Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UN aomba msaada zaidi kwa visiwa vidogo vinavyopambana na mabadiliko ya tabianchi

Katribu Mkuu  António Guterres  akiwa na waziri mkuu Ralph E. Gonsalves wa Saint Vicent na Grenada wakiangalia mradi wa kukabiliana na kupanda kwa kina cha maji
UN Photo/Lucanus Ollivierre
Katribu Mkuu António Guterres akiwa na waziri mkuu Ralph E. Gonsalves wa Saint Vicent na Grenada wakiangalia mradi wa kukabiliana na kupanda kwa kina cha maji

Mkuu wa UN aomba msaada zaidi kwa visiwa vidogo vinavyopambana na mabadiliko ya tabianchi

Tabianchi na mazingira

Ufadhili zaidi unahitajika kusaidia nchi zinazoendelea za visiwa vidogo SIDS, vilivyo katika mstari wa mbele wa mabadiliko ya tabianchi, amesema Jumamosi  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akiwa katika visiwa vya Saint Vincent na Grenada.

Bwana Guterres alitembelea mradi ambao unalisaidia taifa hilo la Caribea kukabiliana na athari za mmomonyoko wa ardhi wa pwani na kuongezeka kwa kina cha baharí ikiwa ni miongoni mwa athari za ongezeko la joto duniani.

Pia amepongeza mpango unaondeshwa nchini huo unaojulikana kama Ulinzi wa Bahari ya Georgetown, na kusistiza haja ya mshikamano zaidi na msaada wa kifedha.

Haki ya mabadiliko ya tabianchi

Guterres amesema ni "Lazima tupate uungwaji mkono wa nguvu kutoka kwa jumuiya ya kimataifa kwa kile tunachoita haki ya mabadiliko ya tabianchi ambayo ina maana ya ufadhili wa kutosha kwa gharama ya chini, iliyotathiminiwa haraka, ili kuruhusu kazi hizi zote ambazo tumekuwa tukiona kulinda kisiwa hiki dhidi ya bahari, na. dhidi ya mafuriko na dhoruba.”

Akijibu swali la mwandishi wa habari, Katibu Mkuu amesema kuwa SIDS lazima iwe na upatikanaji wa haraka na rahisi wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia Mfuko wa Hasara na Uharibifu.

Juhudi za kukabiliana na mmomonyoko wa udongo na kupanda kwa kina cha bahari zinaendelea St. Vincent and the Grenada sand Bay
UN Photo/Lucanus Ollivierre
Juhudi za kukabiliana na mmomonyoko wa udongo na kupanda kwa kina cha bahari zinaendelea St. Vincent and the Grenada sand Bay

Ameongeza kuwa utaratibu uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu wa kuzisaidia nchi zilizo hatarini kukabiliana na uharibifu unaotokana na ukame, mafuriko na hali mbaya ya hewa iliyosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, hatimaye ulianza kufanya kazi mwaka jana katika mkutano wa mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa COP28 huko Dubai.

Bwana Guterres ameeleza kuwa chini ya hazina hiyo, miradi midogo kama aliyoitembelea haitahitaji kiwango sawa cha urasimu kama ile inayogharimu mabilioni.

Badala yake ametoa wito wa "maamuzi ya haraka na uendeshaji wa haraka wa pesa zilizopo na ufadhili mwingi zaidi." 

Guterres ameongeza kuwa "Watu wa nchi zinazoendelea za Visiwa vidogo wako kwenye mstari wa mbele wa mabadiliko ya tabianchi. Hawakuchangia ongezeko la joto duniani, lakini wanalipa gharama kubwa ya ongezeko hilo," 

Nyumba zilizojengwa kwenye makazi ya Orange Hill Kaskazini Mashariki kwa ajili ya watu waliopoteza nyumba zao kutokana na Volkano
UN Photo/Lucanus Ollivierre
Nyumba zilizojengwa kwenye makazi ya Orange Hill Kaskazini Mashariki kwa ajili ya watu waliopoteza nyumba zao kutokana na Volkano

Kuibuka kutoka kwenye majivu

Katibu Mkuu pia amezuru maeneo ya Saint Vincent na Grenada ambayo yaliathiriwa na mlipuko wa Aprili 2021 wa volcano ya La Soufrière.

Watu wapatao 20,000, takriban moja ya tano ya idadi ya watu wote, walilazimika kuhama mara moja. 

Nyumba mpya zilijengwa katika eneo la makazi kwa wale ambao nyumba zao ziliharibiwa.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amekuwa nchini humo kuhudhuria mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Mataifa ya Amerika Kusini na Caribea (CELAC), uliofanyika Ijumaa.

Aliwasili katika mji mkuu, Kingstown, Alhamisi, ambapo, wakati wa mkutano na waandishi wa habari, aliwapongeza kwa ujasiri, mnepo na mshikamano wa watu baada ya janga la volkano.