Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaonya kwamba raia Gaza wanaishi kwa taharuki na hofu ya mashambulizi ya Israel Rafah

Wapalestina waliofurushwa kwao wakiwa katika makazi ya muda katika mji wa Rafah Kusini mwa Ukanda wa Gaza.
© OHCHR/Media Clinic
Wapalestina waliofurushwa kwao wakiwa katika makazi ya muda katika mji wa Rafah Kusini mwa Ukanda wa Gaza.

UN yaonya kwamba raia Gaza wanaishi kwa taharuki na hofu ya mashambulizi ya Israel Rafah

Msaada wa Kibinadamu

Wakati juhudi za kimataifa zikiendelea kufikia usitishaji vita huko Gaza, mkuu wa  shirika la Umoja wa Mataifa la misaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, alionya leo kwamba wale walio katika eneo hilo bado wametiwa kiwewe na vita ya Israel na wanahofia kushambuliwa kwa kiasi kikubwa Rafah katika eneo hilo la kusini.

"Watu wana wasiwasi na wanahofia uwezekano wa operesheni kubwa ya kijeshi," amesema Philippe Lazzarini, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka katika mkutano na nchi wanachama mjini Geneva Uswis. 

Ameongeza kuwa "Ikiwa shambulio hilo litatokea, swali ni, Raia wataenda wapi? Hakuna mahali salama kabisa huko Rafah na hofu ni kwamba idadi ya watu waliouawa na kujeruhiwa inaweza kuongezeka tena kwa kiasi kikubwa."

Baada ya mapigano ya zaidi ya miezi minne, yaliyochochewa na mashambulizi ya mauaji yaliyoongozwa na Hamas tarehe 7 Oktoba mwaka jana nchini Israel na kusababisha takriban watu 1,200 kuuawa kwa kuchinjwa na zaidi ya 250 kuchukuliwa mateka, zaidi ya watu 100,000 wa Gaza wameripotiwa kuuawa, kujeruhiwa au kufukiwa chini ya vifusi kwa mujibu wa mamlaka ya afya ya eneo hilo, huku kukiwa na mashambulizi makali ya Israel yanayoendelea.

Wimbi kubwa la watu wanaotawanywa

Bwana Lazzarini amesisitiza kuwa haiwezekani kutarajia zaidi ya watu milioni moja waliokimbia makazi yao waliojazana katika mkoa wa Rafah kuhama kwa mara nyingine tena, ili vikosi vya Israel viendelee kuwasaka wanamgambo wa Hamas.

"Watu hao wanaombwa kuhama, swali ni wapi pa kuhamia," amesema, akibainisha kuwa huko Rafah, kila kipande cha ardhi katika eneo la kilomita 20 kinakaliwa na mamia ya maelfu ya watu wanaoishi katika makazi ya muda yaliyoezekwa kwa maplastiki.

Akigeukia suala la madai mazito kwamba baadhi ya wafanyakazi wa UNRWA walishirikiana na Hamas, mkuu wa shirika hilo amebainisha kuwa amewafuta kazi mara moja waliohusika na kuanzisha uchunguzi. 

Bwana Lazzarini pia ametoa wito wa ushirikiano wa mamlaka ya Israel.

Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini akihutubia wanahabari katika Ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva.
UN News/Anton Uspensky
Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini akihutubia wanahabari katika Ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva.

Kamishna huyo Mkuu wa UNRWA pia amebainisha kuwa mapitio ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa yataanza kesho kuhusu tuhuma dhidi ya shirika hilo kuhusu "matumizi yake ya mitandao ya kijamii, kuhusu njia, kuhusu misimamo ya kisiasa na jinsi limekuwa likikabiliana na mapigo hayo.”

Mchakato huo huenda ukachukua miezi miwili lakini unapaswa kuambatana na uchunguzi, ikiwa ni pamoja na madai ya jeshi la Israel kwamba handaki na kituo cha takwimu kilichoko mita 20 chini ya makao makuu ya UNRWA katika Mji wa Gaza kilitumiwa na Hamas, amesema Bwana Lazzarini.

Vituo vya UNRWA vyashambuliwa

Tweet URL

Kamishina wa UNRWA ameongeza kuwa "Tunahitaji kuangalia hali zote ambapo majengo ya Umoja wa Mataifa yamedharauliwa waziwazi. Tangu mwanzo wa vita zaidi ya mitambo yetu 150 imepigwa na makombora. Tunajua kwamba mitambo mingine imeharibiwa kabisa, mamia ya watu wameuawa, maelfu wamejeruhiwa na yote haya yanahitaji uchunguzi huru ikiwa ni pamoja na madai ya handaki.”

Hapo awali, Balozi wa kudumu wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa huko Geneva, Meirav Eilon Shahar, alibainisha kuwa serikali yake haitaki "madhara yoyote kwa raia wa Gaza na kwamba ina nia ya kushirikiana na uchunguzi wa UNRWA, ingawa inasalia kwenye vita na shirika la kigaidi la Hamas”.

"Vita vyetu ni dhidi ya Hamas, si ya watu wa Palestina," amesema Balozi huyo, ambaye pia amesisitiza kwamba "kuna njia mbadala za UNRWA"  madai ambayo yalikataliwa na Bwana Lazzarini ambaye amesema kuwa itakuwa "kutokuona mbali kufunga shirika hilo wakati wasaidizi wakuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu na mashirika yasiyo ya kiserikali wakitoa wito wa kuongezwa msaada zaidi hadi Gaza.”

Mustakbali uko hatari

Mkuu wa UNWRA amesema "Tuna wasichana na wavulana nusu milioni waliojeruhiwa vibaya na tunahitaji haraka kurejea katika mfumo wa elimu,". Hili halitatolewa na "tawala za mitaa zinazoibukia", amesisitiza, akiongeza kuwa "hakuna shirika lingine la Umoja wa Mataifa au NGO yenye uzoefu katika kutoa huduma kama za serikali, ikiwa ni pamoja na elimu kwa mamia ya maelfu ya watoto.”

Amehitimisha kwa kusema kwamba "Ikiwa tunataka kutoa nafasi kwa mabadiliko yoyote yajayo kufanikiwa, tunahitaji pia kuhakikisha kuwa jumuiya ya kimataifa ina zana, na mojawapo ya zana hizi ni UNRWA."