Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuhairishwa kwa uchaguzi wa Rais Senegal kunanitia hofu: Guterres

Dakar, mji mkuu wa Senegal
© Unsplash/Kurt Cotoaga
Dakar, mji mkuu wa Senegal

Kuhairishwa kwa uchaguzi wa Rais Senegal kunanitia hofu: Guterres

Amani na Usalama

Baada ya Rais wa Senegal Macky Sall kutangaza Februari 3 kuahirishwa kwa uchaguzi wa rais uliokuwa umepangwa kufanyika Februari 25 mwaka huu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kupitia msemaji wake kwamba anafuatilia kwa karibu matukio husika na ameonyesha wasiwasi wake kuhusu sula hilo.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, Sall alitangaza uamuzi wake wa kuahirisha uchaguzi huo katika hotuba ya kitaifa kupitia televisheni tarehe 3 mwezi huu, na akasema ametia saini amri ya kufuta mswada wa kuweka tarehe ya awali ya uchaguzi.

Mwezi uliopita, Baraza la Katiba la Senegal liliwanyima uhalali wanachama kadhaa wa upinzani kuwania nyadhifa zao kwa madai kwamba hawakukidhi vigezo vya wagombea. 

Sall alitaja hilo kama sababu ya kuahirisha uchaguzi huo, akisema hali hiyo inaweza kuzua mizozo kabla na baada ya uchaguzi na kuathiri pakubwa uaminifu wa kura.

Wito wa mazungumzo ili kuepusha vurugu

Hata hivyo, uamuzi wa Sall ulisababisha maandamano katika maeneo mengi, ikiwa ni pamoja na mji mkuu wa Dakar. 

Kulingana na ripoti, mnamo Februari 5, bunge la kitaifa la Senegal lilianguka katika machafuko. 

Baadhi ya wanachama wa upinzani walijaribu kuzuia mswada uliopitishwa kuahirisha uchaguzi, lakini wakakamatwa badala yake. 

Siku hiyo hiyo, polisi pia walitumia nguvu dhidi ya waandamanaji waliokusanyika nje ya Bunge kwa kuwavurumishia mabomu ya machozi.

Katika taarifa iliyotolewa tarehe 9 Februari, Katibu Mkuu Guterres amewataka wadau wa Senegal kushiriki katika mazungumzo na kudumisha mazingira ya kisiasa yenye amani huku wakiepuka matumizi ya ghasia ili kuhakikisha kuwa mkutano jumuishi unafanyika ndani ya mfumo wa katiba ya nchi hiyo, kuzingatia ujinsia na uwazi katika uchaguzi wa Rais.

Rais wa Senegal Macky Sall akizungumza wakati wa mjadala wa Baraza Kuu (Toka Maktaba)
UN Photo/Cia Pak
Rais wa Senegal Macky Sall akizungumza wakati wa mjadala wa Baraza Kuu (Toka Maktaba)

kuunga mkono uimarishaji wa demokrasia

Sall alichaguliwa kuwa Rais wa Senegal kwa mara ya kwanza mwaka 2012 na alifanikiwa kuchaguliwa tena mwaka 2019. 

Muhula wake wa pili utakamilika Aprili 2 mwaka huu. Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, Sall hataruhusiwa kugombea tena urais, na yeye mwenyewe amekuwa akisema mara kwa mara kwamba hatawania muhula wa tatu wa urais.

Hata hivyo, baadhi ya wanachama wa upinzani bado wanaamini kuwa Sall ameahirisha uchaguzi ili aendelee kubaki madarakani, pia kuna dhana kwamba hatua ya Sall inaonyesha kutomuunga mkono mgombea urais aliyependekezwa na muungano unaotawala "Common Hope Alliance" na waziri mkuu wa sasa Amadou Ba. Amadou Ba hajiamini.

Inaarifiwa kuwa hii ni mara ya kwanza kwa uchaguzi wa urais kuahirishwa nchini Senegal. 

Kwa mujibu wa mswada uliopitishwa na bunge la kitaifa la Senegal tarehe 5, tarehe mpya ya uchaguzi imepangwa kufanyika Desemba 15 mwaka huu.

Guterres amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa umejitolea kuendelea kuiunga mkono Senegal katika kuimarisha demokrasia na kukuza amani, utulivu na maendeleo.