Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Suriname inatoa “tumaini na msukumo kwa ulimwengu kuokoa misitu yetu ya mvua”: Mkuu wa UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (katikati) akutana na wanachama wa vyama vya ushirika vya kilimo vinavyoongozwa na wanawake na wanaume wazawa katika Kijiji cha Pierre Kondre-Redi Doti, katika ukanda wa msitu wa kitropiki wa Suriname.
UN Photo/Evan Schneider
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (katikati) akutana na wanachama wa vyama vya ushirika vya kilimo vinavyoongozwa na wanawake na wanaume wazawa katika Kijiji cha Pierre Kondre-Redi Doti, katika ukanda wa msitu wa kitropiki wa Suriname.

Suriname inatoa “tumaini na msukumo kwa ulimwengu kuokoa misitu yetu ya mvua”: Mkuu wa UN

Tabianchi na mazingira

Suriname inaweza kuwa nchi ndogo na isiyo na watu wengi zaidi katika ukanda wa  Amerika ya Kusini, lakini ni moja ya nchi za kijani kibichi. Inachukuliwa kuwa kinara wa kimataifa katika uhifadhi wa bioanuwai, huku zaidi ya asilimia 90 ya ardhi yake ikifunikwa na misitu ya asili, rasilimali asilia isiyo na kifani ya taifa zaidi ya kufidia saizi yake.

Msitu mzuri wa mvua wa Suriname, mnene, unaouruhusu kuwa na alama ya karibu kutokuwa na hewa ya kaboni, unaweza kuonekana kwa urahisi kutoka mahali popote, hata kutoka viunga vya mji mkuu, Paramaribo, ambao wenyewe umejaa masoko na vituo vya kitamaduni.

Siku ya Jumamosi (Kuni 02,2022), Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres alishuhudia moja kwa moja kujitolea kwa watu wa Suriname kulinda hazina zao za asili na maarifa ya mababu zao.

“Misitu ya mvua ni zawadi ya thamani kwa wanadamu. Ndiyo maana kutoka hapa Suriname, nataka kutuma ujumbe kwa ulimwengu: Ni lazima tuheshimu na kuhifadhi zawadi ya misitu ya mvua kwa sababu hii si zawadi ambayo itaendelea kutoa”, Guterres aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari na Rais Chan Santokhiat wa nchi hiyo mwisho wa siku yake ya kwanza ya ziara yake nchini humo.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia alitoa onyo kali: “Ikiwa tutaendelea kuona ukubwa [wa sasa] wa uharibifu katika misitu ya mvua duniani, hatuumi tu mkono unaotulisha bali tunaipasua”.
Bwana Guterres alisisitiza kuwa uharibifu mkubwa wa misitu na athari mbaya za hali ya hewa zinaongeza uchomaji moto misitu na ukame.

“Hii ni hali ya kuchukiza na ya aibu. Ni kujiua duniani kwa mwendo wa polepole,” alisema, akiongeza kuwa uharibifu huo unapaswa kuwa kengele ya kimataifa kuokoa mapafu ya sayari yetu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (katikati) akutana na wanachama wa vyama vya ushirika vya kilimo vinavyoongozwa na wanawake na wanaume wazawa katika Kijiji cha Pierre Kondre-Redi Doti, katika ukanda wa msitu wa kitropiki wa Suriname.
UN News/Laura Quinones
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (katikati) akutana na wanachama wa vyama vya ushirika vya kilimo vinavyoongozwa na wanawake na wanaume wazawa katika Kijiji cha Pierre Kondre-Redi Doti, katika ukanda wa msitu wa kitropiki wa Suriname.

Wito kutoka kwa watu wa asili wa Suriname

Mapema siku hiyo, Katibu Mkuu alitembelea kijiji cha wenyeji cha Pierre Kondre - Redi Doti, kilichoko kilomita 67 kusini mwa mji mkuu, kilichozungukwa na hekta 9,000 za msitu, na nyumbani kwa wakazi wapatao 100.

Baada ya kuendesha gari katika maeneo ya mashambani yenye aina ya ardhi yenye madini ya chuma, yenye sifa ya udongo mwekundu, Guterres alipokelewa na Kapteni Lloyd Read wa watu wa Kaliña, pamoja na wanawake na wanaume wanajamii wakiimba na kuvaa nguo zao za kitamaduni zenye rangi nyekundu inayotawala.

“Changamoto [tunayo kabiliana nayo] ya kulinda Mama Duniani na msitu wa Amazon haithaminiwi na inaleta vitisho kwa maisha yetu,” Lloyd Read alilalamika, akiongeza kuwa watu wake  bila kosa lao kwa sasa wako hatarini kutokana na unyonyaji wa maliasili na matokeo ya mabadiliko ya tabianchi kama vile mvua kubwa na endelevu na mafuriko.

Alisema kuwa uchafuzi wa zebaki hasa ukisababishwa na shughuli za uchimbaji haramu pia unatishia maisha na maisha ya wazawa.

“Kusini, maisha yameharibiwa na Zebaki. Hakuna samaki, hakuna nyama na hakuna maji safi ya kunywa. Hata viwango vya juu sana vya chuma hiki vimepatikana kwenye nywele za wenyeji wetu,” alisema.

Katibu Mkuu akizungumzia kero hizo wanazokabilian nazo na kumuuliza Bw. Lloyd maelezo zaidi, aliahidi kuwa ‘msemaji’ wa jumuiya hiyo wakati wa mkutano wake na Serikali baadaye.

“Hii ni ziara ya mshikamano na jamii za asili nchini Suriname na kote ulimwenguni. Tunaposhuhudia kuwa bado tunapoteza katika vita ya mabadiliko ya tabianchi, unapoona bayoanuwai inazidi kutishiwa kila mahali, unapoona uchafuzi wa mazingira duniani kote ni muhimu sana kutambua kwamba jamii za kiasili zinaonesha hekima, ustahimilivu na utashi. kuwa katika amani na asili”, aliwaambia wale waliokusanyika kijijini hapo.

Tweet URL

Mananasi kwa maendeleo endelevu

Kijiji cha Redi Doti, ambacho kimejikita ndani ya ukanda wa savanna wa Suriname, eneo la mchanga mweupe wenye mchanganyiko wa madini ya silicate ambao kwa kiasi kikubwa hauna rutuba, hufaulu kulima mananasi, matunda ya pasheni na mihogo, ambayo ndio chanzo kikuu cha kiuchumi cha maisha ya jamii.

Guterres alijionea kazi za vyama viwili vya ushirika ambavyo vinaungwa mkono na Umoja wa Mataifa na mashirika yake, likiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), pamoja na Umoja wa Ulaya.

Ushirika mmoja kama huo, unaoongozwa na wanawake wenyeji, huunda bidhaa za kikaboni zinazotokana na mananasi, kama vile jamu, juisi na vikombe vya matunda. Vyama vingine vya ushirika vinahusika na mchakato wa kilimo, ambao unajaribu kugeuza mavuno ya mananasi kuwa uzalishaji wa mwaka mzima, badala ya msimu.

Kulingana na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP), ujumuishaji wa jamii za kiasili na makabila katika ustawi wa kiuchumi ni muhimu. Ingawa wanajumuisha 4% tu ya watu wote, haki zao za ardhi zinachukua zaidi ya 80% ya eneo la Suriname, lakini hazitambuliki rasmi na sheria za kitaifa.

Kabla ya kuondoka katika jumuiya hiyo, Kapteni Lloyd Read alimwambia Katibu Mkuu kwamba atamwomba Tamushi Mwenyezi [Mungu mkuu wa roho], ampe nguvu na uwezo wa kwenda mbali zaidi, katika ulimwengu unaotishiwa na mabadiliko ya tabianchi na vita.

Akiimba sala nzuri katika lugha yake ya asili ya Kaliña, aliaga na kumwambia kwamba anatumaini angewakumbuka.

“Watu wa kiasili hawajachangia mabadiliko ya tabianchi, hata hivyo ni miongoni mwa walioathirika zaidi. Wakati huo huo, wana masuluhisho ambayo ulimwengu unaweza kujifunza mengi kutoka kwao. Wao ni walezi wanaojivunia baadhi ya viumbe hai vya lazima katika sayari hii, na wanahitaji kuungwa mkono kufanya hivyo,” mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisisitiza baadaye katika mkutano na waandishi wa habari.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na Waziri wa Mambo ya Nje wa Suriname, Albert Ramchand Ramdin, wakipanda mti mchanga wa mikoko katika eneo la ukarabati wa mikoko la Weg Naar Zee nchini Suriname.
UN Photo/Evan Schneider
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na Waziri wa Mambo ya Nje wa Suriname, Albert Ramchand Ramdin, wakipanda mti mchanga wa mikoko katika eneo la ukarabati wa mikoko la Weg Naar Zee nchini Suriname.

Kupanda matumaini na mikoko

Kutoka msituni, Katibu Mkuu alielekea ufukweni, ambako aliweza kuona athari mbaya za mabadiliko ya hali ya tabianchi yanayochochea mmomonyoko wa pwani, mafuriko na kupanda kwa kina cha bahari.

Weg Naar Zee, eneo la pwani linalofikika kwa urahisi la ekari zipatazo 10,000 lililo kaskazini-magharibi mwa Paramaribo na sehemu ya kilomita 386 za ukanda wa pwani wenye matope wa Suriname, umekumbwa na mmomonyoko wa udongo ambao umesababisha kukosekana kwa tope laini, makazi yanayopendwa zaidi na ndege wa pwani.

Tangu mwaka 2016, Umoja wa Mataifa unaunga mkono juhudi za nchi, zikiongozwa na wasomi na wanafunzi, kuongeza uhifadhi, urejesho wa asili na ukarabati wa mikoko. Mradi mmoja kama huo, unaoongozwa na Chuo Kikuu cha Anton de Kom cha Suriname, ambacho huweka miundo ya kunasa ardhi inayoporomoka kando ya pwani na mimea ili kurejesha uharibifu.

Akitembea kando ya ufuo wa matope pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Suriname, Albert Ramchand Ramdin, Katibu Mkuu Guterres alipanda mti mchanga wa mikoko.

“Suluhu za asili kama vile kuhifadhi mikoko, misitu ya mvua na mifumo mingine ya ikolojia ni muhimu. Dunia inahitaji mipango zaidi kama hii,” aliambia wanahabari.

Awali Katibu Mkuu huyo alisema mikoko ina maana ya pekee kwake, kwa sababu kitabu cha kwanza alichosoma akiwa mtoto kilikuwa kinahusu miti hiyo migumu na yenye manufaa ya kipekee.

Mikoko ina sehemu muhimu katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, kwani inaweza kunasa na kuhifadhi kiasi kikubwa cha kaboni kwenye mizizi na hata kwenye udongo inamokua.
Pia ni muhimu sana kwa mazingira yetu ya pwani na makazi na hifadhi za kitalu kwa safu tofauti za viumbe hai. Wanaitwa 'figo za pwani' kwa sababu ya jukumu wanalofanya katika kuzungusha virutubishi ndani ya mazingira ya pwani.

Katibu Mkuu akizungumza na waandishi wa habari katika ziara yake nchini Suriname
UN News
Katibu Mkuu akizungumza na waandishi wa habari katika ziara yake nchini Suriname

Mfano wa kipekee

“Nilichoona hapa Suriname kinanipa matumaini na msukumo. Lakini tunachokiona kote ulimwenguni ni sababu ya mshtuko mkubwa na hasira, “ Guterres alisema zaidi mwishoni mwa siku yake ya kwanza katika mkutano na waandishi wa habari.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisisitiza kuwa kwa bahati mbaya, Suriname inajitokeza katika upekee kwenye ulimwengu ambao unaelekea katika mwelekeo mbaya.

"Duniani kote, tunaona kushindwa kwa uongozi wa mabadiliko ya tabianchi na kuenea kwa uharibifu mbaya wa hali ya hewa ... Ili kufikia lengo la kupunguza ongezeko la joto kwa nyuzi 1.5, uzalishaji wa hewa duniani lazima upungue kwa asilimia 45 ifikapo mwaka 2030. Hata hivyo ahadi za sasa za tabianchi zingeweza kusababisha ongezeko la hewa chafu kwa asilimia 14 ifikapo 2030,” alionya.
Akisisitiza kwamba wazalishaji wakubwa wa hewa chafu wana jukumu maalum, Guterres alisisitiza kwamba mataifa ya Karibea yako mstari wa mbele wa mgogoro wa tabianchi na yameonesha uongozi thabiti mara kwa mara.

“Kama nilivyoona leo, tuna zana na ujuzi. Ulimwengu wetu unahitaji utashi wa kisiasa na mshikamano kuleta mabadiliko yanayohitajika. Suriname na eneo la Karibia zinaongoza njia mbele. Lazima tufuate mwongozo huo kwa watu, kwa vizazi na kwa sayari yetu ", alihitimisha.

Katibu Mkuu atakuwa Suriname hadi Jumapili, atakapohudhuria ufunguzi wa Mkutano wa 43 wa Kawaida wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Karibiani (CARICOM).