Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ni 'ya kushtua, isiyo endelevu na ya kukatisha tamaa' kote Gaza

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likikutana kujadili hali ya Mashariki ya Kati likiwemo suala la Wapalestina.
UN Photo/Loey Felipe
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likikutana kujadili hali ya Mashariki ya Kati likiwemo suala la Wapalestina.

Hali ni 'ya kushtua, isiyo endelevu na ya kukatisha tamaa' kote Gaza

Amani na Usalama

Baraza la Usalama limekutana leo Alhamisi Februari 22 kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani kuhusu hali ya Ukanda wa Gaza, iliyokumbwa na miezi kadhaa ya vita isiyoisha na mivutano iliyoenea katika eneo hilo la Mashariki ya Kati, bila suluhu.

Tor Wennesland, Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Mchakato wa Amani ya Mashariki ya Kati, amewaambia mabalozi kwamba "bado hakuna mwisho huko mbele" wakati vita inakaribia siku 140.

"Hakuna mwisho wa kiwewe cha wale walioathiriwa na maovu yaliyotokea tarehe 7 Oktoba. Hakuna mwisho wa mateso na watu kukata tamaa katika Gaza. Hakuna mwisho wa machafuko ya kikanda." Amesema Bwana Wennesland aliyezuru Gaza wiki hii na kuelezea hali ya kibinadamu huko kuwa ya kushtua, na ya kukatisha tamaa.

Mazungumzo, sio vurugu

Akionya kwamba kiwango cha hali ya dharura kinaweza kusambaa haraka, Bwana Wennesland ametoa wito kwa jibu la pamoja, lililoratibiwa na la kina sio tu kushughulikia mzozo wa haraka katika Ukanda huo lakini kusaidia kurejesha upeo wa kisiasa kwa Wapalestina na Waisraeli.

"Ili kufanya hili, tunahitaji haraka mpango wa kufikia usitishaji mapigano wa kibinadamu na kuachiliwa kwa mateka," amesisitiza, akiongeza pia haja ya kuunda nafasi ya mazungumzo juu ya ghasia.

"Hatimaye, suluhisho pekee la muda mrefu kwa Gaza ni la kisiasa," amesema Wennesland.

"Pamoja na kutilia maanani wasiwasi halali wa usalama wa Israel, lazima kuwe na njia wazi kuelekea kurejesha utawala bora wa Palestina katika eneo la OPT (eneo linalokaliwa la Palestina), ikiwa ni pamoja na Gaza." ameongeza.

Suluhu ya Serikali Mbili

Kando na hayo, uungwaji mkono wa kimataifa wa kuimarisha na kurekebisha Mamlaka ya Palestina ili kuboresha uhalali wa ndani na kimataifa utakuwa muhimu.

Ili kuunda mazingira haya, Wennesland ametoa wito wa kuwepo kwa mfumo wa kisiasa wa muda ili kukomesha uvamizi huo na kujadiliana suluhu ya Serikali mbili.

"Juhudi hizi lazima ziunganishwe na kuharakisha ikiwa tunataka kuibuka kutoka kwa jinamizi hili na kuingia katika njia ambayo inaweza kuwapa Wapalestina na Waisraeli fursa ya amani ya kudumu," alihitimisha.

Kura ya turufu inagharimu maisha, inaonya MSF

Pia aliyetoa maelezo kwa Baraza  niChristopher Lockyear, Katibu Mkuu wa Médecins Sans Frontières (MSF), au Madaktari Wasio na Mipaka.

Akihofia mashambulizi mengine mabaya zaidi ya Israel, amesema "amechukizwa" na Marekani kutumia mara kwa mara mamlaka yake ya kura ya turufu kuzuia juhudi za kupitisha maazimio yaliyo dhahiri zaidi: moja la kutaka kusitishwa kwa mapigano mara moja.

"Tunaishi kwa hofu ya uvamizi wa ardhini" huko Rafah, amesema.

Akiliita rasimu mpya ya azimio la Washington "linalopotosha", amesema Baraza linapaswa kukataa azimio lolote "ambalo linatatiza zaidi juhudi za kibinadamu ardhini na kusababisha Baraza hili kuidhinisha kimyakimya kuendelea kwa ghasia na ukatili mkubwa huko Gaza".