Mwanamke akidhamiria, anaweza kufanya chochote- Meja Seynabou Diouf

5 Novemba 2019

Meja Seynabou Diouf kutoka jeshi la polisi la taifa la Senegal amechaguliwa na kutangazwa kutwaa tuzo ya polisi mwanamke wa Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2019. 

Meja Diof anasema mwanamke anapodhamiria jambo anaweza hata kuliko wengine na amemekabidhiwa tuzo yake hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani na kutoa wito kwa wasichana na wanawake wengine kwamba  “wanapaswa kuangalia mazingira yao na kutambua kwamba dunia hivi sasa imeundwa na usawa wa kijinsia, ambacho mwanaumme anaweza kufanya mwanamke atakifanya kwa ubora zaidi, lakini wakati wote tunapaswa kuwaelimisha  kwamba ni jinsi gani tunavyowahitaki kujiunga  lakini pia kuongeza na viongozi wa jamii kuwapa fursa, watuwezeshe kwa sababu huwezi kusajilia polisi wa kike kama wa kiume , tunamahitaji maalum na lazima yapewe uzito”

Hivi sasa Meja Diouf anaongoza kikosi kazi cha kusaidia kuzuia na kukomesha unyanyasaji na ukatili wa kingono kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC katika eneo la Goma mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.

Pia anaendesha mtandao wa wanawake polisi wa Umoja wa Mataifa ambao unawaunganisha maafisa wanawake kwa ajili ya uanagenzi, mafunzi kwa ajili ya kuendeleza taaluma zao na kusaidiana.

MejaSeynabou Diouf wa UNPOL kutoka Senegal, (katikati) akitembelea kituo cha watoto yatima huko Kibati nchini DRC
United Nations
MejaSeynabou Diouf wa UNPOL kutoka Senegal, (katikati) akitembelea kituo cha watoto yatima huko Kibati nchini DRC

Baada ya kutunukiwa tuzo hiyo Bi. Diouf amesema “ni heshma kubwa kupokea tuzo ya mwaka ya polisi mwanamke wa Umoja wa Mataifa, ni thamani kubwa kwangu. Kuzuia unyanyasaji na ukatili wa kingono ni kipaumbele kwangu, timu yangu na ofisi yangu. Na ninaamini kwamba juhudi zetu zinazaa matunda , kwa mfano mwaka huu hakuna madai yoyote yaliyowasilishwa dhidi ya polisi wa MONUSCO. Lakini siku zote tunaweza kuweka juhudi zaidi haka dai moja, ni dai kubwa. Tunahitaji kufanya kila tuwezalo kuhakikisha kwamba hakuna dai hata moja na waathirika wa ukatili huu wanapokea msaada wanaostahili.”

Meja Diouf alichaguliwa miongoni mwa majina 30 yaliyopendekezwa kutoka katika sehemu 8 za operesheni za Umoja wa Mataifa.

Uzoefu wake wa nyuma katika Umoja wa Mataifa ujnajumuisha kufanya kazi katika ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika wa kulinda amani jimboni Darfur, UNAMID na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA.

Ana uzoefu wa miaka 33 katika jeshi la polisi la taifa nchini Senegal.

Tuzo ya Umoja wa Mataifa ya polisi wa mwanamke wa mwaka ilianzishwa mwaka 2011 ili kutambua mchango mkubwa wa maafisa wa polisi wanawake katika operesheni za ulinzi wa amani na kuchagiza uwezeshaji wa wanawake.

Hivi sasa zaidi ya maafisa wa polisi wanawake 1400 wanahudumu katika operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa na Senegali ni mchangiaji mkubwa wa polisi miongoni mwa nchi tano zinazotoa maafisa wengi wa polisi wanawake.

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter