Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mgogoro wa ufadhili UNWRA ukiendelea raia Gaza wapekua malori kusaka mlo

Wapalestina wakiwa kwenye foleni ya kutafuta chakula kwenye mvua kwenye makazi huko Deir Al-Balah, Gaza.
© UNRWA
Wapalestina wakiwa kwenye foleni ya kutafuta chakula kwenye mvua kwenye makazi huko Deir Al-Balah, Gaza.

Mgogoro wa ufadhili UNWRA ukiendelea raia Gaza wapekua malori kusaka mlo

Amani na Usalama

Wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo ankukutana na wawakilishi kutoka nchi zinazotoa misaada kwa shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA kufuatia madai ya baadhi ya wafanyakazi wa shirika hilo kushirikiana na Hamas, shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, leo limesema sasa si wakati wa kuwatelekeza watu wa Gaza.

Licha ya mashambulizi yanayoendelea ya Israel yaliyochochewa na mashambulizi yaliyoongozwa na Hamas tarehe 7 Oktoba mwaka jana ambayo yalisababisha vifo vya watu 1,200 nchini Israel na mateka zaidi ya 250, UNRWA inaendelea kutoa msaada wa kuokoa maisha huko Gaza kwa zaidi ya raia milioni mbili.

Vita hivyo vimesababisha vifo vya Wapalestina 26,637 Gaza na wengine 65,387 kujeruhiwa, kulingana na talwimu za mamlaka ya afya ya Gaza. 

Na jeshi la Israel limeripoti wanajeshi wake 218 kuuawa na 1,267 kujeruhiwa huko Gaza tangu kuzuka kwa machafuko hayo ya karibuni.

Kama shirika kubwa zaidi la kibinadamu katika eneo hilo, UNRWA pia inaendesha makazi kwa zaidi ya watu milioni moja, kutoa chakula, maji na huduma za afya, huku pia likibeba jukumu muhimu la kuwezesha kazi za UN na mashirika mengine washirika wao huko Gaza.

"Makazi, vituo vya afya na kila kitu kingine kinatolewa Gaza kupitia UNWRA," amesema Christian Lindmeier, msemaji wa WHO

Akirudia maneno ya Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus, Bwana Lindmeier ametoa wito kwa wafadhili kutositisha ufadhili kwa UNWRA “katika wakati huu muhimu Kukata ufadhili kutawaumiza tu watu wa Gaza ambao wanahitaji kuungwa mkono.”

Marekani ilisema Ijumaa kuwa imesitisha ufadhili kufuatia tuhuma zilizotolewa dhidi ya wafanyakazi 12 wa UNRWA ambao Israel inasema walishiriki katika mashambulizi ya Oktoba 7 mwaka jana. 

Uchunguzi kamili na wa haraka unaendelea na baadhi ya wafanyakazi wanaodaiwa kuhusika wamefutwa kazi na shirika hilo.

Tishio la njaa linaendelea

Licha ya juhudi za mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika wengine wa kibinadamu wanaofanya kazi huko Gaza, watu wengi wako kwenye hatihati ya njaa baada ya karibu miezi minne ya vita.

Wengine wameamua kutafuta na kupekua misafara ya chakula na vifaa, ikiwa ni pamoja na asubuhi ya leo Jumanne katika mji wa kusini wa Khan Younis.

"Tulikuwa na msafara asubuhi ya leo tukijaribu kufikia Hospitali ya Nasser na wagonjwa, wahudumu wa afya, kila mtu pale anayehitaji chakula, lakini idadi ya kubwa ya watu wenye uhitaji tayari walifika na walichukua vifaa," amesema Lindmeier.

Ameongeza kuwa tukio hilo sio la nadra "linaonyesha jinsi mahitaji yalivyo makubwa", aliwaambia waandishi wa habari huko mjini Geneva, akionya kwamba magonjwa miongoni mwa watu wenye utapiamlo Gaza "yanaweza kuenea kama moto wa nyika na hiyo ni kutokana na mashambulizi ya mabomu na makombora na yanayoanguka kwenye majengo”.

Ndani ya Hospitali ya Nasser yenyewe, afisa wa WHO ameripoti kwamba hali "imekuwa mbaya zaidi na mashambulizi ya risasi, mapigano na ugumu wa watu kufikia Nasser au kuondoka".

Wanawake na watoto wakijihifadhi katika kituo chenye watu wengi cha UNRWA huko Khan Younis, Gaza, huku kukiwa na milio ya risasi na makombora karibu.
© UNRWA/Hussein Owda
Wanawake na watoto wakijihifadhi katika kituo chenye watu wengi cha UNRWA huko Khan Younis, Gaza, huku kukiwa na milio ya risasi na makombora karibu.

Kufurushwa tena

Haya yanajiri huku ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA ikionya kwamba watu zaidi wamefurushwa kutoka makwao huku kukiwa na mapigano yanayoendelea na maagizo ya kuhama tena kutoka kwa wanajeshi wa Israel.

"Tuko katikati ya wimbi lingine la watu kuhama Gaza, kufuatia amri za kufukuzwa katika maeneo makubwa ya makazi na huku kukiwa na mapigano mkali," OCHA imesema katika chapisho lake leo kwenye mtandao wake wa kijamii wa X, zamani Twitter. 

Imeongeza kuwa "Watu zaidi wanauawa au kujeruhiwa. Kusini mwa Gaza kumefurika watu wengi na ufikishaji wa misaada ya kibinadamu kuelekea kaskazini mwa Gaza ni mdogo sana.”