Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Volkano yaendelea kulipuka huko St. Vincent, UN iko mashinani kutoa usaidizi

Volkano katika mlima La Soufriere ilianza kulipuka tarehe 14 mwezi Aprili katika kisiwa cha St Vincent
WFP/Amy Chong
Volkano katika mlima La Soufriere ilianza kulipuka tarehe 14 mwezi Aprili katika kisiwa cha St Vincent

Volkano yaendelea kulipuka huko St. Vincent, UN iko mashinani kutoa usaidizi

Tabianchi na mazingira

Volkano imeendelea kulipuka katika kisiwa cha Saint Vincent kilichoko kwenye taifa la Saint Vincent na Grenadines huko Karibea na hadi sasa zaidi ya watu 4,000 wanaishi katika makazi ya muda yaliyoandaliwa na serikali.
 

Kwa mujibu wa taarifa ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu, OCHA, hata jana Jumatano volkano katika mlima La Soufriere iliendelea kulipuka wakati ambao eneo kubwa la kisiwa hicho kimefunikwa na majivu.
Tayari kuna vituo 89 vinavyohifadhi zaidi ya watu 4,021 huku usajili ukiendelea wa watu waliosaka hifadhi kwenye vituo hivyo ambapo hadi sasa 2,045 wamesajliwa.

Vituo 8 vya kufuatilia mitetemo ya volkano hivyo vimefunikwa ambapo Umoja wa Mataifa unasema vituo vingine 4 vitafungwa pindi itakapokuwa salama kufanya hivyo ili kufuatilia mwenendo wa mlipuko wa volkano hiyo kaskazini mwa St. Vincent.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa nayo yanaendelea na shughuli zao kutekeleza wajibu wao likiwemo la kuhudumia watoto, UNICEF, chakula na kilimo, FAO, mazingira, UNEP, afya, WHO na mpango wa chakula duniani, WFP.
Katika siku tano zilizopita, watu 127 wameokolewa kutoka eneo la Owia ambako ndio hatari zaidi, watu hao walikuwa wanaendelea kuwepo eneo hilo licha ya agizo la wiki iliyopita la kuwataka waondoke.