Skip to main content

Tuwajumuishe watu wenye ualbino kwenye mijadala:UN 

Lucas na kaka yake wote wana  ualbino ambao unasababisha ngozi yao kupata matatizo na uoni wao ni hafifu.
UNICEF
Lucas na kaka yake wote wana ualbino ambao unasababisha ngozi yao kupata matatizo na uoni wao ni hafifu.

Tuwajumuishe watu wenye ualbino kwenye mijadala:UN 

Haki za binadamu

Ikiwa leo dunia inaadhimisha siku ya kimataifa ya kuelimisha jamii kuhusu watu wenye ualbino, Umoja wa Mataifa umetoa  rai kwa nchi zote duniani kuwajumuisha watu wenye ualbino katika mijadala na mipango inayoathiri haki zao za kibinadamu, ili kuhakikisha wanafurahia usawa na ulinzi unaotolewa kwao katika sheria na viwango vya kimataifa.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu inasema ”Tuungane pamoja kufanya sauti zetu zisikike” ikihamasisha haja ya kufanya kazi pamoja na kujenga ushirikiano ili kukabiliana na changamoto za haki za binadamu zinazowakabili watu wenye ualbino. 

Mtaalam Huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu ualbino Muluka-Anne Miti-Drummond amesema kupitia taarifa yake aliyotoa leo mjini Geneva Uswisi kuwa sehemu za kufanya maamuzi kuanzia ngazi za kimataifa, kitaifa , kijamii na hata katika sekta binafsi kumekosa uwakilishi wa watu wenye ualibino na hivyo wanashindwa kushiriki katika mijadala ya kufanya maamuzi na hali hiyo inaweza kusababisha ukiukwaji wa haki zao za kibinadamu. 

Amesema,  “ni ubaguzi wa kimuundo na ukosefu wa usawa wa kihistoria. Hakuwezi kuwa na usawa bila kujumuishwa kwa sauti za walio hatarini zaidi. Ikiwa hatutajumuisha watu wenye ualbino katika majadiliano na maamuzi, tunaendeleza ubaguzi wa kimuundo na ukosefu wa usawa wa kihistoria. Hakuwezi kuwa na usawa bila kujumuishwa kwa sauti za walio hatarini zaidi.”

Wakati baadhi ya nchi zikipiga hatua katika nyanja za afya, elimu na ajira, bado dunia imeendelea kushuhudia mauaji ya watu wenye ualbino kwasababu za kishirikiana, kubaguliwa, kuonewa pamoja na vikwazo vya kimtazamo dhidi yao. Pamoja na hayo yote, masuala ya haki za binadamu na sera zinazotengenezwa ili kukabiliana na masuala yanayowahusu zinaendelea kuwaacha nyuma watu wenye ualbino.

Mtaalamu huru Drummond ameongeza kuwa pamoja na mafanikio yaliyofikiwa tangu mwaka 2015 watu wenye ualbino bado wana safari ndefu katika kufikia usawa na kutambuliwa katika nyanja mbalimbali za jamii.

Maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kuelimisha jamii kuhusu watu wenye ualbino mwaka huu pia yanasherehekea kazi zilizofanywa na vikundi vya wenye ualbino katika kupaza sauti zao nakuhamasisha kuendeleza mshikamano wakati wakiendelea kupambana kuhakikisha sauti zao zinasikika.