Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko mliojitoa kimasomaso kutetea wenye ualbino- Guterres

Watu wenye ualbino mara nyingi wanakuwa na uoni hafifu na wanahitaji matunzo maalum ili waweze kujikinga na jua.
Corbis Images/Patricia Willocq
Watu wenye ualbino mara nyingi wanakuwa na uoni hafifu na wanahitaji matunzo maalum ili waweze kujikinga na jua.

Heko mliojitoa kimasomaso kutetea wenye ualbino- Guterres

Haki za binadamu

Leo ni siku ya kimataifa ya kuelimisha jamii kuhusu watu wenye ualbino ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea mshikamano wake na watu wenye ualbino.

Katika ujumbe wake kwa siku hii Guterres amesema kauli mbiu ya mwaka huu, uthabiti licha ya mazingira magumu “‘ni kielelezo cha uthubutu, ustahimilivu na hatua za watu wenye ualbino katika mazingira ya habari potofu, unyanyapaa na ukatili.”

Tweet URL

Katibu Mkuu ameongeza kuwa licha ya vikwazo hivyo vya ustawi na usalama wao, viongozi wa mashirika ya kuwakilisha watu wenye ualbino huendelea kufanya kazi kwa bidii na kuunga mkono walio hatarini.

“Natoa wito kwa nchi na jamii kulinda na kuhakikisha haki za binadamu kwa watu wote wenye ualbino na kuhakikisha msaada na ulinzi,” amesema Guterres akiongeza kuwa anatiwa moyo kwamba watu wenye ualbino wanaendelea kuchukua nafasi katika maeneo ya kufanya maamuzi kote ulimwenguni na kufikia dhamira muhimu kwa mfano mpango wa hatua kuhusu ualbino Afrika.

Amekaribisha kazi inayotekelezwa na Ikponoswa Ero, mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wenye ualbino,kazi ambayo ni ya kuendeleza haki za kundi hilo.

Hata hivyo amesema bado kuna kazi kubwa ya kufanya, “kuna umuhimu mkubwa wa kuondoa fikra potofu kuhusu hali ya ualbino na kutokomeza kabisa ubaguzi dhidi ya kundi hili.”

Katibu Mkuu ametumia ujumbe wake kusihi nchi zote na jamii ulimwenguni kulinda na kutetea haki za watu wenye ualbino na kuwapatia huduma na msaada unaotakiwa.

Hali halisi

Ingawa idadi inatofautiana, Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa katika Amerika ya Kaskazini na Ulaya, mtu mmoja kati ya kila watu 17,000 hadi 20,000 wana ualbino lakini katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la sahaba, idadi ni kubwa zaidi.

Mtu mmoja kati ya 1,400 nchini Tanzania ana ualbino na huko Zimbabwe ni mtu mmoja kati ya 1,000.

Kutokana na hali ya kutokueleweka kwa baadhi ya watu kwenye jamii, watu wenye uabino wanakumbwa san ana ubaguzi duniani kote.

Mara nyingi imani za kishirikina zinafanya waenguliwe kwenye masuala ya kijamii na hata kukabiliwa na vipigo na kuuawa kwa sababu ya viungo vyao.

Katika ujumbe wake kwa siku ya leo, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amekazia wito kwa Guterres akitaka walindwe.

“Kadri janga la COVID-19 linavyoongeza changamoto zinazokabili watu wenye ualbino, katika baadhi ya nchi wanapatiwa jina “Corona” na “COVID-19” na wengine wamepigwa marufuku katika shughuli za kijamii,” amesema Bi. Bachelet.