndio marafiki wao wa kudumu.

Kwa kuzingatia hilo hii leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto,  UNICEF limetangaza ombi la dola bilioni 3.6 kwa ajili ya usaidizi wa kibinadamu kwa mwaka 2018, likilenga watu milioni 86 ambapo kati yao milioni 45 ni watoto.

UNICEF inasema asilimia 84 ya ombi hilo linaelekezwa nchi zenye mahitaji kutokana na mizozo.

Manuel Fontaine ambaye ni mkurugenzi wa UNICEF anayehusika program za dharura akizungumza na waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi amesema fedha zinalenga nchi 51 na kwamba wakiweza kupata fedha hizo na uwezo wa kufikia wahusika…

(Sauti ya Manuel Fontaine)

Tunatarajia kufikisha huduma ya maji safi na salama kwa watu milioni 35.7, tutapatia chanjo watoto milioni 10 dhidi ya Surua, na pia tutajaribu kuwapatia elimu rasmi ya msingi na isiyo rasmi kwa watoto takribani milioni 9, na pia tutawapatia tiba watoto milioni 4.2 dhidi ya utapiamlo uliokithiri na pia usaidizi wa kisaikolojia kwa takribani watoto milioni Nne.”

Fungu kubwa zaidi la fedha linakwenda Syria kuhudumia watoto wakimbizi na waliokimbilia nchi jirani ilihali Yemen ni ya pili.  Maeneo mengine ni Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi, Kenya na Somalia.