Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Taharuki yaongezeka Gaza huku msafara wa UN ukizuiliwa nje ya hospitali iliyoshambuliwa

Timu ya Umoja wa Mataifa inajaribu kupeleka mafuta katika hospitali ya Nasser kupitia barabara zilizoharibiwa katikati ya Februari 2024.
© UNOCHA/Themba Linden
Timu ya Umoja wa Mataifa inajaribu kupeleka mafuta katika hospitali ya Nasser kupitia barabara zilizoharibiwa katikati ya Februari 2024.

Taharuki yaongezeka Gaza huku msafara wa UN ukizuiliwa nje ya hospitali iliyoshambuliwa

Amani na Usalama

Mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa yanayofanya kazi Ukanda wa Gaza uliokumbwa na vita yameonyesha kusikitishwa sana leo kutokana na kuendelea kwa vizuizi vya upatikanaji wa misaada ya kibinadamu vilivyowekewa na jeshi la Israel, baada ya magari ya kubebea wagonjwa yaliyokuwa yamewabeba wagonjwa kutoka hospitali iliyoshambuliwa mwishoni mwa juma kusimamishwa kwa saa kadhaa huku wahudumu wa afya wakisakwa na kuswekwa kizuizini.

Hayo yamesemwa na timu ya Umoja wa Mataifa ya Kibinadamu huko Palestina, baada ya operesheni ya kuwahamisha wagonjwa 24 kutoka Hospitali ya Al Amal huko Khan Younis. 

Imeongeza kuwa “Hili si tukio la pekee. Misafara ya misaada imeshutumiwa na inanyimwa kimfumo fursa ya kuwafikia watu wenye uhitaji.” 

Hayo yanajiri huku kukiwa na mapigano makali yanayoendelea katika eneo hilo, yaliyochochewa na mashambulizi ya kigaidi yanayoongozwa na Hamas nchini Israel tarehe 7 Oktoba mwaka jana ambapo takriban watu 1,200 waliuawa kinyama na zaidi ya 250 kuchukuliwa mateka.

Wakati kukiwa na wito wa mara kwa mara wa kimataifa wa kusitisha mapigano, mazungumzo yameendelea kati ya mamlaka ya Israel na wawakilishi wa Hamas kwa ajili ya kuachiliwa huru kwa mateka na wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa nchini Israel. 

Hadi sasa, karibu raia 30,000 wa Gaza wameuawa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kulingana na mamlaka ya afya ya Gaza.

Hakuna la kufanya

Wagonjwa kadhaa "kama sio wote walihitaji aina fulani ya huduma wa upasuaji ambayo bila shaka haikuweza kutokea katika Hospitali ya Al Amal", amesema Jens Laerke, ambaye ni msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA.

Wagonjwa wengine 31 ambao hawako mahututi ilibidi waachwe nyuma.

Akizungumza mjini Geneva, Bwana Laerke amethibitisha kwamba operesheni ya kuwahamisha watu ulikuwa imefahamishwa kwa mamlaka ya Israeli ambao walikuwa wamekubali kama sehemu ya itifaki za kawaida za upunguzaji wa migogoro.

Bwana Laerke amesema “Lakini, jeshi la Israel lilikuwa halijatoa taarifa yoyote au mawasiliano yoyote kuhusu kwa nini magari ya kubeba wagonjwa yalizuiliwa kwa takriban saa saba au kwa nini wahudumu wa afya walitolewa nje, wakilazimishwa kuvua nguo, na wawili bado hawajaachiliwa.”

Hali ni tete

Maendeleo hayo yalihusisha msafara unaoongozwa na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO siku ya Jumapili kuelekea Hospitali ya Al Amal. 

Mara baada ya hapo, mshirika wa Umoja wa Mataifa wa shirika la Hilali Nyekundu la Palestina PCRS, waliwahamisha wagonjwa 24, akiwemo mwanamke mjamzito, mama na mtoto mchanga.

Hospitali hiyo ambayo ni kituo kinachosimamiwa na PCRS imekuwa kitovu cha operesheni za kijeshi katika mji wa kusini mwa Gaza kwa zaidi ya mwezi mmoja, kukiwa na mashambulio 40 kati ya Januari 22 na 22 Februari ambayo yalisababisha vifo vya takriban watu 25 na wafanyikazi wa afya pia kuogopa kuondoka katika kitengo cha matibabu kwa wiki kadhaa, timu ya nchi ya Umoja wa Mataifa imesema katika tarifa hiyo.

Sehemu ya uharibifu ulioathiri Hospitali ya Al-Amal huko Khan Younis.
UN News
Sehemu ya uharibifu ulioathiri Hospitali ya Al-Amal huko Khan Younis.

Nia ya kufanya kazi

Leo huko Gaza, ni hospitali 12 tu kati ya 36 "zinazofanya kazi kwa kiasi", amesema msemaji wa WHO Christian Lindmeier akiwaambia waandishi wa habari huko Geneva na kuongeza kuwa hospitali hizo sita ziko kusini na sita kaskazini lakini hospitali 23 hazifanyi kazi hata kidogo".

Timu 15 za ziada za matibabu ya dharura pia zimetumwa kusini mwa Gaza na hospitali nne zamuda zilizoanzishwa ambazo kwa jumla zina vitanda 305, Bw. Ameendelea kusema bwana Lindmeier. 

Ameongeza kuwa "Huu ni msaada muhimu, lakini bila shaka itakuwa muhimu zaidi kurejesha mfumo wa afya wa Gaza na kuwapata furs wahudumu wote wa afya ambao wapo na wamepata mafunzo na wako tayari, chini ya hali hizi kufanya kazi katika nafasi walizo na uwezo wa kufanya kazi."

Kufanya kila liwezekanalo

WHO imeripoti kwamba siku ya Jumamosi, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kutoa misaada kwa hospitali ya Al Amal ulifanikiwa kuwasilisha vifaa vya matibabu vilivyohitajika sana, dawa na antibiotics, pamoja na baadhi ya chakula, maji na mafuta kwa ajili ya jenereta.

"Wahudumu wa afya walithibitisha kwamba waliweza kutoka nje ya majengo ya hospitali Jumamosi baada ya mwezi mmoja kuwa ndani sababu walihofia maisha yao, kwani kulikuwa na mapigano karibu na eneo hilo na hospitali ilikuwa imeshambuliwa mara nyingi."

Kabla ya vita, hospitali ilikuwa na vitanda 100 na ililenga afya ya mama na mtoto na uwezo wa kushughulikia mahitaji ya msingi ya upasuaji na dawa, pamoja na huduma maalum za ukarabati. 

Lakini, uharibifu uliosababishwa na ulipuaji wa ghorofa ya tatu ya hospitali hiyo ulipunguza uwezo wa vitanda takriban 60.

Mashirika sita ya Umoja wa Mataifa yalishiriki katika operesheni hiyo ambayo iliwasilisha vifaa vya kutosha kuwatibu wagonjwa 50 wenye kiwewe.

Mashirika hayo ni WHO, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya OCHA, shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Palestina UNRWA, Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya misaada ya kutegua mabomu yaliyotegwa ardhini UNMAS na Idara ya Umpoja wa Mataifa ya ulinzi na Usalama na Usalama UNDSS.