Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu bora bado ‘kizungumkuti’ kwa watu wenye ualbino - Miti-Drummond

Nchini Tanzania, chama cha watu wenye ualbino, TAS kinaendesha programu za kuelimisha watu kuhusu haki za watu wenye ualbino. Pichani ni mkoani Morogoro, mashariki mwa Tanzania, mafunzo yakiendelea kwa wanafunzi.
UN News
Nchini Tanzania, chama cha watu wenye ualbino, TAS kinaendesha programu za kuelimisha watu kuhusu haki za watu wenye ualbino. Pichani ni mkoani Morogoro, mashariki mwa Tanzania, mafunzo yakiendelea kwa wanafunzi.

Elimu bora bado ‘kizungumkuti’ kwa watu wenye ualbino - Miti-Drummond

Haki za binadamu

Ijapokuwa maendeleo yamefikiwa duniani kote la kuhitimu elimu ya msingi na sekondari kwa mujibu wa lengo namba 4 la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, bado kwa watu wengi wenye ualbino, elimu bora imesalia kuwa ndoto, amesema hii leo mtaalamu wa Umoja wa Mataifa.

“Haki ya elimu ‘inapigiwa debe’ kama haki ya kimataifa inayotambuliwa kisheria lakini vikwazo lukuki vinazuia watu wenye ualbino kupata haki hii,” amesema Muluka-Anne Miti-Drummond, ambaye ni mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wenye ualbino.

Kupitia ripoti yake aliyowasilisha leo mbele ya Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu, kikao cha 55, HRC55 huko Geneva, Uswisi, mtaalamu huyo ametaja miongoni mwa vikwazo vya elimu bora ni kutojumuishwa kwa watu wenye ualbino katika mitaala ya elimu, michezo na elimu ya juu; ukosefu wa malazi yanayokidhi mazingira yao ikiwemo vifaa vya usaidizi; changamoto wakati wa safari; hofu ya kuathiriwa na mionzi ya juu inayoweza kusababisha saratani; na unyanyapaa na ubaguzi ambavyo mara nyingi huwatumbukiza kwenye kuonewa shuleni.

“Nina masikitiko makubwa juu ya ripoti nyingi za kuonewa kwa watu wenye ualbino na kunyanyaswa, ikiwemo vitendo hivyo kufanywa na walimu, vitu ambavyo vinasababisha washindwe kumaliza shule na vile vile kupata elimu  ya kutosha,” amesema Miti-Drummond.

Nini kifanyike sasa?

Muluka-Anne Miti-Drummond, Mtaalamu wa UN kuhusu haki za binadamu kwa watu wenye ualbino
© Global Albinism
Muluka-Anne Miti-Drummond, Mtaalamu wa UN kuhusu haki za binadamu kwa watu wenye ualbino

Mtaalamu huyo anasema juhudi za makusudi zinahitajika hasa miongoni mwa watumishi wa sekta ya elimu. “Hii itasaidia kutatua mzizi wa visababishi vya unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya watu wenye ualbino unaofanyika nchi kadhaa.”

Amesema elimu lazima iundwe kulingana na mahitaji ya watu wenye ualbino, kwa kuwa nao ni watu wenye ulemavu kutokana na uhafifu wa uoni na hatari kubwa waliyo nayo ya kupata saratani.

Kwa nchi maskini vikwazo ni vingi zaidi

Bi. Miti-Drummond ametanabaisha kuwa kwa nchi za kipato cha chini ambako watu wenye ulemavu hawawezi kupata vifaa vya usaidizi, vikwazo ni vingi zaidi katika kupata elimu.

Lakini hali si shwari sana pia kwa wale walioko nchi za kipato cha juu kwani kundi hilo nalo linahaha kupata elimu bora hivyo ni lazima hatua za kimataifa zichukuliwe kuondoa vikwazo hivyo.

Baadhi ya nchi zimesonga mbele kuondoa vikwazo

Licha ya changamoto, baadhi ya nchi zimechukua hatua kupatia kundi hilo malazi sahihi wakati wa masomo darasani na wakati wa mtihani kwa lengo la kupunguza hatari ya kupata saratani. Wanapatiwa pia mafuta ya Ngozi na pia vifaa vya kuwawezesha kusoma.

Soma taarifa nzima hapa