Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yalaani ghasia zinazoendelea Senegal, yataka utulivu

Bendera ya Senegal
UNOWAS
Bendera ya Senegal

UN yalaani ghasia zinazoendelea Senegal, yataka utulivu

Amani na Usalama

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya  Afrika Magharibi ,UNOWAS,  Mohamed Ibn Chambas, amelaani vitendo vya ghasia viliyofanyika kwenye maeneo tofauti tofauti nchini Senegal ambako mtu mmoja ameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa.

 

Taarifa ya UNOWAS iliyotolewa leo mjini Dakar, Senegal inasema ghasia hizo zimetokea siku mbili zilizopita.
Bwana Chambas ametoa wito kwa wahusika wa vitendo hivyo kujizuia huku akitaka mamlaka zichukue hatua za lazima kumaliza mvutano na kuhakikisha haki ya kikatiba ya kuandamana inazingatiwa.
Mwakilishi huyo ametoa wito pia kwa mamlaka za ulinzi kuhakikisha zinazingatia ueledi katika kazi zao ili waandamanaji watekeleze haki yao ya msingi ya kuandamana kwa usalama.

Kilichotokea ni nini?

Vyombo vya habari vinaripoti kwamba maandamano hayo yanafuatia tukio la kuswekwa ndani kwa kiongozi wa upinzani Ousmane Soko kwa tuhuma za ubakaji, tuhuma ambazo amedai zina ushawishi wa kisiasa.
Inaripotiwa kuwa huduma za mitandao ya kijamii zimedhibitiwa mapema Ijumaa nchini Senegal kabla ya kufanyika kwa maandamano yaliyopangwa na mashirika ya kiraia na vyama vya upinzani.

Sonko, alikuwa mshindi wa tatu kwenye uchaguzi wa rais mwaka 2019 na ana ushawishi mkubwa miongoni mwa viaja na anaweza kufunguliwa mashtaka kwa kuwa wiki iliyopita alivuliwa kinga yake ya kibunge.

Alikamatwa siku ya Jumatano kwa mashtaka ya kusababisha vurugu baada ya maandamnao ya kupinga tuhuma dhidi yake za ubakaji, akidai kuwa serikali inalenga kumkandamiza.