Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde wadau hakikisheni uchaguzi unakuwa huru na wa amani Chad: Guterres

Migogoro katika Sahel iliwalazimu watu wengi nchini Chad kukimbia makazi yao na kujihifadhi katika kambi za muda zinazoungwa mkono na Umoja wa Mataifa. (Maktaba)
UN Photo/Eskinder Debebe
Migogoro katika Sahel iliwalazimu watu wengi nchini Chad kukimbia makazi yao na kujihifadhi katika kambi za muda zinazoungwa mkono na Umoja wa Mataifa. (Maktaba)

Chonde chonde wadau hakikisheni uchaguzi unakuwa huru na wa amani Chad: Guterres

Amani na Usalama

Kuelekea uchaguzi wa duru ya kwanza wa Rais nchini Chad unaotarajiwa kufanyika Mei 6 mwaka huu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewasihi wadau wote katika uchaguzi huo kuhakikisha unafanyika kwa amani, uwe jumuishi, huru, wa haki na wa mchakato unaoaminika na duru ya pili ya uchaguzi huo, ikihitajika, itafanyika tarehe 22 Juni 2024.

Antonio Guterres kupitia taarifa yake iliyotolewa na msemaji wake hii leo mjini New York Marekani amewachagiza viongozi wote wa kisiasa  kujizuia na vitendo vyovyote ambavyo vitaathiri mchakato wa amani wa uchaguzi, na kuhakikisha wanatatua hali yoyote ya kutoafikiana katika mchakato huo kwa njia ya mazungumzo.

Katibu Mkuu pia amewasihi wagombea kushughulikia malalamiko yoyote yatakayojitokeza kupitia mfumo wa kisheria uliopo.

Uchaguzi huo wa Chad unafuatia kura ya maoni ya katiba iliyofanyika tarehe 17 Desemba 2023, kufuatia kifo cha Rais Idriss Déby mwaka wa 2021. 

Rais wa mpito aliye madarakani Mahamat Déby, mtoto wa hayati rais Idriss Déby, anagombea kwa muhula kamili kama mgombeaji wa Vuguvugu la ukombozi wa Wazalendo, na hivyo kuwa na uwezekano wa kuongezwa kwa utawala wa miaka 33 wa familia ya Déby.

Guterres amerejelea kusema kwamba Umoja wa Mataifa umejizatiti kuendelea kuisaidia chad katika juhudi zake za kujenga mustakbali wa amani na wenye ustawi kwa wote.