Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vipaumbele vya Umoja wa Mataifa mwaka huu 2024

Katibu Mkuu Antonio Guterres akitoa maelezo kwa wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu kazi ya shirika hilo na vipaumbele vyake kwa mwaka 2024.
UN Photo/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu Antonio Guterres akitoa maelezo kwa wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu kazi ya shirika hilo na vipaumbele vyake kwa mwaka 2024.

Vipaumbele vya Umoja wa Mataifa mwaka huu 2024

Masuala ya UM

Leo Jumatano Februari 2, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amehutubia jumuiya ya kimataifa - wajumbe wa Baraza Kuu - na kueleza kuhusu vipaumbele vya jukumu lake akisema ulimwengu unahitaji marekebisho ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mfumo wa fedha wa kimataifa, ushiriki wa kizazi kipya katika kufanya uamuzi na Mkataba wa Kimataifa wa Kidijitali ulioundwa ili kuongeza manufaa ya teknolojia mpya na kupunguza hatari zinazohusiana nazo.

Pia amesema haja ya kuunda jukwaa kuimarisha mwitikio wa kimataifa kwa majanga ya kimataifa.

"Ninaona juhudi kubwa sana za kujenga mfumo bora zaidi, jumuishi, unaokubaliwa na hali halisi ya karne ya 21 na ulimwengu wetu unaozidi kuwa na pande nyingi." Guterres amesema.

Amani duniani

Guterres ameahidi kwamba ataendelea kufanyia kazi amani duniani. Leo, akisisitiza, maisha kwa mamilioni ya watu kwenye sayari ni kuzimu kila siku na hapo akakumbushia hali ya Ukanda wa Gaza, ambayo ni tishio kwa ukanda mzima.

"Operesheni za kijeshi za Israel zimesababisha uharibifu na kupoteza maisha ya watu huko Gaza kwa kiwango kikubwa na kwa kasi isiyo na kifani katika kipindi changu kama Katibu Mkuu." Guterres amesema.

"Hakuna kinachoweza kuhalalisha mashambulizi ya kigaidi ya kutisha yaliyotekelezwa na Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba. Hakuna uhalali wa adhabu ya pamoja kwa watu wa Palestina." Amesema.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia ametaja changamoto za kibinadamu na amani na usalama katika nchi za Sudan, Ukraine, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Yemen na Myanmar.

Ajenda ya tabianchi

Kwa kutambua kwamba janga la tabianchi linaendelea kuwa "changamoto ya uhakika ya wakati wetu", Guterres anaonya kwamba miaka michache ijayo ni muhimu kupunguza ongezeko la joto duniani hadi 1.5ºC. Kwake, enzi ya nishati ya mafuta ya kusukuku inaisha, na kuhamia kwenye nishati isiyoharibu mazingira hakuepukiki. Hata hivyo, Guterres anasema hatua zinahitajika mara moja ili kuhakikisha mchakato huo unakuwa wa haki kwa watu na sayari, pamoja na haraka vya kutosha ili kuepusha janga la tabianchi.