Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: Hawana matumaini, hawana nyumba – Katibu Mkuu UN

Katibu Mkuu António Guterres akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York.
UN Photo/Loey Felipe
Katibu Mkuu António Guterres akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York.

Gaza: Hawana matumaini, hawana nyumba – Katibu Mkuu UN

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameelezea wasiwasi wake mkubwa juu ya hali inayoendelea huko Gaza, Mashariki ya Kati na kusisitiza wito wake wa sitisho la mapigano haraka iwezekanavyo na kuachiliwa huru kwa mateka bila masharti yoyote.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Alhamisi jijini New York, Marekani, Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa “hatua halisia, dhahiri na za msingi,” kuelekea suluhu ya uwepo wa mataifa mawili kwa kuzingatia maazimio ya Umoja wa Mataifa, sheria ya kimataifa na makubaliano ya awali.

“Kurejea kwa chuki za mara kwa mara zinazosababisha umwagaji wad amu, na miongo ya mivutano na kukaliwa, kumekwamisha kufanikisha Taifa la Wapalestina, au usalama kwa Israeli,” amesema Katibu Mkuu.

“Eneo la Mashariki ya Kati na duniani kote, tunahitaji amani katika kila hali… dunia yetu haiwezi kusubiri,” amesema Guterres.

Amani ndio kinachojitaka

Akirejea hotuba yake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  jana, ambako aliwasilisha vipaumbele vyake kwa mwaka 2024, Katibu Mkuu amemulika mizozo, mivutano ya kijiografia na kuzidi kuimarika kwa mgawanyiko ndani ya jamii na kusisitiza kuwa amani ni saw ana ‘uzi’ “unaounganisha changamoto za aina mbalimbali zinazokumba dunia.”

“Jana niliwasilisha tathmini yangu ya dhahiri kabisa kuhusu dunia. Huu si wakati wa kuvutana,” amesema Katibu Mkuu.

Akiangazia changamoto za wazi zinazokumba dunia – kuanzia hatari ya nyuklia hadi dharura ya tabianchi na hatari inayoweza kutokea iwapo Akili Mnemba au AI haitadhibitiwa na kusema hatua zaidi zinahitajika katika maeneo yote.

“Inahitaji mazungumzo mazito kati ya nchi zilizoendelea na zisizoendelea; kati ya nchi tajiri na nchi zenye uchumi unaoibukia; kati ya nchi za kusini na kaskazini, mashariki na magharibi,” amesema Katibu Mkuu.

Marekebisho yanahitajika

Katibu Mkuu ametoa wito wa marekebisho ya taaisi, akianza na ‘kulifumua’ Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Taasisi za Bretton Woods ambazo ni Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani, (IMF).

Akitambua kubadilika kutoka mwenendo wa dunia wa kuhama kutoka mwelekeo wa upande mmoja hadi kuwa na dunia iliyogawanyika kimakundi makundi, Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa kuangalia upya mifumo jumuishi ya usimamizi kwenye ushirikiano wa kimataifa na hivyo kupunguza hatari mbali mbali.

Akiangazia siku za usoni, Katibu Mkuu amemulika mkutano ujao wa siku za zama zijazo utakaofanyika mwezi Septemba, huku akielezea umuhimu wa Ajenda Mpya ya Amani, Fungu la kuchochea SDG na Bodi ya ushauri kuhusu Akili Mnemba.

Amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha taasisi za saas zinatunza na kuzingatia kanuni kama vile kuheshimu Chata ya Umoja wa Mataifa, sheria ya kimataifa na sheria ya kimataifa ya kibinadamu.

Hali Gaza

Akizungumzia majanga ya sasa, Bwana Guterres ameelezea wasiwasi wake mkubwa juu ya mapigano yanayoendelea Ukraine na Gaza, ambako amesema “hali hii inazidi kubwa mbaya,” na operesheni za kiutu zinaendelea kukumbwa na vizuizi vya kufikisha misaada, hatari za kukabiliana na mapigano.

“Hebu tuwe wazi: kuzuia ufikishaji wa misaada ya kiutu kunamaanisha kuwanyima misaada ya kiutu raia,” amesisitiza.

Katibu Mkuu pia ameelezea wasiwasi wake juu ya ripoti ya kwamba Israel ina mpango wa kuelekeza operesheni zake Rafah.

“Nusu ya idadi ya wakazi wa Gaza, sasa wamejilundika Rafah. Hawana pa kwenda. Hawana nyumba na hawana matumaini,” amesema Katibu Mkuu huku akisisitiza umuhimu wa sitisho la mapigano kwa minajili ya kiutu, mateka waachiliwe huru bila masharti nah atua thabiti zichukuliwe kuwezesha suluhu ya mataifa mawili kwa mujibu wa maazimio ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.

Amani ni muhimu

Bwana Guterres amehitimisha akisisitiza amani, kwa njia yoyote ile, kwani ni muhimu kwa Mashariki ya Kati.

Amesisitiza udharura wa hatua, akiongeza kuwa dunia haiwezi kusubiri mabadiliko yanayohitajika.